25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Kuyumbayumba kimsimamo kunachelewesha upinzani kuingia Ikulu

lipumba

Na ADRIAN MGAYA,

KUNA kasumba nyingi zimejengeka juu ya siasa huku baadhi zikiwa za kweli lakini nyingi zina ukakasi. Chukulia mfano mtu anakwambia siasa ni mchezo mchafu, au kwa wengine wanaoamini siasa ni uongo au ujanja ujanja.

Kuna maneno yanapatikana katika wimbo uitwao ‘sleeping dogs’ utunzi wake Lucky Dube.

Katika wimbo huo Dube anasema: “I don’t wanna look up politicians They’re gonna feed me political bull And I will have political diarrhea”.

Maneno ya wimbo huu kwa tafsiri ya kawaida niliyojaribu kuitoa, Dube anasema sitaki kufuatilia masuala ya kisiasa, wanasiasa watanilisha (kupandikiza) siasa (mambo yasiyotimia) na nitapata homa ya kisiasa (ahadi zisizotimia).

Maneno ya wimbo huu yanaakisi mwenendo wa siasa nchini, hasa siasa za upinzani.

Ukifuatilia siasa sana, utagundua baadhi ya wanasiasa ni pasua kichwa tena huwezi kupata mwafaka juu ya yale wayafanyayo.

Mwanasiasa anaweza akakwambia jambo fulani ukaliamini, lakini akazunguka mlango wa pili na kukana kile alichokisema awali.

Kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, tulishuhudia mambo mengi ;mazuri na  mabaya yaliyofurahisha na kukasirisha.

Sote tulikuwa mashahidi wa yale yaliyokuwa yakitokea, mengine tuliamini yalitengenezwa kama mbinu za kisiasa, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, alipotangaza kuvua gwanda za chama hicho, yalizungumzwa mengi ikiwemo kukosoa ama kupongeza hatua aliyoifikia.

Dk. Slaa alikaririwa akisema: “…nimestaafu siasa, sina chama…” ni kauli iliyowashtusha wengi kutokana na ukweli kwamba Dk. Slaa ni kama aliwaacha wenzake katika uwanja wa mapambano licha ya kwamba aliondoka kusimamia msimamo wake wa kutokubaliana na hasimu wake kisiasa Edward Lowasa aliyekaribishwa katika chama alichohudumu.

Yakasemwa mengi kuhoji kwanini Dk. Slaa aliyekiri kushiriki kumleta Lowasa Chadema na baadaye kudai hajafurahishwa na ujio wake.

Sinema ya Dk. Slaa ikiwa bado moto moto, kukaibuka sinema nyingine iliyovuta hisia za wafuatiliaji wa siasa za hapa nchini pale Profesa Lipumba wa CUF alipojivua nafasi yake ya uenyeketi.

Alipotangaza nia yake ya kuachia madaraka, hakuna aliyetegemea mtu muhimu mwenye nafasi kama aliyokuwa nayo Profesa kufanya maamuzi yale.

Nimekuwa nikijiuliza maneno yake kipindi anatangaza uamuzi wake wa kuachana na nafasi yake yametoka moyoni kweli.

“Najua jambo hili litawashtua, litawakasirisha litawafadhaisha…” Ni kauli yake Profesa Lipumba kabla ya kuachia ngazi ya uongozi na kubaki kama mwanachama wa kawaida.

Maneno yale ya Lipumba yamedumu mpaka sasa, hasa ukizingatia wakati ule wa mapambano, Profesa Lipumba alihitajika kufanikisha lengo la wapinzani kung’oa chama tawala madarakani.

Baadhi waliamini Profesa Lipumba amewasaliti lakini ule ndio ulikuwa msimamo wake, muda ukapita ya Lipumba yakaisha na uchaguzi nao ukaisha salama.

Hivi karibuni, kumeibuka jambo jingine la ajabu ambapo aliyeomba mwenyewe kwa hiari yake kuvua wadhifa alionao tena akitoa sababu alizoona zina mashiko kwake, tena akitoa tahadhari huenda uamuzi wake ukawachukiza wengine, lakini leo anataka kurudi madarakani.

Ama kweli ukistaajabu ya Musa… huenda Profesa Lipumba alisahau wakati aliohitajika kujenga chama chake ni ule ambao aliwaacha njiapanda wanachama wake.

Hayati Shaaban Hamis Mloo, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF, aliwahi kusema: “wanaolazimisha mambo yasiyowezekana katika siasa kwa kuwa tu nafsi zao zinayapenda au wana masilahi binafsi hata kama hayana tija, hawajajifunza majira ya siasa.

Mwanasiasa yeyote asiyejifunza majira ya siasa hawezi kuyadhibiti. Siasa ni majira, tujiandae kabla hayajafika maana huja na upepo wake na hayadhibitiki.”

Maneno haya yananikumbusha jinsi gani wanasiasa walio wengi wanatanguliza masilahi yao mbele na kusahau kile wanachotakiwa kufanya kupigania wanaotaka kuwaongoza.

Ni aibu isiyoepukika kwa watu wanaotegemewa katika taifa kukosa msimamo, tutaamini vipi kwamba mtu ana mapenzi ya dhati na nchi yake hata akipewa jukumu la kuongoza nchi yake, ikiwa chama chake kinamshinda.

Katika ukurasa wake wa facebook, Julius Mtatiro aliwahi kuandika “Katika siasa, kuwa na misimamo yenye tija ni msingi mkuu. Nyimwa kila kitu lakini usinyimwe misimamo katika masuala ya msingi. Na kwa hiyo, katika ndoa, biashara, shughuli yoyote, taaluma na maisha ya kila siku, msimamo ni nguzo yako kuu! Unapokuwa na misimamo yenye tija inahitajika tu wenzako waijue na waiheshimu, huna haja kutumia nguvu kubwa sana kuionesha”.

Nilipoona maneno hayo, nikapata funzo kuna mengi ya kujifunza kutoka kwa wanasiasa wetu, si kwamba Mtatiro na Lipumba wanakinzana na mimi kusimama upande wa Mtatiro, hapana! Maneno ya Mtatiro yana ukweli usiopingika, lazima mtu usimame katika yale unayopigania ili iaminike kweli hayo uliyoyasimamia yana mashiko.

Tunatakiwa kujifunza kutokana na makosa, Profesa Lipumba huenda alijikwaa alipotanganza kuachia ngazi CUF, lakini pia huenda alikuwa sawa kuchukua uamuzi ule.

Franklin Roosevelt aliwahi kusema: “In politics nothing happens by accident. If it happens, you can bet it was planned that way”.

kwa maana kwamba, hakuna linalotokea katika siasa kwa ajali, ikiwa limetokea huwezi kukataa lilipangwa kuwa hivyo. Vivyo hivyo hata kwa kilichotokea kwa Profesa Lipumba huwezi kukataa kama hakijatokea kama ajali.

Jambo la msingi kwa wana CUF na kwa Profesa Lipumba ni kuangalia kama msomi huyo wa uchumi alijikwaa kuchukua uamuzi ule, achukuliwe hatua kulingana na katiba ya chama chake.

Lakini pia kama alikuwa sawa kuchukua uamuzi ule, basi abaki na msimamo wake na huu ndio uwe wakati sahihi wa nafsi yake kumsuta endapo atajisaliti yeye mwenyewe kuacha kuufuata msimamo wake.

Afrika imekuwa ikilaumiwa kwa viongozi wake kung’ang’ania madarakani, viongozi wengi wanaong’ang’ania madarakani ni wale wanaoamini wao pekee ndio waliopigania nchi zao kuwa sehemu zilipo.

Hali kama hiyo inaweza kujitokeza CUF kama Profesa ataamua kung’ang’ania kuongoza cham, akiamini amepigania chama chake na hakuna mwingine anayeweza kushika nafasi yake.

Kwa mfano, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, asingeona umuhimu wa kuachia madaraka kwa kuwa yeye alikuwa mstari wa mbele kudai uhuru wa taifa hili, tungezungumza yapi?

Siasa ni mchezo msafi kama wanasiasa watakuwa safi katika kauli zao na kusimamia yale waliyowaaminisha watu.

Kuyumbayumba kimsimamo ndiko kunakochelewesha upinzani kuionja Ikulu, hivyo ifike wakati wanaokwamisha safari ya mapambano wawekwe kando, safari iendelee bila vikwazo.

Mwandishi wa makala haya ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anapatikana kwa namba 0656110670 au barua pepe [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles