23.7 C
Dar es Salaam
Saturday, September 23, 2023

Contact us: [email protected]

Babu wa miaka 91 anywa mkojo kurudi ujanani

Mark Ambrose akiwa na mwenzi wake.
Mark Ambrose akiwa na mwenzi wake.

NA JOSEPH HIZA,

KATIKA zama ambazo watu huhaha kutafuta ujana kwa namna mbalimbali ikiwamo upasuaji, vidonge hadi krimu zenye kemikali na athari kiafya. Kuna njia ambayo inaaminika ni nafuu zaidi kuanzia upatikanaji wake, gharama hadi madhara, ambayo hata hivyo si wengi wenye ujasiri wa kuitumia.

Naam, si wengi wenye ujasiri wa kutosha kunywa mkojo wao wenyewe, licha ya kwamba hilo linaweza kuwafanya waonekane wadogo hata miaka 10 tofauti na umri wao.

Lakini mzee mwenye umri wa miaka 91 Mark Ambrose ana ujasiri huo na anasisitiza kuwa maji haya kutoka mwili mwa binadamu ni ufunguo tosha wa mwonekano wake wa ujana na staili yake ya maisha ya kujishughulisha.

Ambrose, ambaye anaishi na mwenzi wake wa miaka 87,  Joyce, kusini mwa Hispania, hunywa glasi ya mkojo wake kila siku.

Pia huutumia kuweka katika majeraha akiamini unasaidia mchakato wa uponyaji.

Ambrose aliliambia gazeti la MailOnline: “Joyce na mimi wote tuna matatizo makubwa ya kiafya ambayo yanapaswa kushughulikiwa.

“Niliumia vibaya uti wa mgongo na mwenzangu anakabiliwa na maradhi ya misuli, magoti ambayo huhitaji kubadilishwa na maumivu mengine ya kawaida yanayohusiana na uzee.

“Hata hivyo, tunaendesha maisha ya kujishughulisha na marafiki wanasema naonekana mdogo tofauti na ukubwa wa umri wangu, na mwenza wangu anaonekana kuwa na nishati akionekana na umri si zadi ya miaka 65-70,” anasema.

Mkurugenzi huyo wa zamani wa uenezi anasema: “Kwa kadiri nijuavyo, ninaamini mkojo ni tiba kamili, ambayo niliianza kuitumia miaka mitatu iliyopita na ndiyo chanzo cha mwonekano wangu wa ujana.”

Ambrose anakiri kuwa alijikuta akiingia katika kile anachopenda kuita chanzo cha ujana kwa bahati tu wakati alipokuwa akitafuta tiba ya maumivu yake ya mgongo kwa njia ya mtandao.

Anaeleza: “Nilishapitia operesheni tatu ikiwamo ya kuwekewa hogo nchini Marekani na Hispania huku wataalamu wakikiri kutokuwa na njia mbadala zaidi ya kumsaidia kuua maumivu yanayomkabili.

“Nikiwa sina cha kupoteza, nilidhani napaswa kujaribu tiba ya kusaidia kunipatia maisha bora kwa miaka yangu iliyobakia.”

Alianza kwa matamanio kutafiti nini anachohitaji kufanya, lakini hakupata chochote kipya cha kumsaidia.

Lakini mwishowe akakutana na suala la maajabu ya mkojo katika kutibu maradhi mbalimbali.

Kwa sababu hiyo, Ambrose hayuko pekee duniani ya watu wanaoamini na kuitumia tiba hiyo, ambayo ipo tangu nyakati za Kibiblia.

Nyaraka za kihistoria zinaonesha mkojo huweza kusafisha majereha huku manufaa yakielezwa katika riwaya nyingi za India na China.

Kwa mujibu ya watalaamu, mkojo ni mchanganyiko wa asilimia 95 za maji na asilimia tano za madini yanayotoka baada ya mmeng’enyo wa chakula kufanyika mwilini.

Madini hayo ni pamoja na urea, chloride, sodiamu, potassiamu na chuma.

Baada ya kula na mmeng’enyo kufanyika, maji pamoja na mabaki yaliyomeng’enywa husafirishwa katika kibofu cha mkojo.

Maji hayo ndiyo husaidia kufanya usafirishaji wa mabaki hayo hadi katika kibofu cha mkojo.

Nchini India, kwa mfano tiba ya mkojo inaitwa ‘shivambu’.

Jina hilo likimaanisha ‘dawa ya hekima’  ambayo ilitangazwa zaidi na Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Morarji Desai.

Desai ambaye alifariki dunia mwaka 1995 akiwa na umri wa miaka 99, alidiriki kuutangazia umma kuwa anakunywa mkojo wake wa asubuhi kila siku na hiyo ndiyo siri ya afya njema na maisha marefu.

Lakini pia inaelezwa kuwa mkojo una utajiri wa protini na madini mengine ambayo huweza kutumika katika matibabu na pia ni miongoni mwa vichanganyo katika dawa nyingi, kwa mfano dawa za ureacini, urecholin na urowave.

Watetezi wa tiba ya mkojo wanaamini kwamba viungo hivyo vina faida kuanzia kuimarisha mfumo wa kinga hadi macho na masikio.

Akitiwa moyo na suala hilo, Ambrose aliamua kufanya jaribio.

Anakumbuka: “Kuchukua sampuli katika glasi ndogo ni rahisi kwa mwanamume kuliko mwanamke, nadhani – kwa uangalifu nilionja na kuona kimiminiko hiki cha rangi ya kaharabu kipo poa.

“Haikuwa mbaya sana, niliona – ladha isiyo ya kawaida, kitu ambacho sikuwahi kuonywa kabla. Si nzuri wala kufurahisha, lakini kwa upande mwingine haikuwa ya kuchukiza mno.”

Akiwa na dhamira ya kuendelea, kipindi cha siku chache zilizofuata aliendelea kuufyonza mkojo wake hadi alipopata ujasiri wa kutosha kuunywa.

Alianza kufyonza kidogo kidogo, kisha kunywa kidogo kidogo kila alipoenda haja ndogo na  taratibu akaongeza kiwango kwa kadiri wiki zilivyopita na kufanikiwa kunywa glasi.

Kuhusu kubakia na harufu ya mkojo mdomoni, anasema kusafisha mdomo haraka kwa maji kunasaidia kuondoa.

Miaka mitatu imepita kwa sasa amekuwa mtalamu wa kunywa mkojo na namna unapaswa kuonekana.

“Nilijifunza mtu anapaswa kuona rangi ya maji ya mwenzake na kufanywa iwapo si nyeupe sana au yenye rangi sana.

Kwa maana hiyo, anasema sahau kunywa mkojo mweupe. “Iwapo ni mweupe basi hauna radha na ninadhani haufai kuwa wakala wa uponyaji,” anashauri.

Na kwa upande mwingine anasema iwapo mkojo ni njano mno, unaonekana mzuri lakini ngumu kwake kuutumia, pamoja na kuwa na uwezekano wa faida kubwa.

Anasema anakunywa nusu glasi ndogo ya mkojo mara nyingi kwa kadiri awezavyo kwa siku za kawaida.

Pia anasugua ngozi yake kwa mkojo ikiwamo usoni, miguuni na mikononi hadi machoni na masikioni.

“Mwili wangu sasa uko bomba na marafiki na wageni wengi wanashangazwa na mwonekano wangu usioendana na umri mkubwa nilio nao,” anasema.

“Nadhani naonekana kuwa miaka 10 pungufu ya niliyo nayo. Nina leseni ya udereva ya Hispania, nafanya mapishi yote mwenyewe na niko chini ya Klabu ya ambayo nilisaidia kuianzisha miaka 20 iliyopita na ninajifunza kupiga piano.

Lakini wakati mwenzake Joyce ingawa anafurahishwa na matunda ya juhudi zake, anashindwa kukabiliana na hisia za kunywa mkojo wake mwenyewe.

Nilimshawishi lakini amepinga kunywa tiba hii, anakiri.

Maajabu mengine ya mkojo

Wanayansi na watafiti nchini Uingereza walivumbua nguvu za mkojo katika kuzalisha nishati ambayo inaweza kuchaji simu kwa muda wa dakika 25 na pia kumwezesha mteja kutuma ujumbe na kuperuzi intaneti.

Watafiti hao  kutoka Chuo Kikuu cha Watafiti cha Bristol wakishirikiana na wenzao wa Maabara ya Robot wanasema kuwa nishati hiyo ya mkojo ni mapinduzi ambayo yatasaidia katika upungufu wa nishati wakati wowote badala ya kutegemea jua au upepo.

Timu ya watafiti hao iliweka mkojo katika chombo maalumu ambao baada ya muda huzalisha bakteria.

Bakteria hao baada ya kuwa na njaa huzalisha nguvu za kielektroni na kuwa nishati. Elektroni hizo hudondoshwa katika kontena maalumu kwa ajili ya kuhifadhiwa.

Mmoja wa wahandisi aliyevumbua nguvu za mkojo, Dk. Ioannis Ieropoulo, wa Chuo Kikuu cha West of England (UWE), Bristol anasema, mkojo ni bidhaa ambayo haiwezi kutupungukia tofauti na bidhaa nyingine kama maji, upepo au jua.

Wavumbuzi hao wanasema mkojo ni nishati inayopatikana wakati wowote hivyo hatua hiyo inasaidia kuwa na uhakika wa kutopungukiwa na nishati hata kwa watu wa vijijini.

Anaongeza kuwa madhumuni ya uvumbuzi huo ni kupata nishati inayopatikana wakati wowote, rahisi kuiunda na itakayowasaidia watu wengi wa matabaka mbalimbali.

“Tumevumbua na tumehakikisha kuwa inafanya kazi. Kilichobaki sasa ni kuangalia uwezekano wa mkojo kutumika katika matumizi ya nyumbani,” anasema mhandisi huyo.

Mpaka sasa betri iliyoundwa kwa nishati ya mkojo huo ina uwezo wa kuchaji simu itakayoweza kudumu kwa dakika 25, kutuma ujumbe na kupiga simu kwa sekunde 20.

Wanasayansi wanaamini kuwa teknolojia hiyo ina manufaa makubwa katika jamii kwani huenda ikatumika katika bafu na vyoo na kuzalisha nguvu ya umeme kwenye mabomba ya bafuni, taa na kuchaji simu.

Hata hivyo mkojo hauna manufaa katika nishati na tiba pekee, bali hivi karibuni watafiti wamedai kwamba mkojo unaweza pia kutumika kutengeneza pombe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,699FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles