MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amesema chama hicho kimeshajiandaa vya kutosha kwa ajili ya kufanya maandamano yatakayofanyika Septemba mosi.
Amesema kwamba kwa kuwa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia nay a watu wote, haiwezekani mtu mmoja azuie demokrasia.
Lowassa aliyasema hayo jana mjini Tunduma, mkoani Songwe, alipokuwa akizungumza na wanachama wa chama hicho katika mkutano wa ndani uliolenga kuweka mikakati ya kufanikisha kile wanachokiita Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta).
“Ukuta siyo fujo, Ukuta siyo machafuko bali Ukuta unalenga kupiga kelele dhidi ya uvunjwaji wa haki ya kidemokrasia na katiba ya nchi, unaofanywa na utawala huu wa awamu ya tano.
“Hivi Chadema ni nani wakapambane na polisi ambao ni watoto wetu, ndugu zetu na hata wake na waume zetu?
“Ila tunawahakikishia hatutorudi nyuma pale katiba na haki ya kidemokrasia itakapochezewa au kuwa chini ya mtu fulani.
“Najua polisi watapiga watu, wataumiza watu na hata kuua, ila niwahakikishie wao na walio na mamlaka wataishia katika mahakama ya kimataifa,” alisema Lowassa.
Pamoja na msimamo huo, Lowassa ambaye aligombea urais kupitia Chadema wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka jana, alisema chama chake bado kimefungua milango ya mazungumzo kwa vyombo vinavyohusika kabla ya Septemba mosi.
“Milango yetu bado iko wazi kwa ajili ya mazungumzo ila kwa kuwa hawahitaji, na sisi hatutorudi nyuma Septemba mosi kwa kuwa tumejiandaa vya kutosha.
“Kwa sasa tuko ngazi ya kaya na nyinyi wajumbe mkakamilishe kazi katika kaya zenu ili tarehe mosi sauti ya kutosha ipazwe kwa maandamano na mikutano kama tulivyokubaliana katika kata zetu na majimbo nchi nzima.
“Haiwezekani hata kidogo mtu mmoja azuie kila kitu, nchi hii ni mali yetu sote. Kitendo cha Serikali ya awamu ya tano cha kupiga mafuruku mikutano ya siasa ni uvunjwaji wa kanuni na katiba ya nchi, ibara ya 20 (1).
“Vilevile ni ukiukwaji wa sheria namba 5 ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 kifungu cha 11.
“Kwahiyo, eleweni kwamba Kamati Kuu yetu ilipoamua katika suala la Ukuta haikukurupuka kwa sababu inaundwa na mchanganyiko wa wasomi wa kada mbalimbali, wakiwamo wazee wenye busara na vijana machachari. Na pia Ukuta ni haki ya Watanzania wote,” alisema.
Katika maelezo yake, Lowassa alitolea mfano kiongozi mmoja wa Ujerumani aliyemtaja kwa jina la Martin Nimolar aliyejitokeza kupinga ukandamizaji wa demokrasia wakati unaanza nchini humo.
“Kule Ujerumani wakati ufashisti unaanza, yupo mchungaji mmoja aliyefahamika kwa jina la Martin Nimolar, ambaye alisema ‘at first they came’ na na sisi tuna wimbo huu huu katika Ukuta.
“Awali walifungia matangazo ya Bunge ‘live’, hatukusema kwa kuwa sisi si wabunge, lakini sasa tunaamua kusema,” alisema.
Pamoja na hayo, mwanasiasa huyo aliwapa matumaini ya ushindi wa urais mwaka 2020 wafuasi wa chama hicho kwa kusema uko wazi iwapo tu wataamua kushikamana.
Alisema kwamba kama watakuwa na umoja, wakiheshimiana, wakisameheana na kuimarisha chama ndani na nje ya chama pamoja na kwa wananchi, hakuna kitakachokwamisha.
Pamoja na hayo, aliwashukuru wananchi wa Mbeya kwa kura walizompa wakati wa uchaguzi mkuu na kuwataka wasikate tamaa kwa kuwa nafasi ya ushindi bado ipo.
Awali, wakati anawasili mjini Tunduma, Lowassa alipokewa na mamia ya wananchi na kusababisha baadhi ya biashara na huduma za kijamii kufungwa.
Kutokana na wingi wa watu, askari polisi waliokuwa na silaha za moto, walianza kuwatawanya, jambo ambalo lilisababisha vurugu zilizodumu kwa dakika kadhaa.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chadema , Mkoa wa Songwe, Jicva Jivava, aliahidi kuyafanyia kazi maagizo yote waliyopewa kwa kuwa wako tayari kuimarisha Ukuta.
Lowassa na timu yake, kesho wataendelea na ziara mkoani Katavi na Rukwa kwa ajili ya kuendelea na vikao vya ndani.
BAVICHA
Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) limesema maandamano ya Ukuta yatafanyika nchi nzima kama ilivyopangwa awali bila kujali nguvu yoyote itakayotumiwa na Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, Patrobas Katambi, alisema maandamano hayo ni halali na yapo kwa mujibu wa sheria.
Alisema wamelazimika kutoa ufafanuzi wa uhalali wa Ukuta kutokana na alichodai kuwa viongozi wa Serikali, hasa wakuu wa mikoa, wamekuwa wakipotosha kwa kutoa matamko ambayo yanaleta mgawanyiko kwa jamii.
“Sasa hivi watu wameanza kubaguliwa kiitikadi… Ma-DC wanamdanganya Rais Dk. John Magufuli na tunafikiri pengine mwenyewe hajui hilo, Chadema tutasema ukweli kupitia Ukuta… tunataka kumsaidia Rais. Hali si shwari, lakini viongozi wamekuwa wakipeleka taarifa za uongo ili wasitumbuliwe,” alisema.
Alisema wanalaani vikali upotoshwaji wa makusudi au wa kutojua mamlaka, haki na wajibu wa vyama vya siasa kwa mujibu wa sheria unaofanywa na baadhi ya viongozi wa jeshi la polisi na wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Wamo baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya ambao Katiba ya CCM ya 1977 inawataja kuwa ni wajumbe wa mkutano mkuu na wajumbe wa kamati za siasa za ngazi ya wilaya na mikoa, kwa mujibu wa kifungu cha 76 na 90 vya katiba hiyo, wana masilahi ya kisiasa nyuma yao, kupambana dhidi ya vyama vya upinzani wakitumia mgongo wa dola kwa kilemba cha wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama,” alisema.
POLISI NA UKUTA
Wakati Chadema ikiendelea kuwatawanya viongozi wake katika mikoa mbalimbali nchini kwa ajili ya maandalizi ya Operesheni Ukuta, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limeeleza kuwa Ukuta huo umevunjika baada ya kubaini mbinu za maandalizi yake.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, alisema askari wake wamejiandaa vizuri kupambana na Ukuta na kueleza kwamba ukuta huo tayari umebomoka kabla ya kufika Septemba Mosi mwaka huu.
Viongozi hao tayari wametawanywa katika mikoa mbalimbali ambapo Edward Lowassa yupo Mbeya, John Mnyika na Salum Mwalimu wapo Mara, Dk. Vicent Mashinji yupo Mwanza, Freeman Mbowe, Godbles Lema, Kilimanjaro na Arusha na Frederick Sumaye yupo Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi linamshikilia Yoramu Seth (42) mkazi wa Mburahati kwa kosa la kuuza fulana zenye maneno ya kichochezi, zikiwa na alama ya Chadema.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, alisema mtuhumiwa huyo amekamatwa akiwa na flana zaidi ya 200 dukani kwake.
Alisema fulana hizo zenye rangi nyekundu, nyeusi, kaki na nyeupe, zina maneno yaliyoandikwa “Tujipange tukatae udikteta uchwara”, “Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania” na “Ukuta”.
“Tulipata taarifa toka kwa raia wema kwamba katika Mtaa wa Ufipa, Kinondoni kuna duka linauza fulana mbalimbali zenye maneno ya uchochezi, askari wetu walifika na kuona t-shirt hizo na zote tumezichukua,” alisema.
Habari hii imeandaliwa na Veronica Romwald, Asifiwe Geogre na Grace Shitundu (Dar)