NA HADIA KHAMIS-DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amesema Sh bilioni 2 zimerudishwa kati ya Sh bilioni 3.8 za fedha za mikopo zilizotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kwa wanafunzi hewa kwa mwaka wa masomo 2015/2016.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Profesa Ndalichako alisema urejeshaji wa fedha hizo umetokana na agizo alilolitoa Agosti 7, mwaka huu la kuvitaka vyuo 31 kati ya 81vya elimu ya juu kurudisha fedha hizo.
Licha ya kurudishwa fedha hizo, Waziri Ndalichako amesema kuna walimu wengine wameomba kurudisha Sh milioni 600 kwa awamu.
“Tayari Sh bilioni 2 zimerudishwa serikalini kati ya Sh bilioni 3.8, natarajia kupokea tena Sh milioni 600 ambazo walimu wa vyuo husika wameomba kurejesha taratibu,”alisema Profesa Ndalichako.
Alisema bado uhakiki wa wanafunzi unaendelea kufanywa kwa sababu wengine wakati kazi hiyo inaendelea hawakuwapo vyuoni.