30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Omog kutumia mfumo wa Azam kuiua Mbeya City

img_3357

WINFRIDA NGONYANI NA THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

KOCHA mkuu wa timu ya Simba, Joseph Omog, amesema atatumia mbinu na uzoefu alioupata katika mechi za ugenini wakati akiifundisha Azam FC, ili kukabiliana na ugumu wa mechi yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City.

Omog raia wa Cameroon, amepanga kutumia mbinu zilizoiwezesha Azam kushinda ungenini na kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu wa 2013/14 ili kuwamaliza Mbeya City.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Omog alisema anafahamu changamoto za timu kucheza ugenini, lakini anaamini uzoefu alioupata wakati akiinoa Azam utamsadia kuendeleza rekodi ya ushindi na kuendelea kubaki kileleni.

Alisema matumaini ya Simba kutwaa ubingwa msimu huu yanaonekana wazi, kwa kile alichodai kuwa wachezaji wamekuwa wepesi kufuata maelekezo anayowapa na kufanya mfumo wa ufundishaji kuwa rahisi zaidi.

“Naelewa mechi za ugenini zinavyokuwa na changamoto nyingi, lakini nitaandaa kikosi imara ambacho kitapambana kuzikabili ili tuendeleze rekodi yetu ya ushindi msimu huu,” alisema.

Alisema hii ni mara yake ya kwanza kuifundisha Simba ambayo anafahamu wazi haina rekodi ya kunyakua ubingwa kwa misimu minne mfululizo, hivyo kwa kushirikiana na kocha msaidizi, Jackson Mayanja, watahakikisha malengo hayo yanafikiwa na kuwapa faraja mashabiki.

Akielezea sababu ya kikosi hicho kusafiri mapema kwenda jijini Mbeya, kocha huyo alisema lengo ni kuwapa wachezaji muda wa kuzoea mazingira ya hali ya hewa kabla ya kuvaana na wenyeji wao Mbeya City.

“Wachezaji walifanya mazoezi mepesi ya kuwaweka sawa wakati tukiwa jijini Dar es Salaam, lakini baada ya kuwasili Mbeya, programu imebadilika na kuanza kufanya mazoezi ya nguvu ambayo yatawazidishia ukomavu,” alisema.

Kwa sasa, Simba ndio vinara wanaoongoza katika  msimamo wa ligi kuu kwa kufikisha pointi 17, ikiwa imeshuka dimbani mara saba na kushinda michezo mitano na kulazmishwa sare mara mbili.

Kwa upande wake kocha mkuu wa Mbeya City, Mmalawi Kinnah Phiri, alisema kikosi cha wapinzani wao Simba hakina tofauti na timu nyingine walizokutana kwenye ligi hiyo, hivyo anaamini ushindi utabaki nyumbani.

Alisema hawawezi kupata hofu ya mchezo kutokana na wapinzani wao kuongoza pamoja na kikosi chao kusheheni wachezaji wazuri wa kimataifa, kwani wachezaji wake sasa wameimarika zaidi tofauti na awali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles