LIBREVILLE, GABON
RAIS anayetetea kiti chake nchini Gabon, Ali Bongo na mpinzani wake mkuu Jean Ping, kila mmoja amedai kushinda uchaguzi wa urais uliofanyika hapa Jumamosi iliyopita.
Jean Ping aliwaambia wafuasi wake kuwa ameshinda uchaguzi huo na anamsuburi Rais anayemaliza muda wake kumpongeza.
Na kwa upande wa timu ya Rais Bongo imesema inaendelea na awamu nyingine madarakani.
Kufuatia mvutano huo wa pande hizo mbili, wizara ya mambo ya ndani imesema si halali kwa mtu yeyote kutangaza matokeo, isipokuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi pekee.
Jean Ping, kiongozi wa zamani katika Umoja wa Afrika anajaribu kuuondoa madarakani utawala wa familia ya Bongo, ambayo imekaa madarakani kwa karibu miaka 50.
‘Uamuzi uliochukuliwana wengi unajulikana sasa kwa kila mtu. Gabon ni nchi ndogo na hivyo ni rahisi kujua matokeo yote,” aliwaambia wanahabari.
Ping (73) alisema amechukua hatua hiyo ya kujitangaza mshindi kuzuia Bongo (57) asichakachue matokeo akikumbushia kilichotokea mwaka 2009 wakati matokeo yalipokaribiana.
Akijibu madai ya Ping, Bongo alisema kwamba anasubiri kwa utulivu matokeo na ana imani ya kushinda.