MIONGONI mwa mambo ambayo mzazi au mlezi anaweza kufanya kosa ni pale ambapo atashindwa kutimiza ahadi kwa mtoto endapo alimwambia kuwa akifanya jambo fulani mfano kufaulu mtihani atampatia zawadi.
Hakika mtoto huyo pamoja na kuwa hana uwezo wa kumwadhibu mzazi au mlezi kwa kitendo cha kutotimiziwa, lakini ni wazi atanung’unika huku akipoteza imani kwa yule aliyemuahidi.
Ni dhahiri watumishi wa Serikali ni kama watoto wadogo kwa Serikali wanayoitumikia. Watumishi hawa kufananishwa na watoto ni kwa sababu hutumia muda wao mwingi kuitumikia nchi.
Rais akiwa ndiye kiongozi mkuu wa nchi, anachukuliwa kama mzazi au mlezi wa watu wote anaowaongoza wakiwamo watumishi wa umma ambao kimsingi hutimiza wajibu kwa Serikali iliyoko madarakani.
Katika muktadha huu wa Rais kuwa mzazi au mlezi hakika kila jambo atakalolisema au kuliahidi huchukuliwa na wananchi kwa namna ya pekee na kwa uzito mkubwa.
Rais John Pombe Magufuli kutokana na historia yake ya uadilifu na uchapa kazi huku akitimiza kwa vitendo anayoyatoa kinywani, kumesababisha wananchi waendelee kumuamini hata baada ya kuchaguliwa kuiongoza dola.
Ikumbukwe Rais huyu mara baada ya kuingia madarakani aliwaahidi watumishi wa Serikali ya kuwa wakifanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu atajitahidi kuboresha maslahi yao.
Msisitizo wa maboresho ya kipato cha watumishi ulidhihirika wazi wakati wa kusoma Bajeti ya Serikali ya 2016/2017 ambayo ilikuwa ya kwanza kwa Rais Magufuli na hivyo kuchukuliwa kama dira ya kupima uelekeo wa uongozi mpya.
Ni katika bajeti hiyo palijitokeza mabadiliko makubwa ikiwamo mfumo mpya wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi wa vyombo vya dola hususani majeshi kwa kufuta utaratibu wa awali wa motisha kupitia vinywaji na maduka.
Mfumo huu wa kufuta motisha katika majeshi ulikuja kutiwa asali na mwenye nchi ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu Jumatatu ya Julai 18, mwaka huu, wakati maafisa mbalimbali wa polisi wakila kiapo cha uadilifu Ikulu.
Katika hafla hiyo ya kuwapandisha vyeo maafisa wa polisi, Rais alisema pesa ambazo zilikuwa zinapitia kwenye mgongo wa motisha zitatolewa kama kifungashio ili kila afisa au askari ajipangie bajeti yake mwenyewe.
Baada ya hapo zilianza kujitokeza hadithi nyingine ya kwamba Serikali haitapandisha vyeo, kuajiri au kuongeza mishahara kwa muda wa miezi miwili ili kutoa nafasi ya kuondoa watumishi hewa.
Ajabu ni kwamba pamoja na kuwa watumishi walivumilia na kuendelea kumuamini Rais, lakini hata baada ya miezi miwili kumalizika hakuna mabadiliko yoyote yamefanyika zaidi ya kusikia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki akisema nyongeza itatangazwa baadaye kana kwamba suala la watumishi hewa limekuja kama mvua.
Ni ukweli usiopingika Rais wetu ameonyesha njia kwa kupinga hujuma na hivyo anastahili pongezi na kutiwa moyo lakini hata hivyo kuna sababu ya kuchukua tahadhari katika kutoa ahadi. Kwa mambo yasiyo na uhakika ni heri kunyamaza ili yatekelezwe kwa kushtukiza.
Ili kuondoa hali ya sintofahamu ambapo wafanyakazi wameanza kulia kwamba maisha ni magumu na kuhisi Serikali inajitapa kumbe haina pesa, huku wengine wakisema inataka misifa kwa kununua haraka vitu vya bei ghali kama ndege, kuna haja Baba wa kaya kutimiza ahadi zake kama anataka kupambana na ufisadi, rushwa na uzembe kazini.