TUNU NASSOR NA MAULI MUYENJWA, DAR ES SALAAM
WATANZANIA wanaokwenda kufanya kazi za ndani Mashariki ya Kati wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na mazingira magumu ya kazi.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya kati wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Abdallah Kilima alipokuwa akitoa ufafanuzi wa taarifa za wafanyakazi hao kuteswa zilizoandikwa kwenye gazeti moja (siyo MTANZANIA)
Kilima alisema changamoto za mazingira wanayokutana nayo zinasababisha kujisikia kunyanyasika na kuteswa na mabosi wao.
“Watu wengine wanaona ni fursa kwenda Oman kufanya kazi lakini hana ujuzi wa kazi hiyo, na kuna wengine hawana ujuzi wa kutumia mashine za kufulia, anakosea na kuweka kwenye jiko la oven.
“Kwa hali ya kawaida ni lazima kutakuwa na matatizo katika utendaji wake wa kazi ambao hautamfurahisha bosi wake.
“Mazingira ya hapa kwetu mfanyakazi wa ndani amezoea kufanya kazi kidogo, anapumzika na kwenda kuongea na majirani lakini kule mambo hayo hakuna kazi ni nyingi.
“Huku amezoea akipika chakula kimoja wanakula familia nzima lakini huko nje kila mmoja anaweza kutaka kupikiwa chakula anachopenda pamoja na kufanyiwa kazi zake hivyo hawapati muda wa kupumzika na hivyo kuhisi wananyanyasika,” alisema Kilima.
Alisema changamoto nyingine ni ya utamaduni kama katika suala la uhuru wa kuabudu ambako kama ni mkristo atalazimika kusali Ijumaa au Jumamosi na Jumapili inahesabika siku ya kazi.
“Kuna mambo ambayo huku ni ya kawaida lakini kule ni makosa ya jinai.
“Kwa mfano huku ni suala la kawaida kuwa na uhusiano wa mapenzi lakini kule ni jinai ingawa pia inatokea wafanyakazi hao wakawa wanatongozwa na watoto wa mabosi wao au bosi mwenyewe lakini kesi kama hizo tunapozipata zinashughulikiwa,” alisema Kilima.