WAZIRI Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, amewataka Watanzania kuachana na mila zinazoruhusu ndugu kuchukua mali za marehemu.
Badala yake, ametaka mila hizo zizuie utaratibu huo ili mali hizo zitumiwe na mke na watoto wa marehemu.
Pinda aliyasema hayo juzi wakati wa mazishi ya aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kasansa Halmashauri ya Mpimbwe, Wilaya ya Mlele, Sixto Chalahani.
“Ndugu wa marehemu wanapaswa kuachana na utamaduni huo wa kugombania mali za marehemu kwani unasababisha mjane wa marehemu na watoto kuhangaika .
“Watoto na mjane aliyeachwa na marehemu, wanaendelea na masomo na kama mali zilizochwa na marehemu zitakwisha, jamii iendelee kusaidia kadiri inavyowezekana.
“Katika Kabila la Wapimbwe ninalotoka mimi, mwanamume anapofariki, tuna utamaduni wa ndugu wa upande wa mume kugawana mali za marehemu na kuwaacha mjane na watoto wa marehemu wakihangaika mitaani.
“Kwa hiyo, naomba tuache utaratibu huu kwa sababu si mzuri na unarudisha nyuma maendeleo,” alisema Pinda.
Wakati huo huo, Pinda aliwataka wananchi wa kata hiyo kuanza kujiandaa na uchaguzi mdogo kwa kufikiria ni nani atakuwa diwani wao atakayeendeleza aliyoacha marehemu Chalahani.
Chalahani alikuwa ni Diwani wa Kata ya Kasansa tangu mwaka 2010 hadi alipofariki Agosti 23 mwaka huu, akitibiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa.