NA BENJAMIN MASESE,
SEPTEMBA 7 mwaka huu, Tume ya Utumishi wa Mahakama iliwafukuza kazi watumishi 34 wa mahakama mbalimbali nchini wakiwamo mahakimu na maofisa kutokana na makosa ya nidhamu, sheria na mzaha wa sheria.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Othman Chande, hatua zilizochukuliwa kwa watumishi zilitokana na kutumia vibaya muhuri wa mahakama, kusaidia mtu kufungua kesi moja kwenye mahakama mbili tofauti kinyume na maadili, pia hakimu kufungua kesi ya mirathi bila kuwapo na hati ya kifo.
Kwa wale ambao walishakumbana na adha hiyo kutoka kwa watumishi wa mahakama hizo, wanaelewa uchungu wake.
Ni hatua nzuri kwani tunaambiwa wahusika watafikishwa mbele ya kamati ya maadili na nidhamu ya mahakama.
Ni jambo jema na la busara kufikishwa kwenye kamati kwani katika mahojiano hayo lazima mambo fulani yatabainika yalifanywa na mahakama kinyume na utaratibu.
Iwe kwa lengo la kumpendelea mtumishi wa taasisi hiyo ambayo inatoa haki kwa watu wote bila kujali jinsia, uwezo wa kiuchumi wala cheo cha mtu.
Vitendo vya namna hiyo vimewachosha wananchi wanaofika mahakamani kutafuta haki zao hususani wale wanaotoka vijijin,i kwani wenye uwezo ndiyo wanaopatiwa haki na imefikia hatua wanyonge kuonewa hadharani na matajiri.
Kibaya zaidi, wananchi wa vijijini wamekuwa hawana elimu ya kutosha juu ya kudai haki yao badala yake wamezoeshwa kununua haki yao huku wachuuzi wa haki hiyo ni hakimu na wazee wa mahakama wakitumia udhaifu na uelewa mdogo wa wananchi hao.
Kwenu Tume ya Utumishi wa Mahakama, iwapo mtahitaji ushirikiano pale inapohitajika juu ya kile nilichokiandika nipo tayari.
Lakini mnapaswa kutambua kwamba wananchi wanaofika Mahakama ya Mwanzo Kiagata, iliyopo Wilaya ya Butiama pamoja na Mahakama ya Wilaya ya Musoma, wanapata adha kubwa juu ya haki zao.
Mahakama hizi kupitia watumishi wake zimekuwa zikijihusisha na usikilizwaji wa  baadhi ya kesi ambazo hazipaswi kusikilizwa hapo zikiwamo za migogoro ya ardhi.
Lakini kutokana na kutofuata misingi ya maadili ya kazi na sheria ambazo zimewafukuza wenzao 34, mahakimu hao wamekuwa wakisikiliza na kutoa hukumu na inapotokea mlalamikaji kukata rufaa kwenda mahakama za juu zaidi, wamekuwa na tabia ya usumbufu wa kutopeleka nakala zinapotakiwa.
Pia watumishi hao wamekuwa na tabia ya kushirikiana kati ya Mahakama ya Mwanzo na Wilaya kwa nia ovu katika kuminya haki za mlalamikaji.
Wakati mwingine wanafikia hatua ya kutoa hukumu mbili katika kesi moja iliyokatiwa rufaa kwenda Mahakama Kuu na wanapoona mambo yanakwenda kuwaumbua, hulazimika kuwakutanisha mlalamikaji na mlalamikiwa na kufanya mazungumzo.
Mahakama ya Kiagata imekuwa na tabia ya kutoa kifungo cha nje na kuweka utaratibu wa mfungwa kufika mahakamani kwa muda Fulani, lakini utekelezaji umekuwa haufanyiki kutokana na rushwa.
Haiwezekani kwa mahakimu wanaojua sheria kupokea kesi ambazo hazipaswi au ambazo haziwahusu kisha kusikiliza na kutoa hukumu, lakini mwisho wa siku wanatoa hukumu nyingine ya pili inayoeleza kwamba Mahakama ya Wilaya haina uwezo wa kusikiliza kesi fulani ambayo tayari kuna hukumu yake.
Yapo maswali ya kujiuliza kwa hakimu ambaye amepokea kesi na kuisikiliza zaidi ya miezi minne na kutoa hukumu na baadaye kubadilika na kukana hukumu yake baada ya kesi hiyo kutakiwa kupelekwa Mahakama Kuu.
[email protected], 0683608958