Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
SEKTA binafsi inazidi kuathiriwa na sera za uwekezaji katika ngazi ya Taifa.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye, wakati wa akifunga mkutano uliojadili mpango wa mazingira ya kuimarisha biashara Tanzania ulioandaliwa na Taasisi ya BEST-AC.
Alisema wamedhamiria kuhakikisha kuna mazingira mazuri ya biashara kwa umma na lazima yawe endelevu bila kujali kiwango cha maendeleo katika nchi.
“BEST AC imekuwa ikiendesha shughuli zake nchini kwa miaka 10 sasa na ninakiri kwamba pale tulipo hivi sasa si kama ilivyokuwa mwanzo,” alisema Sembeye.
Alisema BEST-AC imekuwa endelevu sehemu kubwa katika programu zake na mradi huo umeleta manufaa makubwa katika sekta binafsi na kufanya kuwepo kwa mwingiliano endelevu wa mafunzo kwa pande zote.
Alipongeza uamuzi uliotolewa na Serikali wa kufanya mazingira ya biashara kwa Taifa kama matokeo muhimu.
Alisema TPSF ilikuwa na wasiwasi suala la urasimu halijawahi kujadiliwa katika mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwa mazingira ya biashara.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa President’s Delivery Bureau (PDB), Peniel Lyimo, alipongeza BEST-AC kwa jukumu lake la kusaidia sekta binafsi kwa ajili ya kutetea mazingira bora ya biashara.
“BEST-AC wamefanya kazi nzuri na mchango wao ni mkubwa sana katika sekta hiyo,” alisema Lyimo.