TELEVISHENI ya NBC ya Marekani imemfuta kazi mtangazaji Billy Bush ambaye amekuwa akiendesha kipindi cha Today kutokana na kumhoji Mgombea wa urais wa Republican, Donald Trump, miaka 10 iliyopita.
Katika mahojiano hayo, Trump alitoa matamshi ya kuwadhalilisha wanawake, kashfa ambayo hivi sasa inamwandama katika kampeni zake za kugombea urais.
Mkanda wa mahojiano hayo yaliyofanyika mwaka 2005 ulifichuliwa juzi na gazeti la Washington Post.
Baada ya kufichuliwa mkanda huo, viongozi wengi wakuu wa Chama cha Republican walijitenga na Trump suala ambalo limezua utata.
Kwenye video hiyo, Bush anasikika akicheka baada ya matamshi ya Trump.
Bush ambaye ni mpwa wa rais wa zamani wa Marekani, George Bush, awali alisimamishwa kazi baada ya kufichuliwa video hiyo.
Kutokana na hali hiyo, Bush amekuwa mtangazaji wa kipindi cha Today kwa miezi miwili pekee.
“Ingawa alikuwa mgeni tu katika waandaaji wa kipindi cha Today, amekuwa na NBC kwa muda mrefu. Tunamtakia kila la heri,” ilisema televisheni hiyo katika taarifa yake.
Mke wa Donald Trump, Melania, amemshutumu Bush akisema alimchochea mumewe kusema mambo mabaya kuhusu wanawake.
Bush mwenyewe aliomba radhi Oktoba 7 mwaka huu na kusema binafsi aliaibishwa na tabia yake alipokuwa akifanya mahojiano hayo.