23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

Simba yakata ‘ngebe’ za Ruvu, Yanga yabanwa

3

Na THERESIA GASPAR- DAR ES SALAAM

WEKUNDU wa Msimbazi, Simba jana walikata ngebe za maafande wa Ruvu Shooting, baada ya kuwatandika mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, iliyokuwa ikichezwa jana katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Wakati Simba ikikata ngebe za maafande hao waliokua wanachonga sana kupitia msemaji wao, Masau Bwire, Azam imewatembezea kichapo cha bao 1-0 Maafande wa Prisons, huku watani wao wa jadi, Yanga walijikuta wakibanwa mbavu Nangwanda Sijaona, Mtwara, pale walipolazimishwa suluhu na wenyeji wao Ndanda.

Katika mchezo wa Dar es Salaam, Ruvu Shooting ilikuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza dakika ya nane kipindi cha kwanza, kupitia kwa mshambuliaji wake, Abdulhaman Musa, aliyepiga shuti kali akiwa ndani ya 18  mbele ya  kipa Vicent Angban.

Bao hilo halikudumu kwani dakika ya 11  mshambuliaji wa Simba,  Ibrahim Ajib, aliisawazishia Simba baada ya kupokea krosi safi iliyopigwa na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na kuwanyanyua vitini mashabiki.

Ajib dakika ya 15 almanusura aongeze bao la pili kwa Simba, alipiga shuti kali akiwa nje ya 18 lililopanguliwa na kipa Abdallah Rashid.

Kosakosa hiyo kwa Simba ziliendelea, lakini kubwa ni ile ya dakika 36 baada ya mshambuliaji kipenzi cha Simba, Laudit Mavugo, kukosa bao akipiga shuti kali lililopaa juu.

Timu hizo zilimaliza kipindi cha kwanza zikiwa na matokeo ya sare ya bao 1-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa nguvu, huku Simba ikiongeza bao la pili dakika ya tatu baada ya mpira kuanza likifungwa na Mavugo, aliyepokea pasi kutoka kwa Jonas Mkude, akitumia vema makosa yaliyofanywa na mabeki wa Ruvu Shooting na kufunga bao hilo lililodumu hadi dakika ya 90.

Katika mechi hiyo, Mwamuzi Ngole Mwangole, alitoa jumla ya kadi tisa, tano zikiwa za Ruvu Shooting nne za Simba.

Mwamuzi huyo alitoa kadi hizo kwa Renatus Kasase, Said Dilunga, Issa Kanduru na alitoa nyekundu kwa Jabir Aziz ‘Stima’, aliyemfanyia madhambi mshambuliaji, Mudhamir Yassin.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,712FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles