* Kamati ya Bunge yaingilia kati sakata hilo
Na Mwandishi Wetu,DAR ES SALAAM
NI kauli tata; ndivyo unavyoweza kusema. Hatua ya kupungua kwa mizigo imeliamsha Bunge huku Kamati ya sekta ya Viwanda, Biashara na Mazingira ikitangaza uamuzi wa kuwakutanisha wadau kujadili mdororo huo wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam.
Kamati hiyo imetangaza kukutana na wadau na Serikali kujadili namna ya kuiwezesha bandari hiyo kurejesha mizigo ambayo kwa sasa inaonekana kupungua kutokana na sababu mbalimbali.
Juzi, kamati hiyo ilikutana na wadau na uongozi wa Mamlaka ya Bandari (TPA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambako ilibainika mkanganyiko wa taarifa kutoka kwa kila upande.
Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Dalali Kafumu alisema kuna umuhimu wa kukutanishwa pande hizo kutokana na mkanganyiko huo.
“Nafikiria ni vizuri tukaenda kwenye mazungumzo tuweze kurekebisha, tuweze kuambiana ukweli na tupate majibu, sisi tutaitisha mkutano wa pamoja haraka.
“…nchi iko katika hali ambayo si ya kawaida, wakati mwingine kuna mambo mengi sana tunamdanganya Rais kwa hiyo tutaitisha mkutano,” alisema Dk. Kafumu.
Alisema kwa mujibu wa wadau hao, kuna mambo ambayo yamechangia mizigo kupungua ikiwamo mizigo inayoenda nje ya nchi kutozwa tozo la Ongezeko la Thamani (VAT), mfumo wa himaya moja ya ushuru wa forodha (Single Custom Territory) na kutokuwa na uhusiano mzuri.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania TPA, Deusdedit Kakoko, alikiri kupungua mizigo katika bandari hiyo huku akielezea mambo mbalimbali yanayochangia mdororo huo wa mizigo.
Alisema miongoni mwa sababu hizo ni kudorora kwa uchumi wa China, kushuka bei ya mafuta, gesi na shaba, hali iliyosababisha kupungua shehena inayohudumiwa katika bandari nyingi duniani, zikiwamo za Afrika.
“Hofu ya wateja inayotokana na kuanzishwa sheria ya VAT kwenye huduma zinazotolewa kwenye mizigo ya nchi jirani ambayo haitozwi kodi katika nchi zenye bandari shindani,” alisema Kakoko.
Alisema jambo jingine ni hofu ya wateja kuhusu utaratibu wa himaya moja ya ushuru wa forodha na kwamba mzigo unaohudumiwa kwenye mfumo huo unatozwa kodi kwa asilimia 100.
Kakoko alisema jambo hilo huwafanya baadhi ya wafanyabiashara kuona kupitisha mizigo yao nchini ni gharama kubwa.
Naye Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa wa TRA, Jocktan Kyamuhanga alisema baadhi ya watu wamekuwa wakijichanganya kwa sababu mizigo inayosafirishwa kwenda nje ya nchi haitozwi kodi.
“Ninataka kusema hapa hakuna mzigo unaoenda nje ya nchi unaotozwa kodi, ila huduma ya kupakua mzigo, kuhifadhi na nyingine ndizo zinazolipwa lakini hakuna kodi inayotozwa kwa mzigo unaoenda nje,” alisema. Kyamuganga
Awali, wakizungumza kwenye mkutano wa wadau, baadhi ya wadau hao walisema mizigo imepungua katika bandari hiyo kutokana sababu kubwa tatu.
Walitaja sababu hizo kuwa ni VAT, mfumo wa himaya moja ya ushuru wa forodha na kukosekana ushirikiano kati ya wao na viongozi wa mamlaka husika.
Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha (TAFFA), Stephen Ngatunga, alisema asilimia 42 ya mizigo iliyokuwa ikienda nje ya nchi imepungua katika bandari hiyo na hivyo kusababisha madhara kwa serikali kukosa mapato, baadhi ya watu kukosa kazi na bandari kavu kukosa mizigo.
Msemaji wa Chama Usafirishaji Mizigo Tanzania (Tatoa), Elias Lukumay, alisema upo ushahidi wa kupungua mizigo bandari sababu ikiwa ni pamoja na suala la VAT.
“Sisi tunao ushahidi kwa suala la VAT kuwa limeongeza kwenye balance sheet yao Dola milioni 6 mpaka 7 kwamba kila tani moja inawagharimu dola 35 kwa hiyo wakizidisha kwa oda walizonazo (waagizaji) kwa mwaka huu.
“Hali hii imewafanya wachague kutumia bandari nyingine. Kwa mfano Kampuni ya Impala kwa mwaka jana kipindi kama hiki kwa mwezi ilikuwa inaagiza tani 40,000 lakini mwa mwaka huu kipindi kama hiki imeleta tani 1000 tu,” alisema Lukumay.
Hali ya mizigo
Ripoti ya bandari inaonyesha shehena yote imeongezeka kwa asilimia 9.1 kutoka tani milioni 11.029 mwaka 2011/12 hadi tani milioni 14.007 mwaka 2015/16
“Shehena ya makasha iliongezeka kwa wastani wa asilimia 4.4 kwa mwaka. Makasha yaliyohudumiwa na TICTS yaliongezeka kutoa makasha TEUS 353,471 mwaka 2011/12 hadi makasha TEUS 496,431 sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 8.8 kwa mwaka,” ilieleza taarifa hiyo.
Suala la usalama mdogo wa mizigo inayosafirishwa kwenda nchi za jirani nalo linaelezwa limelazimisha wenye mizigo kuingia gharama ya kuweka walinzi wa kusindikiza mizigo yao.
“Kukosekana kwa uaminifu kwa baadhi ya Wakala wa Forodha wanaowatapeli wafanyabiashara. Muda mfupi (Short grace period for transit bulk liquid) kwa mzigo wa mafuta wa nchi za jirani kuwa siku 30, tofauti na bandari za nchi shindani ambazo huwa ni siku 60 hadi 90,”.
Uhalisia wa mapato
Taarifa hiyo ya bandari ilieleza kwamba katika kipindi cha mwaka 2011/12 hadi mwaka 2015/16 makusanyo ya mapato katika bandari ya Dar es Salaam yaliongezeka kwa wastani wa asilimia 16.85 kwa mwaka.
“Katika kipindi cha mwaka 2015/16 bandari ya Dar es Salaam ilikusanya Sh milioni 694,383 zaidi kwa asilimia 2.2 ikilinganishwa na Sh milioni 679,331 ya mwaka 2014/15,” ilisema taarifa hiyo.