JONAS MUSHI Na HARRIETH MHUNGA(SJMC), DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amepokea ripoti na mapendekezo ya uchunguzi wa migogoro ya mipaka ya Kijiji cha Mwabwegere na vijiji jirani katika Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.
Awali akimkaribisha Mchunguzi ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara, Jacob Mwambegele, Lukuvi alisema kwa mujibu wa sheria za ardhi hatua ya kumtumia mchunguzi ni ya mwisho katika utatuzi wa migogoro ya ardhi nchini.
Alisema kutokana na hali hiyo mapendekezo na maelekezo yaliyotolewa na Mchunguzi huyo yatakuwa ya mwisho na hayatakuwa na mjadala katika usuluhishi wa mgogoro huo.
“Kwa mujibu wa sheria zetu za ardhi mapendekezo yake hayana mjadala na ni ya mwisho katika usuluhishi na utatuzi wa migogoro ya ardhi,” alisema Lukuvi.
Baada ya kukabidhiwa mapendekezo hayo, Lukuvi alisema mapendekezo hayo ni “hatari na moto” na kwamba lazima tahadhari ichukuliwe na yatapangiwa kalenda za utekelezaji.
“Mapendekezo yaliyotolewa humu ni hatari na ni moto kwa hiyo kabla ya kuyatoa lazima tuandae tahadhari za kwenda kuuzima moto huo, ” alisema Lukuvi alipotakiwa na waandishi wa habari kueleza baadhi ya mapendekezo ya Jaji Mwambegele.
Uchunguzi huo ulifanywa kwa siku 60 huku Mchunguzi akishirikiana na wataalamu wengine kutoka Wizara ya Ardhi na Mahakama.
Akiwasilisha ripoti hiyo, Jaji Mwambegele alisema uchunguzi huo ulifanywa kwa mujibu wa Sheria ya ardhi na sheria ya ardhi ya vijiji ya mwaka 1999 kwa lengo la kutafuta chanzo cha mgogoro na kutafuta utatuzi wa mgogoro huo.
“Naomba kuwasilisha taarifa ya uchunguzi wa mgogoro wa mipaka kati ya kijiji cha Mambwegere na vijiji jirani vya Nambega, Mbigiri, Dumila, Matongoro na Mfuru vilivyopo Kilosa mkoani Morogoro,” alisema Jaji Mwambegele.
Alitaja maeneo yaliyofanyiwa uchunguzi kuwa ni uanzishwaji, upimaji na utolewaji hatimiliki ya kijiji, maeneo yenye mgogoro na hatua zilizowahi kuchukuliwa katika migogoro hiyo, uwiano wa ardhi, mifugo na mahitaji mengine ya ardhi na ukaidi wa kijiji kushiriki katika usuluhushi wa awali.
“Maeneo mengine ya uchunguzi ni kuhusu vyanzo vingine vya mgogoro tofauti na mipaka na mambo mengine yanayoweza kusaidia kufikia utatuzi wa mgogoro,” alisema Jaji Mwambegele.
Alisema pia uchunguzi ulifanyika kubainisha athari za sheria kwa kutekeleza mapendekezo ya ripoti hiyo kutokana na kuwapo uamuzi wa Mahakama ya Rufani kupitia kesi namba 53 ya mwaka 2010 kati ya Halmashauri ya kijiji na Khamis Shaban Msambaa na wenzake 32.
Alisema mbinu zilizotumiwa katika uchunguzi huo kuwa ni kufanya mikutano katika ngazi mbalimbali kuanzia ngazi ya mkoa hadi ya kijiji.
“Mkutano wa kwanza ulikuwa kati ya timu yangu ya uchunguzi na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), mikutano na halmashauri za vijiji husika kwa kuhusisha viongozi wa kati ambao walikuwa 25 kutoka kila kijiji na madiwani wa kata husika.
Febuari mwaka jana wakulima watatu waliuawa katika Kijiji cha Mbigili baada ya kushambuliwa na kundi la wafugaji wa wamasai kutokana na mgogoro katika eneo hilo la Mambwegere wilayani Kilosa.