Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL), Mohamed Dewji ‘Mo”, ameibuka kidedea, baada ya kutangazwa kushinda tuzo ya Kiongozi Bora Kijana wa Biashara Afrika.
Dewji ametangazwa na taasisi ya Choiseul 100 Afrika yenye makao makuu Paris, Ufaransa.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana, ilisema Taasisi ya Choiseul 100 Afrika imetoa tuzo hiyo kwa mwaka wa tatu mfululizo kwa viongozi vijana wenye ushawishi katika biashara barani Afrika inayojulikana kama ‘Choiseul 100 Africa: Viongozi wa Uchumi wa Kesho.
Tuzo hiyo hulenga kutambua wafanyabiashara wenye ushawishi na kuchangia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Afrika na ambao ni mfano wa kuigwa kwa ajili ya kulifufua bara hilo.
Katika orodha ya 2016, Dewji ameshika nafasi ya kwanza kati ya viongozi vijana wa biashara 100.
Kwa miaka kadhaa, Taasisi ya Choiseul imekuwa kichocheo cha kuleta mabadiliko makubwa na kukua kwa fursa na vipaji barani Afrika.
Utambuzi wa Mo katika tuzo hiyo kunatuma ujumbe mkubwa wa matumaini kwa Tanzania na Afrika kuwa bara linazidi kujihusisha katika kuchochea ukuaji wake na watu wake.
Watu wanaoingia katika Choiseul 100 Africa ni wale wenye sifa za kuwa na utaifa katika moja ya nchi 54 za Afrika, umri wa miaka 40 au chini ya hapo kufikia Januari mwaka huo.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Dewji alisema: “Nimepata heshima kubwa na nina furaha ya kupokea hadhi hii kwa kutambua kazi ambayo nimekuwa nikiifanya barani Afrika.
“Katika safari yangu yote ya ujasiriamali nimekuwa nikiendelea kuboresha tasnia ya biashara…Kupitia MeTL nitaendelea na dhamira yangu ya kuiendeleza Afrika kupitia sekta binafsi”.
Alisema MeTL inaendelea kupanua himaya katika ukanda wake baada ya kuwekeza katika nchi 11 na miradi mipya ya biashara ikiwamo uanzishaji wa benki ya biashara, kiwanda cha utengenezaji sukari, nguo.
Hivi karibuni alichukua hisa nyingi katika klabu kubwa ya mpira Tanzania, Simba Sports Club (SSC).
Watanzania wengine waliochomoza katika tuzo hizo za mwaka huu ni Elsie Kanza, Mkuu wa Afrika wa Jukwaa la Uchumi wa Dunia (WEF), Luca Neghesti, Mwasisi wa Bongo5 Media Group, Edha Nahdi, Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Amsons Group na Moremi Marwa, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE).