Clinton, Trump washambuliana vikali

0
568
Mgombea urais wa Marekani kutoka Chama cha Republican, Donald Trump (kushoto) akimnyooshea kidole mpinzani wake kutoka Democratic, Hillary Clinton wakati wa mdahalo wao wa pili mjini St. Louis juzi

mdahaloWASHINGTON, MAREKANI

WAGOMBEA urais wa Marekani Hillary Clinton na Donald Trump walitumia sehemu kubwa ya mdadahalo wao wa pili usiku wa kuamkia jana kushambuliana vikali.

Tofauti na mdahalo wa kwanza alioshindwa, safari hii mgombea urais kwa tiketi ya Republican, Trump alionesha uhai zaidi, akimshambulia mpinzani wake huku akitishia kumfunga jela, iwapo atashinda urais.

Trump alimshutumu Clinton kwa kile alichokiita uozo wa kimaadili wa mumewe na Rais wa zamani Bill Clinton.

Mdahalo huo pia ulishuhudiwa na Bill Clinton mwenyewe na wanawake wanne wanaodai kutendwa udhalimu na Clinton.

Wakiwa wamekwepa kupeana mikono, mahasimu hao waliingia katika jukwaa la mdahalo la St. Louis, Missouri, ambapo ghafla walitupiana maneno makali kuhusu video iliyosambazwa Ijumaa iliyopita.

Katika video hiyo, Trump alisikika kwa sauti kubwa akijigamba namna alivyokuwa akiwadhalilisha wanawake ikiwamo kuwashika sehemu zao za siri.

Mmoja kati ya waendesha mdahalo huo, Anderson Cooper alimwambia ‘unajivunia kudhalilisha wanawake kingono’.

Kabla ya kubadili mada kuanza kuzungumzia mkakati wa kukabiliana na kundi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS), Trump alijitetea “Hapana sikusema hivyo hata kidogo, nafikiri hukuelewa ilivyokuwa, haya yalikuwa mazungumzo ya mzaha tu, sijivunii jambo hilo, naomba msamaha kwa familia yangu, naomba msamaha kwa watu wa Marekani. Kwa hakika sioni fahari ya jambo hilo.”

Trump aliitumia kashfa hiyo kuelekeza hasira kwa mume wa Hillary Clinton.

“Hakuna mtu kama huyu katika historia ya siasa ambaye amewanyanyasa wanawake kiasi hiki. Mimi niliongea tu kimzaha, Bill Clinton alitenda kabisa unyama huu na mkewe Clinton aliutetea,” alisema.

Hillary Clinton alikataa kujibu tuhuma hizo, ambazo hazijathibitishwa.

Baadaye Trump akabadili mada akisema anapaswa kujikita katika masuala muhimu ambapo akajigamba kuishinda IS.

Lakini muongoza mdahalo alimrudisha katika mada kwa kumhoji ‘umewahi kufanya mambo hayo?” Trump akajibu ‘Hapana, sijawahi.’

Tangu Ijumaa iliyopita maafisa kadhaa mashuhuri wa chama chake cha Repulican, wakiwemo baadhi ya wabunge walijitenga naye kufuatia video hiyo iliyorekodiwa mwaka 2005.

Kashfa hiyo ilikuwa fimbo muhimu kwa mgombea wa chama cha Democratic, Hillary Clinton ya kumchapia mpinzani wake.

“Donald Trump ni tofauti, nilisema hivyo tangu Juni mwaka huu kuwa hafai kuwa rais na amiri jeshi mkuu. Na wengi kutoka vyama vya Republican na Independent wamesema jambo hilo hilo. Kile tulichokiona na kusikia Ijumaa, kinaonesha namna Donald anavyowachukulia wanawake, anavyowafikiria na inaonesha dhahiri jinsi alivyo, “ alisema.

Katika mdahalo huu Trump aliondoa ile kauli yake ya awali ya kudhibiti wahamiaji wa Kiislamu, badala yake ametaka kufanyike uchunguzi mkali wa kuwachuja wale wenye msimamo mkali wanaotaka kuingia Marekani.

Lakini Clinton alimtuhumu moja kwa moja kwa kusema mambo mabaya na yenye kuleta mgawanyiko dhidi ya Waislamu.

Aidha aliongeza kuwa imekuwa vizuri kwa mtu mwenye mhemko kama ya Trump si msimamizi wa sheria za nchini hiyo, jambo ambalo lilimfanya Trump amjibu hapo hapo kwa kumwambia ‘ungekuwa gerezani.’

Trump alikuwa akirejea kashfa ya kutumia barua pepe binafsi katika masuala ya kitaifa, ambayo Clinton mara kadhaa alikiri makosa.

Pamioja na kwamba Trump alionesha uhai zaidi katika mdahalo huo tofauti na ule wa kwanza, huku Clinton akidorora kinyume na matarajio ya wengi, wachambuzi wengi makini bado wamempatia Clinton ushindi.

Ushindi huo umeelezwa kuchochewa na uzoefu wake serikalini pamoja na kuonesha kustahimili mashambulizi ya Trump, ambayo yamehesabiwa yalilenga kupoteza malengo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here