21.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, August 16, 2022

Serikali lawamani kukataa kiwanda

boniface-jacob-chademaNa MAULI MUYENJWA

– DAR ES SALAAM

MEYA wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob (Chadema), ameituhumu Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, kwamba imezuia mradi wa kutengeneza mbolea kwa kutumia takataka, uliopangwa kutekelezwa na Manispaa ya Hamburg ya Ujerumani.

Jacob ambaye pia ni Diwani wa Ubungo, aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa mradi huo ulikuwa umefadhiliwa na Manispaa ya Hamburg kwa gharama ya Sh bilioni 3.5. Ulitarajiwa kukamilika Juni mwakani.

Alisema wafadhili wa kiwanda hicho wamesitisha mpango huo baada ya Serikali kuwataka walipe kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ya Sh milioni 500 pamoja na milioni 400 kwa ajili ya kuingiza mitambo.

“Mradi huu ulikuwa ni wa msaada, si wa biashara. Lakini pia ulitarajiwa kuleta mapinduzi makubwa ya tatizo la takataka na uchafu katika Jiji la Dar es Salaam. Ulikuwa ni mradi wa watu wa Kinondoni na si Meya wala mtu yeyote, na faida ambazo zingepatikana ni kwa ajili ya wananchi,”alisema Jacob.

Katika ufafanuzi huo, Jacob alisema Manispaa ya Kinondoni iliandika barua kwa Serikali ili Manispaa ya Humburg ipate msamaha wa kodi kwa vifaa na magari, vitakavyohitajika katika mradi huo.

Hata hivyo, alidai Wizara ya Fedha na Mipango kupitia barua yenye kumbukumbu No: CAC 355/558/01 iliwakatalia kwa hoja kwamba sheria ya VAT ya mwaka 2014 haitoi msamaha wa kodi, isipokuwa kama kulikuwa na makubaliano ambayo yamethibitishwa na Waziri wa Fedha.

Na kwamba makubaliano hayo yataingiwa kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali nyingine au mawakala wa kimataifa ambao wanalindwa na sheria ya kinga kwa wanadiplomasia.

Barua hiyo ilieleza pia kuwa Sheria ya Forodha ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 haitoi msamaha wa kodi, na kwamba mfadhili huyo anatakiwa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria za kodi za Tanzania.

“Kutokana na zuio hilo, ajira zaidi ya 500 zimekufa na suala la kumaliza changamoto ya takataka katika Manispaa ya Kinondoni na Dar es Salaam kwa ujumla limeyeyuka.

“Inavyoonekana Serikali ya CCM haiko tayari kufanya kazi na wapinzani, na kwamba kilichofanyika ni ‘figisu’ za kisiasa ambazo zimechangia kuzuia utekelezaji wa mradi huo.

“Kwa hali hii tumefikia mahali pabaya ambapo siasa zinahusishwa na mambo ya wananchi,” alisema.

Ofisa Habari wa Wizara ya Fedha na Mipango, Ben Mwaipaja, alipopigiwa simu ili kutolea ufafanuzi suala hilo, alimtaka mwandishi kumpelekea barua hiyo inayodaiwa ni ya wizara kwa ajili ya kuhakikiwa kabla ya kuitolea majibu.

“Muda huu nimekwishatoka ofisini, siwezi kuzungumzia barua ambayo sijaiona, naomba uje kesho ofisini tuifanyie uhakiki,” alisema Mwaipaja.

Naye Mbunge wa Ubungo aliyekuwapo katika mkutano huo, Saed Kubenea, alisema uchaguzi umeshaisha hivyo viongozi wasichanganye mambo ya siasa na mambo ya maendeleo ya wananchi.

“Kazi ya serikali kuu ni kuratibu na kupeleka maendeleo katika halmashauri na manispaa zote bila kubagua zile zinazoongozwa na vyama vya upinzani, kwa sababu wote ni Watanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,814FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles