WAKATI wa Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, Chama cha NCCR-Mageuzi ndicho kilichokuwa chama cha upinzani chenye nguvu zaidi Tanzania Bara, huku Chama cha Wananchi (CUF) kikiwa na nguvu sana kwa upande wa Zanzibar.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka ule ulidhihirisha nguvu ya vyama hivyo viwili, kwani vilifanikiwa hata kupata idadi kubwa ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
Hata hivyo, NCCR-Mageuzi iliyokuwa chini ya Uenyekiti wa Augustine Lyatonga Mrema wakati huo, iliangusha wananchi. Kunyang’anyana uongozi na tamaa ya madaraka ilivuruga kabisa chama na kusababisha Mrema kuanza kufukuzana na Katibu Mkuu wake, Mabere Nyaucho Marando.
Kwa wengi tuliokuwa tukishuhudia yaliyokuwa yakiendelea NCCR-Mageuzi, tulishangazwa sana na hali ile. Kuna wakati Mrema alitangaza kumfukuza uanachama Marando na wakati huo huo, Marando naye alitangaza kumfukuza uanachama Mrema. Vurugu zilizokuwepo wakati ule ndizo zilizosababisha NCCR-Mageuzi kutoka kuwa chama cha upinzani chenye nguvu zaidi Tanzania Bara, hadi kufikia kuwa chama kinachosubiri fadhila ya muungano wa vyama vingine vya upinzani ili kiendelee kujitutumua.
CUF ni chama cha upinzani ambacho tangu mwaka 1995, kimetulia. Kwa Zanzibar huenda kikaendelea kuwa na nguvu ileile, lakini huko nako tunafahamu kwamba hata uwakilishi kwenye Baraza haupo, kutokana na kuususia uchaguzi wa marudio ambao umeua kabisa hata ile Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Huku Bara sasa hali ni mbaya zaidi. Aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, alipoamua kujiuzulu mwaka jana wakati tukielekea kwenye Uchaguzi Mkuu, kulikuwa na utulivu kwenye chama. Licha ya wanachama kutopendezwa na hatua ile ya Profesa, bado aliendelea kuwa mwanachama mwenzao na alikuwa akitumia hata ofisi za chama kufanya mikutano na vyombo vya habari. Huo ulikuwa ukomavu ambao tungependa kuendelea kuuona.
Lakini matukio ya wiki za hivi karibuni, yanaiondolea CUF umakini wote na heshima yote ambayo Watanzania tulikuwa tumewapa. Ugomvi wa kugombania madaraka unafanya chama hicho kuturudisha kulekule ambako NCCR-Mageuzi ilitupeleka miaka ile na kusababisha upinzani kuanza kuonekana dhaifu.
Jumapili iliyopita tu, CUF wamerudia tena ugomvi wao. Kaimu Mwenyekiti, Julius Mtatiro, aliita vyombo vya habari makao makuu ya chama hicho na kilichotokea ni fujo nje ya jengo hilo, huku baadhi ya wanachama wakitaka kumzuia asizungumze kwa madai kwamba hana mamlaka. Bado wanamtaka mwenyekiti wao, Profesa Lipumba. Profesa Lipumba naye bado anautaka uenyekiti wake aliojivua mwenyewe mwaka jana. Uongozi wa CUF nao unautaka uenyekiti wao usibaki kwa Profesa.
Na kama kawaida ya vyama vya upinzani, kufukuzana uanachama ndiko kunaonekana kama kitu kinachoshabikiwa zaidi. Licha ya kumvua Profesa uanachama, CUF imewavua pia uanachama viongozi wake wengine. CUF inasahau kabisa kwamba fukuza-fukuza ya wanachama waandamizi imeshaleta matatizo huko nyuma, kama vile matatizo ambayo NCCR iliyapata na kuifanya kuwa dhoofu hadi leo.
Naomba nitamke wazi kwamba kinachofanywa na CUF ni dhambi kubwa. Watanzania tunautaka mfumo wa vyama vingi ili kutoa changamoto katika ulingo wa siasa na ili chama tawala kiwe makini zaidi katika utendaji wake serikalini.
Inapotokea kwamba chama cha upinzani chenye nguvu sana hapa nchini kinaacha kujadili mambo muhimu kama vile namna ya kukiondoa madarakani chama tawala na badala yake kinawaza namna ya kuondoa madarakani wanachama wake, hapo kunakuwa na tatizo kubwa.
Kwa sasa CUF haipo hata serikalini Zanzibar. Haina hata wawakilishi. Haina hata wabunge wa kumwaga. Huu ulikuwa ni wakati wao wa kujipanga na kujiimarisha, kwani 2020 si mbali hata kidogo kurudisha hadhi yake.
Kama CUF itashindwa kutumia busara na kuendelea kugombana kama watoto wadogo, upinzani Tanzania utatakiwa kurudi darasani.