NA BEATRICE KAIZA, DAR ES SALAAM
WASANII kutoka mataifa mbalimbali wamejishindia tuzo za African Muziki Magazine Awards (Afrimma) kwa mwaka huu, ambapo kwa Tanzania wasanii watatu wamenyakua tuzo hizo.
Wasanii Watanzania walioshinda tuzo hizo zilizotolewa Dallas Texas, nchini Marekani ni Dj D Ommy kutoka Clouds FM aliyeshinda tuzo ya Dj bora Afrika, tuzo ya msanii bora chipukizi Afrika 2016 imekwenda kwa Harmonize, huku msanii bora wa kiume Afrika Mashariki akitangazwa kuwa ni Diamond Platnumz.
Tuzo nyingine imekwenda kwa Wakenya, Sautisol wakinyakua tuzo ya kundi bora la muziki Afrika, Akothee akishinda msanii bora wa kike Afrika Mashariki na mkali wa muziki wa Injili, Willy Paul akishinda tuzo ya ‘Best Gospel Act’.
Tuzo nyingine ni ya wimbo bora wa mwaka wa msanii Tecno ‘Duro’ kutoka Nigeria, Flavour wa Nigeria akaibuka msanii bora wa mwaka, Msanii bora Afrika Magharibi ikienda kwa Olamide, huku Patrick Elis akiibuka kuwa muongozaji bora wa video za wasanii.
Washindani wa mshindi katika kipengele cha msanii bora wa kiume Afrika Mashariki ni Eddy Kenzo kutoka Uganda, Jacky Gosee kutoka Ethiopia, Ali Kiba kutoka Tanzania, Jose Chameleon kutoka Uganda, Bebe Cool kutoka Uganda, Sauti Sol kutoka Kenya, Dynamq kutoka South Sudan na Diamond Platnumz kutoka Tanzania.
Waliokuwa washindani wa mshindi kipengele cha msanii bora chipukizi ni Adekunle Gold kutoka Nigeria, Falz kutoka Nigeria, Locko kutoka Cameroon, Nathi kutoka South Africa, Kofi Kinaata kutoka Ghana, Humblesmith kutoka Nigeria na Harmonize kutoka Tanzania.
Pia waliokuwa washindani wa kipengele cha DJ bora Afrika ni Dj Spinall kutoka Nigea, Dj Joe Mfalme kutoka Kenya, Cndo kutoka Africa Kusini, Dj Neptune kutoka Nigeria, Dj Malvado Jnr kutoka Angola, Dj Labastille kutoka Cameroon na DJ D-Ommy kutoka Tanzania.