32.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Pinda aweweseka na Ukawa

Waziri Mkuu Mizengo Pinda
Waziri Mkuu Mizengo Pinda

Amina Omari na Oscar Assenga, Tanga

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, kwa mara nyingine amesema maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu yanaendelea, huku hatma yake ikibaki kutegemea kukamilika kwa mchakato wa Katiba Mpya.

Amesema ili kuweza kuwa na uchaguzi mzuri, ni muhimu kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurejea ndani ya Bunge hilo.

Kauli hiyo aliitoa jana jijini Tanga, alipokuwa akizungumza na Mameya wa Majiji, Manispaa na Wenyeviti wa Halmashauri za Miji na Wilaya Tanzania katika kikao cha siku moja, ambapo aliwasihi tena Ukawa kurejea katika Bunge la Katiba ili kuweza kumalizia mchakato wa kupata Katiba Mpya.

“Uchaguzi wa Serikali za Mitaa bado ni kitendawili kwa sababu kwa kiasi kikubwa inategemea sana kukamilika kwa Mchakato wa Bunge la Katiba.

“Kama Wizara tunaendelea na maandalizi tukiamini uchaguzi upo, kama hiyo fursa isipotokea bado tutakuwa tumekamilisha maandalizi kwa upande wetu. Tunaendelea kuandaa kanuni kwa kushirikisha wadau wote,” alisema.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kusisitiza suala la ukusanyaji mapato na udhibiti wa matumizi ya fedha za Serikali.

Kuhusu mapato, Waziri Mkuu alisema katika mwaka wa fedha unaokwisha sasa, hali ya ukusanyaji mapato haikuwa nzuri.

Pamoja na hali hiyo, alisema amewaandikia barua Wakuu wa Mikoa akiwataka waweke utaratibu wa kutoa taarifa kila baada ya miezi mitatu juu ya makusanyo ya kila Halmashauri zilizo kwenye mikoa yao.

Wiki iliyopita alipokuwa akiahirisha kikao cha Bunge la Bajeti mjini Dodoma, pamoja na mambo mengine, Waziri Mkuu aliwasihi Ukawa kurejea katika Bunge la Katiba ili kukamilisha mchakato wa kuwa na Katiba Mpya.

Alisema Serikali itaendelea kufanya mazungumzo na Ukawa iweze kurejea kwenye vikao vya Bunge la Katiba kwa ajili ya kusaidia kupatikana katiba mpya kuhakikisha uchaguzi wa serikali za mitaa unafanyika kwa wakati.

Pinda alisema licha ya upungufu uliopo kwa baadhi ya wajumbe kujitoa kwenye Bunge hilo, bado serikali itaendelea na jitihada za kuhakikisha wajumbe hao wanarejea kuendelea na mchakato wa kupata katiba mpya.

Alisema jambo hilo ni muhimu, hasa kwa mustakabali wa taifa na wananchi wake kwa ujumla kwa sababu itakuwa vizuri Katiba hiyo ipatikane ambayo itaweza kutoa mwelekeo wa utendaji na utawala katika nyanja mbalimbali.

“Serikali kwa upande wetu tutaendelea kuwasihi na kuwaomba warejee katika mchakato huo muhimu ili wakamilishe kazi ambayo wameianza kwa sababu uwepo wao ni kwa niaba ya wananchi ambao hawakupata fursa ya kuingia kwenye bunge hilo,” alisisitiza Pinda.

Alisema wizara inaendelea na taratibu zake ikiamini uchaguzi wa kuwapata viongozi wa mitaa, kata na vijiji upo na Katiba Mpya itapatikana kwa wakati uliopangwa kutoa fursa ya shughuli za maendeleo kuendelea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles