LIBREVILLE, GABON
RAIS wa Gabon, Ali Bongo, amedai yu tayari kutii uamuzi wa Mahakama ya Kikatiba iwapo itaagiza kura za uchaguzi mkuu uliofanyika wiki mbili zilizopita zihesabiwe upya.
Waangalizi wa kimataifa wamesema kulikuwa na kasoro nyingi kwenye matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa, ambayo yalimpa Bongo ushindi mwembamba.
Kwenye mahojiano na kituo cha redio cha Ufaransa, Bongo alisema sheria za nchi yake haziruhusu kura zihesabiwe tena, lakini atakubali hilo iwapo mahakama itaamua lifanyike.
Mahakama ya kikatiba inatarajiwa kukutana Alhamisi kuangazia kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo, ambayo iliwasilishwa na mgombea wa upinzani, Jean Ping.
Bongo alisema suala kuu kwake kwa sasa ni kurejesha utulivu na kuiwezesha Mahakama ya Kikatiba ifanye kazi yake.
Bongo alitangazwa mshindi wa uchaguzi, lakini upinzani ukiongozwa na Jean Ping ulipinga matokeo.
Bongo alipata asilimia 49.8 ya kura, huku Ping akiwa na asilimi 48.2, tofauti kati yao ikiwa kura 5,594.
Ping alishinda majimbo sita kati ya tisa na ameomba kurudiwa tena kuhesabiwa kwa kura.
Wakati huo huo, ujumbe wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Gabon ulihoji ushindi wa Rais Bongo na kushauri kura zihesabiwe upya huku Umoja wa Afrika ukipanga kutuma wapatanishi.