29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

MATUKIO YA MOTO SHULENI Mazingira ya kusomea ni salama?

Shule ya Sekondari Lindi.
Shule ya Sekondari Lindi.

NA NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM

KWA zaidi ya miezi miwili sasa kumekuwa na matukio ya kuungua moto kwa baadhi ya shule za sekondari mkoani Arusha ambapo hadi sasa shule sita zimeungua.

Matukio hayo yanaacha maswali mengi vichwani mwa watu bila majibu, wako wanaodhani kwamba huenda ni hujuma, itilafu za umeme, migogoro ya ardhi na wengine wakienda mbali zaidi na kuyahusisha na masuala ya kisiasa.

Katika matukio hayo ziko shule zimeungua mara moja na zingine zilizoungua mara mbili mfululizo hatua inayozidi kuleta hofu kwa wanafunzi, walimu na wazazi.

Picha ya matukio ya moto yaliyowahi kutokea miaka ya nyuma ambapo mengine yalisababisha wanafunzi kupoteza maisha bado haijafutika vichwani mwa watu.

Wengi bado wanakumbuka tukio kubwa lilitokea katika Shule ya Sekondari ya Shauritanga iliyoko mkoani Kilimanjaro na kuteketeza wanafunzi 40 na tukio la Shule ya Sekondari Idodi mkoani Iringa ambapo wanafunzi 12 walifariki dunia.

Shule ya Sekondari Idodi iliungua mara mbili ambapo tukio la mara ya pili lilisababisha mabweni kuungua moto na kusababisha madogoro 190, madogoro 48, mashuka na vitu mbalimbali vya wanafunzi hao kuteketea.

Athari za matukio ya moto shuleni ni kubwa kwani licha ya kuwaathiri kisaikolojia wanafunzi pia yanashusha kiwango cha elimu, yanawafanya wasome kwa shida na wengine kushindwa kabisa kutokana na kuunguliwa vifaa vyao.

Baadhi ya shule zilizoathiriwa na matukio haya zimekuwa zikifungwa kwa muda kupisha ukarabati na hivyo kuzidi kuleta ugumu hasa kwa wanafunzi ambao wanajiandaa na mitihani ya kitaifa ya Kidato cha Pili na Nne.

ARUSHA

Matukio ya hivi karibuni ya moto yametokea katika shule sita za sekondari mkoani Arusha na kuzua sintofahamu.

Ilianza kuungua Shule ya Sekondari Lowassa iliyopo Halmashauri ya Monduli, Nanja na Longido sekondari zilizopo Halmashauri ya Longido, Sokoine sekondari iliyopo Halmashauri ya Monduli, Mlangarini sekondari iliyopo Halmashauri ya Arumeru na Shule ya Sekondari Winning Spirit.

Pia Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Engutoto, nayo iliingua moto mwanzoni mwa mwaka huu.

LINDI

Mwanzoni mwa mwezi uliopita Shule ya Sekondari Lindi, nayo iliungua moto na kusababisha madarasa tisa, samani, ofisi nne za walimu, maabara mbili za kemia na fizikia na madawati 300 kuteketea kwa moto.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, anasema uchunguzi kubaini chanzo cha moto na tathmini ya mali zilizoteketea bado unaendelea.

MBEYA

Februari mwaka huu, majengo mawili ya Shule ya Sekondari Iyunga iliyoko mkoani Mbeya, yaliungua moto na kusababisha magodoro, nguo na vifaa vingine vya wanafunzi kuungua.

SHULE ZINGINE

Mwaka 2008 mabweni ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Mkalamo iliyoko Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga yaliteketea pamoja na vifaa mbalimbali vya wanafunzi ambapo lilikuwa ni tukio la pili kutokea shuleni hapo.

Mwaka 2008 bweni la Shule ya Sekondari Singe iliyopo mkoani Singida liliteketea ikiwa ni wiki moja baada ya bweni lingine kuungua moto.

Mwaka huo huo pia, bweni la Shule ya Sekondari Moita liliteketea na mwaka 2009 tena bweni lingine liliungua.

Mwaka 2003, mabweni ya wasichana katika Shule ya Sekondari Marangu mkoani Kilimanjaro, yaliungua moto na kusababisha kifo cha mwanafunzi mmoja.

Pia Shule za Sekondari Machame, Useri na Kikatiti nazo ziliwahi kukumbwa na matukio hayo ya moto.

WAKUU WA SHULE

Mkuu wa Shule ya Sekondari Erikisongo iliyoko Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, Temu, anasema zaidi ya wanafunzi 169 walionguliwa na bweni lao wanahitaji msaada zaidi kwa sababu nguo zao na vitu vingine vimeungua.

Wanafunzi hao wanalala kwenye vyumba vya madarasa huku wakisubiri ujenzi wa bweni kukamilika.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Iyunga, Edward Mwantimwa, anasema ukarabati wa majengo yaliyoungua umekamilika na tayari baadhi yameanza kutumika.

Hata hivyo anasema shule hiyo inakabiliwa na uchakavu wa majengo kwani yaliyopo ni chakavu kutokana na kujengwa muda mrefu tangu mwaka 1925 hivyo kuhatarisha maisha ya walimu na wanafunzi wanaoyatumia.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Lindi, Honorati Tarimo, anasema chanzo kikubwa kinasadikiwa kuwa ni itilafu ya umeme.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Mlangarini, Elias Pallakyo, anasema moto uliteketeza vitanda 42 na vifaa mbalimbali vya wanafunzi zikiwamo sare za shule na masanduku ya kuhifadhia vifaa vyao.

WANAFUNZI

Muyo Jacob na Lomnayaki Mitawas ni wanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Mlangarini, wanaiomba serikali iwasaidie ili wenzao walioko nyumbani waweze kurejea kwani wanakabiliwa na mtihani wa kidato cha nne ulioko mbele yao.

HATUA ZILIZOCHUKULIWA

Tayari watuhumiwa 27 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kuhusishwa na matukio ya moto mkoani Arusha.

Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Zima moto na Uokoaji mkoani Arusha, Bakari Mrisho, anasema kikosi chake kimefanya uchunguzi katika shule tano za bweni zilizoungua awali na kujirishisha kuwa ni hujuma za kibinadamu zimesababisha kuungua kwa mabweni hayo.

“Kwa sasa tumejielekeza kufanya ukaguzi katika shule za bweni na kuangalia iwapo zina uwezo wa kukabiliana na majanga ya moto,” anasema Mrisho.

NINI KIFANYIKE

Matukio haya yanasababisha watu kuogopa kuwaweka watoto wao mashuleni, hivyo ni dhahiri kuwa yanarudisha nyuma maendeleo ya elimu nchini.

“Kama tunataka kujenga elimu safi, kuweka misingi imara ya kuwawezesha wanafunzi kuelewa, ni lazima mazingira ya kusomea yawe salama, bila hivyo matukio haya yatasababisha kiwango cha elimu kushuka,” anasema Profesa Gaudence Mpangala ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO).

Anashauri majengo ya shule yajengwe kwa mfumo utakaowezesha kukabiliana na majanga ya moto.

Naye Mwalimu Ernest Asenga, anashauri ufanyike uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha matukio hayo.

“Suala la umiliki wa ardhi katika baadhi ya shule nalo linatajwa sana kwamba huenda likawa linachangiwa kuwapo kwa matukio haya, hivyo nashauri umiliki wa ardhi husika uchunguzwe ili kama kuna watu wenye dukuduku basi mamlaka zinazohusika zikutane nao kuondoa tofauti zilizopo,” anasema Mwalimu Asenga.

Mazingira salama ya kusomea ni muhimu kwa wanafunzi wawapo shuleni kwani huongeza mafanikio ya elimu na kukuza maarifa, hivyo ni vema matukio haya yatumike kama darasa ili kudhibiti matukio mengine yasitokee.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles