MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Ardhi imezuia kupigwa mnada mali za Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, hadi uamuzi wa pingamizi lililowasilishwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhusu maombi yake utakapotolewa.
Uamuzi huo wa mahakama ulitolewa jana mbele ya Jaji Sivangilwa Mwangesi baada ya kusikiliza hoja za sheria kuhusu maombi ya zuio la muda yaliyowasilishwa na Mbowe na pingamizi lililowasilishwa na NHC.
Katika maombi hayo namba 722 ya 2016, Mbowe anawakilishwa na Mawakili Peter Kibatala na Omari Msemo wakati NHC inawakilishwa na Mawakili Aloyce Sekule na Mariamu Mungula.
Mbowe Hotels Limited imewasilisha maombi chini ya hati ya dharura dhidi ya NHC na Kampuni ya Udalali ya Poster and General Traders.
Wanaomba mahakama iamuru wadaiwa wamrudishe mdai katika ghorofa namba 007 lililopo Plot No. 725-726/24 Mtaa wa Mkwepu/Indira Gandhi (Makunganya), Manispaa ya Ilala yenye hati namba C. T No. 186018/15 and C. T No. 186018/10 kwa vile walimuondoa kwa makosa.
Kibatala anadai wadaiwa wote wawili, Septemba mosi bila ridhaa ya mahakama walimuondoa mteja wake wakati usuluhishi ukiendelea kuhusu mkataba wa ubia walioingia Mbowe Hotels Limited na NHC kuhusu jengo hilo.
Inadaiwa notisi ya kumuondoa ndani ya jengo hilo ilipelekwa kwa Kampuni ya Free Media Limited ya Tanzania Daima wakati yeye ni Mbowe Hotels hivyo waliiomba mahakama iamuru NHC na Kampuni ya Udalali warudishe vitu walivyopora.
Maombi hayo yaliwasilishwa kwa hati ya dharura na yaliambatanishwa na kiapo kilichoapwa na Freeman Aikael Mbowe.
NHC na Kampuni ya Udalali waliwasilisha pingamizi la awali wakidai kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo ya Mbowe kwa sababu hakuna kesi ya msingi.
Wadai wakijibu pingamizi hilo walidai wanaomba mahakama itoe amri ya muda huku wakisubiri usuluhishi kujua iwapo kweli Mbowe anadaiwa kodi ama la.
Awali, Kibatala aliomba pingamizi hilo na maombi yasikilizwe kwa pamoja kwa sababu anahofia kuna mbinu za kuchelewesha kesi kwa vile hata pingamizi hilo ni njia mojawapo ya ucheleweshaji wa kesi.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Jaji Mwangesi aliamuru wadaiwa wasiuze mali za Mbowe hadi uamuzi wa pingamizi utakapotolewa Septemba 16 mwaka huu.
Kampuni ya udalali ilipewa na NHC kazi ya kumwondoa Mbowe katika jengo hilo kwa madai ya kushindwa kulipa kodi ya pango, Sh bilioni 1.2.
Mbowe aliondolewa kwenye jengo hilo Septemba Mosi, siku chache baada ya NHC kutangaza orodha ya wapangaji wake ambao ni wadaiwa sugu, ikiwamo kampuni hiyo ya Mbowe.
Katika hati yake ya kiapo, Mbowe anadai kuwa yeye ni mmoja wa wamiliki wa jengo hilo na kwamba analimiki kwa ubia baina yake na NHC.
Mbowe anadai analimiki jingo hilo kwa asilimia 75 huku NHC ikiwa na umiliki wa asilimia 25 tu.