Na CLARA MATIMO-MWANZA
ASILIMIA 90 ya eneo la Wilaya ya Ilemela Mkoa wa Mwanza, haijapimwa ingawa wananchi wake wanaishi katika makazi yaliyoendelezwa.
Hayo yamebainishwa jijini Mwanza jana na Meneja Mradi wa Uboreshaji Nyumba na Makazi Wilaya ya Ilemela unaotekelezwa na Shirika lisilo la Serikali la TAHEA kwa ufadhili wa W-Effect la nchini Sweden, Musa Masongo, wakati akizungumza katika kongamano la kujadili fursa ya utawala mpya katika kumiliki ardhi na changamoto zake.
Alisema Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, katika hotuba yake ya bajeti 2016/17 kwa kutambua changamoto zilizopo katika sekta ya wizara yake.
Lukuvi aliziagiza halmashauri zote na wataalamu washushe ramani za mipango miji katika ngazi ya mitaa ili wananchi wajue ni nini kimepangwa kujengwa katika maeneo wanayotaka kujenga, lakini hadi sasa halijatekelezwa kikamilifu.
“Hebu fikiria mwananchi huyu ninayemzungumzia ni wa kipato cha chini kuelekea cha kati ambaye kipato chake kwa siku ni Sh 5,600 anajinyima anajenga nyumba katika eneo ambalo halijapimwa baada ya muda anaambiwa hapo alipojenga si makazi ya watu anabomolewa halafu halipwi fidia kwa wakati jamani huu umaskini tutapambana nao vipi?,” alihoji Masongo na kuongeza.
“Tumeandaa kongamano hili ili kukutana na wenyeviti wa mitaa na watendaji wa kata jumla 50 lengo ni kujadili fursa zilizopo katika utawala huu wa awamu ya tano kwenye suala zima la kumiliki ardhi na changamoto zake,” alisema.
Alisema kama mwananchi hana ardhi iliyorasimishwa hawezi kuwa rafiki wa benki kwa kuwa ili kupata mkopo lazima awe na dhamana, hivyo dhamira ya serikali ya kuboresha maisha ya watu wake inaweza ikatekelezwa kwa urahisi endapo watapimiwa ardhi na kumilikishwa rasmi.