23.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi walia njaa nchi nzima

Profesa Joyce Ndalichako
Profesa Joyce Ndalichako

Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam

WANAFUNZI wa vyuo vikuu nchi nzima wanalia njaa kutokana na kupunguziwa fedha za kujikimu, MTANZANIA linaripoti.

Hali hiyo, imedhihirika baada  ya wanafunzi  wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), kulalamikia uamuzi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu(HESLB) kupunguza kiasi cha fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza kutoka Sh 510,000 hadi 19,000 kila baada ya miezi miwili.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(DARUSO), Erasmi Leon, alisema kiasi cha fedha kilichotolewa mwaka huu ni kidogo ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Leon alikutana na waandishi wa habari baada ya kufika Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa lengo la kutaka kuonana na Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako ili waweze kumweleza malalamiko yao.

Alisema hali hiyo inaweza kuwasababishia wanafunzi kuishi maisha magumu na kushindwa kufanya vizuri darasani.

Alisema wanafunzi hao, pia wamepewa Sh 7,322 kwa ajili ya gharama za stationary na vitabu wakati kipindi kilichopita walikuwa wakipewa Sh 200,000 kwa mwaka.

Alisema licha ya kupewa fedha hizo, idadi ya wanafunzi walioomba mikopo katika chuo hicho kwa mwaka huu ni zaidi ya 5,000, waliobahatika kupata mikopo hiyo ni wanafunzi 949.

“Kiasi cha fedha za mikopo kilichotolewa mwaka huu ni kidogo ikilinganishwa na miaka iliyopita, jambo ambalo linaweza kusababisha wanafunzi kuishi mazingira magumu ya kutangatanga na wanafunzi wakike kuanza kujiuza,”alisema Leon.

Alisema Serikali ilipaswa kushirikisha wadau mbalimbali  katika mfumo wa utambuzi wa kupata majina ya wanaostairi kupewa mikopo na kwa kiasi gani (mean tested) ili waweze kutoa maoni yao kuhusiana na suala hilo.

Alisema, mfumo  wa utambuzi ambao pia unahusisha mambo mawili ambayo ni pamoja na ada pamoja na vitivo maalumu,ungeweza kuzingatia vigezo vya utoaji wa utoaji wa mikopo hiyo kwa wanafunzi hao.

“Hebu fikiria kama Serikali imetoa Sh 19,000 kwa ajili ya chakula, usafiri na hiyo hiyo pia inatakiwa itumike kwa makazi, unaweza kuitumia kiasi gani ili iweze kukidhi mahitaji,?, serikali ilipaswa kuangalia upya suala hilo kabla ya kuamua kutoa mikopo,”alisema Leon.

Aliongeza, serikali ya wanafunzi imewasiliana na viongozi wa wizara ili kuzungumzia suala hilo lakini wameambia linafanyiwa kazi.

Aliwataka wanafunzi kutosaini fedha hizo kwa madai kuwa, hakuna sababu ya kuchukua fedha hizo wakati haziwezi kukidhi mahitaji.

“Ni bora kukosa fedha kabisa, kuliko kupata kiasi kidogo ambacho hakiwezi kukidhi mahitaji ya wanafunzi, Serikali inapaswa kuliangalia suala hilo kwa umakini zaidi,”alisema.

Alisema baadhi ya wanafunzi wametoka mikoani ambao wanaweza kushindwa  kwenda chuo kutokana na ukosefu wa fedha na kujikuta wanaishia mitaani kwa ajili ya kutafuta fedha.

BUGANDO

Naye Rais wa Chuo Kikuu cha Afya cha Bugando, Boniface Nyanda alisema taarifa ambazo zimeifikia serikali ya wanafunzi ni kwamba, wote wa mwaka wa kwanza wamepewa kiasi hicho cha fedha kutoka vyuo mbalimbali.

Alisema mpaka sasa kuna baadhi ya wanafunzi wanaosoma chuo Kikuu cha Afya cha KCMC ambao wamepewa mgao kama huo, jambo ambalo limewafanya kuwasiliana na viongozi wa vyuo vingine ili waweze kupata uhakika.

“Wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza kutoka vyuo mbalimbali nchini wamepewa mgao huo huo wa fedha kutoka bodi ya mikopo, hivyo basi tumepanga kuwasiliana na viongozi wetu wa chuo ili tuweze kujadili suala hili kwa kina na kuwasilisha malalamiko yetu serikalini,”alisema Nyanda.

Hata hivyo, Ambele Gredson ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza, alisema  uamuzi wa kupunguza fedha za mikopo umewasikitisha sana kwa sababu wanafunzi wengi wao wanatoka katika familia duni ambazo haziwezi kukidhi matakwa ya kusoma.

SAUT

Kwa upande wake, Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo cha Mtakatifu Agustine (SAUT),  Emanuel Ayo alisema bado hajapata taarifa za wanafunzi waliopewa mikopo katika chuo hicho kwa sababu wamefungua chuo wiki hii.

Alisema kutokana na hali hiyo, wanasubili wanafunzi wamalize kujisajili ndipo wajue idadi ya walioomba mikopo na wale waliobahatka kupewa ili wajue ni kiasi gani cha fedha walichopewa na bodi ya mikopo.

“Tumefungua chuo wiki hii, mpaka sasa wanafunzi wa mwaka wa kwanza bado wanaendelea kujisajili, hivyo basi kupata takwimu rasmi za wanafunzi walioomba mikopo na wale waliobahatika kupata ni vigumu mpaka wanafunzi wote watakapoanza masomo yao,”alisema Ayo.

CHUO CHA MAJI

Naye Rais wa Chuo cha Taasisi ya  Maji, Barnabas Aligunga, alisema kama ilivyo katika vyuo vingine nao pia wamekumbwa na changamoto hiyo na tayari wanajipanga kutoa tamko.

TAHLISO

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Shrikikisho la Vyuo Vikuu Tanzania (TAHLISO),Stanslaus Kadugalize alisema tatizo la utoaji wa fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa elimu ya juu, limefikishwa kwenye bodi na kwamba upangaji utafanyika upya baada ya uliopo kuonekana kuwa na dosari.

Alisema upangaji wa sasa ulifanyika kwa kuangalia asilimia ya mkopo aliopata mwanafunzi suala lililosababisha wenye asilimia ndogo kupata kiasi kidogo.

Alisema upangaji huo umeathiri wanafunzi wa mwaka wa kwanza tu na kwamba upangaji mpya wa fedha hizo utatolewa Jumatatu ijayo.

“Ni vyema wanafunzi wavute subira kwa sababu tumeshakutana na Bodi ya Mikopo pamoja na Waziri wa Elimu, Mafunzo ya Ufundi, Sayansi na Teknolojia na tumekubaliana kuwa upangaji ufanywe upya na kufikia Jumatatu ijayo utakuwa umekamilika,” alisema Kadugalize

TCU

Nayo Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania(TCU), imeongeza siku tatu za kufanya maombi ya kujiunga na vyuo vikuu ikiwa ni awamu ya nne kutokana na kuwapo kwa nafasi, huku idadi kubwa ya waombaji wenye sifa wakikosa nafasi walizoomba awali.

Kaimu Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka wa TCU, Dk. Kokubelwa Katunzi aliliambia gazeti hili jana, kuwa maombi yataanza kupokewa Oktoba 24 hadi Oktoba 26  mwaka huu.

“Tumetoa nafasi ya kuomba tena vyuo kwa awamu ya nne kwasababu katika awamu ya tatu iliyoishia Oktoba 16 mwaka huu, waombaji 1,119 wamepata nafasi lakini wapo wengine 4,500 ambao wapo kwenye mfumo wamekosa nafasi licha ya kwamba wana sifa na vyuo vina nafasi,” alisema Dk. Kokubelwa.

Akielezea sababu za waombaji kukosa nafasi huku kukiwa na nafasi katika vyuo alisema inatokana na uelewa mdogo wa waombaji kuhusu kile wanachotaka kwenda kusomea kulingana na masomo waliosoma kidato cha sita.

Akitolea mfano wa programu ya udaktari alisema wanafunzi 10,000 waliomba huku vyuo vinavyotoa programu hiyo vikiwa na nafasi 2,500 tu.

Imeandaliwa na Patricia Kimelemeta, Leonard Mang’oha na Jonas Mushi

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles