32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Msaidie mtoto kujifunza, kumudu lugha

pix

Na CHRISTIAN BWAYA,

LUGHA ni nyenzo muhimu tunayoihitaji katika maisha. Hatuwezi kufikiri vizuri, kuongea, kusikiliza, kueleza mambo tuliyokutana nayo na hata tunayoyatarajia siku zijazo bila lugha. Ni wazi tunalazimika kutumia maneno au ishara kuwasiliana na wanaotuzunguka.

Mjadala wa namna gani mtoto hujifunza lugha ya mama una historia ndefu. Hata hivyo, kuna ukweli kwamba ili mtoto ajifunze lugha ipasavyo anahitaji kuwa na uwezo fulani anaozaliwa nao unaomwezesha kuelewa kanuni muhimu za lugha bila msaada mkubwa. Lakini pia mazingira anayokulia mtoto nayo yana nafasi kubwa ya kumwezesha kujifunza na kumudu lugha ya kwanza kirahisi.

Hatua za mtoto kujifunza lugha

Tangu mtoto anazaliwa hujaribu kuwasiliana na wanaomzunguka. Kulia ni lugha ya kwanza anayoitumia mtoto kuwasiliana na wengine. Hulia kuonesha kutokuridhishwa, wasiwasi, maumivu au hata kutafuta kusikilizwa. Lakini kadri mtoto anavyozidi kukua, kulia hupungua na huanza kujifunza kuwasilisha hisia zake kwa kutumia sauti zisizoeleweka.

Mpaka anapofikia umri wa miezi sita mtoto huanza kujifunza lugha ya mama yake hatua kwa hatua kwa kutumia maneno rahisi. Katika umri wa miaka mitatu na minne mtoto huiga maneno mengi zaidi hasa yale anayoyasikia yakitamkwa mara kwa mara katika mazingira yake.

Wakati mwingine neno moja kwa mtoto humaanisha zaidi ya jambo moja. Mfano neno ‘mma’ linaweza kuwa na maana ya ‘mama’, ‘maji’, ‘njaa’ na kadhalika. Ni kama vile mtoto huonekana kuelewa vitu vingi zaidi ya vile anavyoweza kuvitamka kwa maneno yake.

Katika umri wa miaka mitano na sita mtoto huanza kumudu lugha na huwa mwongeaji. Hupenda kusimulia yale anayokutana nayo na kuuliza maswali mengi. Kadri anavyopata msaada kwa wanaomzunguka, mtoto hujifunza msamiati zaidi. Baada ya miaka sita, mtoto huwa bingwa wa lugha na huweza kuitumia kwa ufasaha katika kufikiri asiyoyaona.

Kumsaidia mtoto kujifunza kuongea

Njia ya kwanza iliyozoeleka ni kuongea na mtoto kwa lugha ya kitoto. Hii ni lugha yenye kutumia maneno rahisi yanayotamkwa kwa sauti ya juu kuliko kawaida. Lengo la lugha hii ni kumhamasisha mtoto kuvutiwa kuongea. Kadri tunavyojibidiisha kuongea naye kitoto tunampa hamasa ya kujifunza.

Kadhalika, kurudia kutamka kwa usahihi maneno na sentensi anazojaribu kuzitamka mtoto humsaidia kuiga utamkaji bora zaidi wa maneno. Mfano; anaposema, ‘mma’ tunaweza kurudia kwa marekebisho, ‘Unataka maji? Chukua m-to-to!’ Kurudia maneno yake hukuza uwezo wake wa kuongea bila kuchelewa.

Vile vile, kuongezea maana ya kile anachokisema mtoto humsaidia kujifunza matumizi sahihi ya lugha. Kwa mfano; anaposema, ‘baba kuja’, tunaweza kumsaidia kutengeneza sentensi fupi na sahihi zaidi kama, ‘ndio! Baba anakuja!’ Kufanya hivi humharakishia mtoto kuelewa namna ya kujieleza kwa kutumia sentensi rahisi.

Sambamba na hiyo, tunaweza kumsaidia mtoto kuoanisha majina ya vitu anavyovitumia mara kwa mara na maneno husika. Mfano; anapokuwa ameshika gauni lake tunaweza kumsaidia kutamka neno ‘gauni’ ili aweze kuhusisha neno ‘gauni’ na kile anachokiona. Kwa kufanya hivyo, tunamwekea mazingira ya kuongeza zaidi msamiati wake.

Pamoja na ukweli kwamba si kila anachokifahamu mtoto anakuwa amefundishwa, bado kuna uwezekano mkubwa kuwa mtoto anayeishi kwenye mazingira yanayomtia moyo kujifunza lugha anaweza kumudu lugha kirahisi zaidi.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Anapatikana kwa [email protected] na 0754 870 815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles