Na ELIZABETH HOMBO,
MGOGORO unaofukuta ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) ukichochewa na uamuzi wa Profesa Ibrahim Lipumba aliyejiuzulu uenyekiti kwa hiyari yake Agosti mwaka jana kutaka kurejea kwenye nafasi hiyo, unaonekana kusahaulisha machungu ya mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar.
Itakumbukwa kabla ya mgogoro huo unaokitafuna CUF, mjadala mkubwa ulikuwa ni kuhusu hali ya kisiasa visiwani Zanzibar huku aliyekuwa mgombea urais kupitia chama hicho, Maalim Seif Sharrif Hamad akizunguka katika mataifa mbalimbali akidai haki yake.
Baada ya kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, Maalim Seif alipinga matokeo hayo huku mara kadhaa akisisitiza kuwa tume hiyo imtangaze kuwa mshindi.
Pamoja na hilo lakini baadaye ukafanyika uchaguzi wa marudio Machi 20 mwaka huu na kumbakiza madarakani Rais Dk. Ali Mohamed Shein.
Kuibuka kwa mgogoro wa sasa ndani ya CUF, inaonekana wazi kwamba unaudhoofisha harakati zilizokuwapo awali za kudai kile kilichotokea Zanzibar kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu, ambapo chama hicho kilisusia.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini wanaeleza bayana kuwa kuendelea kupamba moto kwa mgogoro huo ndani ya CUF huenda ukapoza joto la mvutano wa chama hicho na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuhusu madai ya kuporwa ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana.
Yapo mengi ambayo yanasemwa lakini ni wazi kwa wakati huu ambao CUF wanatumia muda mwingi kwenye mgogoro wao huo, wanaweza wakasahau machungu ya Zanzibar na CCM kutumia mwanya huo kuendelea kupeta.
Hakuna asiyefahamu kuwa hata baada ya kufanyika uchaguzi wa marudio na Dk. Shein kuwa Rais wa Zanzibar, ilielezwa hali si shwari visiwani humo huku wafuasi na mashabiki wa vyama hivyo wakiwa hawashirikiani katika shughuli mbalimbali za kijamii.
Tunapomtazama Profesa Lipumba ambaye wakati anajiuzulu nafasi hiyo alisema uamuzi wake huo ulitokana na kile alichokiita kusutwa nafsi yake baada ya Ukawa kumteua Edward Lowassa kuwa mgombea pekee wa ushirika huo wa vyama vya upinzani, yawezekana kwa haya anayoyafanya sasa kuna kitu kilichojificha nyuma ya pazia .
Nasema hivyo kwa sababu Profesa Lipumba tangu awali alishiriki kwenye vikao vyote vya kumkaribisha Lowassa, lakini ghafla akabadili msimamo wake huo.
Hatua yake hiyo ya kujiweka kando dakika za mwisho wakati akihitajika sana, ilionekana kuwa ni usaliti ndio maana kwa haya ambayo anayafanya Profesa Lipumba wengi wanamuona kuwa ni mwendelezo wake wa usaliti.
Hatua ya hivi karibuni kabisa ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kutangaza kumtambua Lipumba kama Mwenyekiti halali wa chama hicho, ndiyo imekoleza zaidi mgogoro huo ndani ya CUF.
Pamoja na mambo mengine, uamuzi huo wa Jaji Mutungi umegusa hisia za wengi huku wengine wakihoji hatima ya mzozo huo na mustakabali wa chama hicho huku wakiufananisha na ule uliopata kutokea ndani ya NCCR-Mageuzi.
Itakumbukwa kuwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, NCCR-Mageuzi ilikumbwa na mgogoro mkubwa uliomhusisha aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Augustino Lyatonga Mrema na Katibu Mkuu wake Mabere Marando.
Mwisho wa yote ukawa ni kumeguka kwa chama hicho kilichokuwa kikuu cha upinzani.
Uamuzi usiotarajiwa wa Lipumba kujirejesha kwa nguvu katika nafasi aliyokuwa amejiuzulu awali na huu wa Msajili wa Vyama vya Siasa unaonekana kufurahiwa na kushabikiwa na baadhi ya wana CCM, ambao wanafahamika kutofurahishwa na kukua kwa upinzani nchini.
Ni CCM hao hao, ambao wakati Lipumba anajiuzulu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, walifurahia uamuzi huo wakifahamu unawapunguza nguvu wapinzani na sasa wanafurahia kurejea kwa vile ni ‘kirusi’ kinachokwenda kuvuruga chama.
Tunapotazama sasa athari za mgogoro huo wa kiuongozi unaoendelea ndani ya CUF, athari zake ni kubwa si kwa demokrasia changa ya Tanzania bali haki kwa Zanzibar ambako ni ngome ya chama hicho.
Kwa kusahaulisha mgogoro wa Zanzibar, kunatoa mwanya wa kuendelea kubinywa kwa haki na demokrasia visiwani humo na kuondoa uwezekano wa kutoa funzo kwa watawala.
Mbaya zaidi mgogoro umeibuka wakati kilio cha Maalim Seif kwa jumuiya ya kimataifa kikiwa kimesikika baada ya Marekani kuishitaki Tanzania katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kupinga nyendo na maamuzi ya Serikali ya Tanzania ikiwemo mgogoro wa Zanzibar.
Marekani ilikwenda mbali ikisema kwamba imebaini tangu uchaguzi ufanyike, Serikali ya Tanzania imeendelea kubana sauti za wapinzani, ikiwa ni pamoja na kufuta matangazo ya moja kwa moja ya Bunge na kuvifunga vyombo kadhaa vya habari.
Bahati mbaya sana, kwa mgogoro huu unaoendelea, suala hilo halikuweza kusikika ipasavyo kutokana na kumezwa na mgogoro huo unaoendelea.
Cha kushangaza zaidi wakati kauli za kupishana maneno makali zikiendelea ndani ya CUF, kuna watu wamejitokeza kujibu kauli hizo tena ni watu ambao mgogoro hautakiwi kuwahusu lakini hao ndio wamegeuka ndio wazungumzaji wakubwa.
Wapo wanaojiuliza Je, kuna jambo linaendelea nyuma ya pazia ya mgogoro huu? Kuna kundi linahusika kujaribu kuua upinzani? Kwanini kuna kundi ambalo ghafla limekuwa mshabiki mkuu wa upinzani?
Wadadisi wanasema au mgogoro huu umepigwa chapuo na wahafidhina kutokana na Maalim Seif kukataa kumpa mkono Dk. Shein walipokutana kwenye msiba wa aliyekuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mzee Aboud Jumbe?
Kuna kila dalili kuwa nyuma ya mgogoro huu kuna ‘mkono wa tawala’ kumtumia Lipumba kuvuruga chama hicho ili kupunguza nguvu za Maalim Seif kuendelea kudai haki yake iliyoporwa.
Kwamba CCM wanamtumia Lipumba kumdhibiti Maalim Seif kwa kuwa amekuwa akizunguka nchi za Ulaya kudai haki yake kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Mbali na mgogoro wa Zanzibar, pia inatajwa kwamba CCM wanamtumia Lipumba kuhakikisha kuwa Ukawa inavunjika.
Mbali na hilo, pia inaelezwa kuwa mgogoro ni zaidi ya inavyoonekana nje kwani ndani ni jambo ambalo linafukuta kwa nguvu na upo uwezekano mkubwa wa kukiangusha chama hicho kisiasa.
Ikiwa haya na mengine yanayosemwa ambayo mengine hayaandikiki ni wazi kwamba ni ndoto vyama vya upinzani kushika dola hata huko tuendako.
Nasema hivyo kwa sababu ikiwa pale inapoonekana upinzani unaimarika lakini maadui zao wanapokuja kuwavuruga tena kwa kutumia fedha nyingi ni vigumu kuitoa CCM madarakani.