23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

JK, Lowassa wakutana

jk-lowassa*Ni baada ya kuachana kwa mwaka mmoja wakiwa CCM

*Wasalimiana kwa bashasha, JPM ataja wake wa Masaburi

JONAS MUSHI Na FERDNANDA MBAMILA

-DAR ES SALAAM

WAMEKUTANA ndivyo unaweza kusema. Hatimaye mazishi ya kuuaga mwili wa Meya wa zamani wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, yamewakutanisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kwa kusalimiana na kushikana mikono.

Tukio hilo la aina yake liliwafanya watu mbalimbali waliokuwa katika msiba huo kubaki wakishangaa, hasa baada ya Rais mstaafu Kikwete kumfuata Lowassa na kumwuliza hali rafiki yake huyo wa zamani waliokulia wote CCM.

Tangu wakati huo viongozi hao ambao walikuwa marafiki wa karibu tangu ujana wao walikuwa wakirushiana vijembe ambapo jana walikutana ana kwa ana katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam wakati wa kuuaga mwili wa Dk. Masaburi kabla ya kwenda kuzikwa nyumbani kwake Chanika Manispaa ya Ilala.

Akiwa katika viwanja hivyo, Kikwete alipomwona Lowassa akiingia viwanjani hapo alinyanyuka na kumfuta Lowassa katika kiti chake kisha kusalimiana naye kwa kupeana mikoni huku wakizungumza.

Lowassa aliyekuwa ameketi jirani na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana pamoja na mkewe Regina Lowassa, alisimama na kumjibu salamu.

MTANZANIA ilimtafuta Lowassa na kutaka kujua alichozungumza na Rais mstaafu Jakaya Kikwete ambapo alisema. “Ni kweli nimesalimiana na Jakaya amenisalimia Assalam Aleykum nami nikamjibu. Kisha akaniuliza hujambo nikamjibu sijambo. Nami nikamuliiza je nawe hujambo akasema hajambo basi kila mmoja akaendelea na shughuli iliyotupeleka ya msiba,” alisema Lowassa.

Kwa muda mrefu wanasiasa hao ambao wamewahi kuwa marafiki hadi kupewa jina la utani ‘Boys II Men’, waliingia katika uhasama kwa kile kinachodaiwa ni kusalitiana kisiasa.

Urafiki wa wawili hao ulianza kuingia doa mwaka 2008 wakati wa kashfa ya Richmond iliyosababisha Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu kwa kile alichoeleza ni kunyimwa haki ya kusikilizwa baada ya kuibuka kwa kashfa hiyo kwa kile alichodai ilikuwa ni vita ya kutaka ‘uwaziri mkuu’.

Ukaribu wa Lowassa na Kikwete uliendelea kupungua na kuwa shakani zaidi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana baada ya Lowassa kukatwa jina lake katika kinyang’ anyiro cha kuwania nafasi ya kugombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuamua kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kwa takribani mwaka mmoja sasa tangu mchakato wa ndani wa CCM wa kumpata mgombea wake wa urais Julai 10, mwaka jana umalizike wawili hao hawajawahi kukutana hadharani na kupeana mikono.

Katika mchakato huo Kamati Kuu ya CCM iliyokutana hadi usiku wa manane iliibuka na jibu kwamba, jina la Edward Lowassa limekatwa katika watu wanaowania urais kupitia chama hicho.

Waliopitishwa na kuingia tano bora na Kamati Kuu walikuwa ni Bernard Membe, Dk John Magufuli, Dk Asha Rose Migiro, January Makamba na Amina Salum Ali, huku makada wengine 33 wakitupwa akiwamo Lowassa.

Kutokana na hali hiyo Lowassa alichukua aumuzi mzito wa kuihama CCM, Julai 28, mwaka jana na kujiunga na Chadema na hatimaye kuteuliwa kuwa mgombea urais kupitia chama hicho cha upinzani akiungwa mkoano na vyama vinaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

JPM na familia ya Masaburi

Katika hali ya kushangaza msiba huo uligeuka kuwa furaha kwa waombolezaji kutokana na maneno yaliyotolewa na Rais Dk. John Magufuli baada ya kupewa nafasi ya kutoa neno la pole kwa familia ya Masaburi.

