NA ESTHER MNYIKA, DAR ES SALAAM
AHADI ya Rais Dk. John Magufuli ya kutoa Sh milioni 50 kila kijijini nchini imeanza kuingia doa baada ya watu wasiokuwa waaminifu kuanza kuwadanganya wananchi kwamba fedha hizo zitapitia kwenye taasisi zao.
Hayo yalibainishwa jana na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).
NEEC iliwatahadharisha wananchi kuwa kuna baadhi ya taasisi na watu binafsi wanawadanganya wananchi kuwa fedha hizo zinapitia kwenye taasisi zao, hivyo kuwataka wananchi kujisajili kwao ili waweze kufaidika na fedha hizo.
Taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Katibu Mtendji wa NEEC, Beng’i Issa, ilisema watu na taasisi hizo zinazowadanganya wananchi wamekuwa wakiwatoza viwango mbalimbali vya fedha kwa kile wanachodai kuwa ni ada ya usajili ili waweze kufaidika na mpango huo.
“Taasisi hizi zinawadanganya wananchi, zimekuwa zikiwatoza viwango mbalimbali vya fedha kwa kile wanachodai ni ada ya usajili ili vikundi hivyo vya wananchi viweze kusajiliwa na kutambulika kuweza kufaidika na mpango huu.
“Kutokana na hali hiyo, Baraza halijamtuma mtu binafsi au taasisi yoyote kwenda kwa wananchi kuahidi jambo lolote kuhusiana na mpango huu, hivyo ikibainika wanadanganya wananchi kwa kuwatoza fedha za usajili, watachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema.
Alisema kuwa Serikali ipo hatua ya mwisho kukamilisha utaratibu wa utekelezaji wa mpango huo na utakapokamilika, taarifa itatolewa kwa umma kupitia vyombo vya habari.
Akiwa kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana, Rais Magufuli aliahidi kutoa Sh milioni 50 kila kijiji ili kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi.