Ethiopia imetangaza hali ya dharura itakayodumu kwa miezi sita kufuatia mlolongo wa maandamano dhidi ya serikali.
Maandamano hayo yaliendeshwa na makabila mawili makubwa nchini hapa, Oromo na Amhara, ambayo yanalalamika kutengwa na serikali kiuchumi na kisiasa.
Ghasia baina ya waandamanaji na polisi zilizidi tangu watu 55 walipokufa katika sherehe za kitamaduni za Oromo, Jumapili iliyopita.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema, mamia ya watu wameuawa, na maelfu kukamatwa tangu maandamano yalipoanza.
Wakati huo huo, Serikali ya Ethiopia imeishutumu Misri kwa kile ilichodai iko nyuma ya mandamano na machafuko yanayotokea hapa, tuhuma, ambazo taifa hilo la kaskazini mwa Afrika limekana.