Ule usemi wa msibani hakuna kupigiwa makofi jana ulibadilika baada ya Rais Magufuli kufichua kile kilichofichwa na mdogo wa marehemu, Fowe Masaburi, wakati akisoma wasifu wa marehemu kaka yake.

Katika wasifu huo Fowe alisema marehemu alifunga ndoa na Janeth Masaburi na kwamba ameacha watoto 20 na wajane ambao hakutaja idadi yao.

Licha ya Rais Magufuli pia waombolezaji walionekana kushangaa kitendo hicho kwani baada ya kusoma kipengele hicho iliibuka minong’ono iliyodumu kwa dakika kadhaa kabla ya mshereheshaji kuwatuliza waombolezaji kwa kuwataka wanyamaze.

Kutokana na kitendo hicho Rais Magufuli alianza kutoa neno lake kwa kusema kwamba licha ya kutajwa mke mmoja kwenye wasifu yeye anafahamu kuwa marehemu alikuwa na wake zaidi ya wanne hadi watano.

Kauli hiyo ya Rais Magufuli ilisababisha waombolezaji wapige makofi huku wengine wakiangua kicheko na baadhi walisikika wakisema ‘amekata mzizi wa fitina’.

“Nimesikia kwenye wasifu kuwa marehemu alikuwa na mke mmoja lakini mimi nafahamu alikuwa na wake zake ni wanne hadi watano. Kwa familia zetu za Afrika kuwa na wake zaidi ya mmoja ni jambo la kawaida na hata Mfalme Sulemani alikuwa na wake 1000 na ameandikwa kwenye vitabu vyote vya dini,” alisema Rais Magufuli huku waombolezaji wakimpigia makofi na kuangua vicheko.

“Nawapa pole wake wote wa marehemu pamoja na watoto wote hapa wametajwa 20 lakini nafahamu wanaweza kuwa zaidi ya hao,”.

Kutokana na hali hiyo Rais Magufuli alitoa wito kwa familia hiyo kutomkaribisha shetani ndani ya familia kwa kuhakikisha hawafarakani.

“Nitoe wito kwa wanafamilia hususani watoto baba yenu aliwapenda wote bila kuwabagua na ndio maana alichagua kuzikwa sehemu ya wote.

“Mtoto mkubwa aliyezaliwa wa kwanza na marehemu ajue yeye ndiye kiongozi wa familia na mjue mkishikamana ninyi hata mama zenu watashikamana pamoja na ndugu wengine,” alisema Rais Magufuli.

Akimwelezea Dk. Masaburi alisema alimfahamu kama rafiki, ndugu na mpiganaji wa CCM na kwamba historia yake haiwezi kufutika hususani katika historia ya jiji la Dar es Salaam.

“Alikuwa ni mtu wa watu na umati huu ni ushahidi tosha kwamba atakumbukwa na wengi katika historia yake kutokana na upendo na mambo aliyowafanyia watu,” alisema Rais Magufuli.

VIONGOZI WALIOHUDHURIA

Mbali na Rais Magufuli, Lowassa na Rais mstaafu Kikwete viongozi wengine waliohudhuria ni Makamu wa Rais Mstaafu, Dk. Mohamed Gharib Bilal, Spika Mstaafu Anne Makinda, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi pamoja na wabunge na mawaziri.

Wengine ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Mkuu WASIFU WA MAREHEMU

Dk. Masaburi alizaliwa Machi 24 mwaka 1960 na alisoma Shule ya Msingi Nseke iliyopo Serengeti na mwaka 1978 alijiunga na Sekondari ya Wavulana ya Tabora na kuhitimu mwaka 1981.

Mwaka 1982 Dk. Masaburi alijiunga na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na kuhitimu mwaka 1985 na kupata cheti cha ufundi wa magari.

Mwaka 1985-1990 alichukua mafunzo ya ugavi na kupata Shahada ya Ununuzi na Ugavi kutoka  Bodi ya Ugavi wakati huohuo akichukua mafunzo ya ununuzi na ugavi nchini Uingereza Chuo cha Chartered Institute of Purchasing and Supply ambapo alitunikiwa cheti cha Diploma ya juu ya Ununuzi na Ughavi mwaka 1988.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles