26.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mayanja: Simba ya leo si ya jana

DSC_8301

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

KOCHA msaidizi wa timu ya Simba, Jackson Mayanja, amesema kikosi cha Simba cha sasa kina tofauti kubwa na cha msimu uliopita, kwani wachezaji walionao wana uwezo tofauti na wale wa msimu uliopita.

Wekundu hao wa msimbazi msimu huu, wamelamba dume kwa kusajili wachezaji wenye uwezo, ambapo kila mmoja anaweza kuitendea haki nafasi yake.

Juzi Simba ilifanikiwa kuwa na mwanzo mzuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa kuifunga timu ya Ndanda bao 31 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Mayanja alisema wamefurahishwa na ushindi walioupata katika mchezo wao.

“Mchezo ulikuwa na ushindani mkubwa lakini tunashukuru tumefanikiwa kupata pointi tatu muhimu katika mchezo wetu wa kwanza, hivyo tutaendeleza ushindi huu  katika michezo mingine,” alisema Mayanja.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Idara ya mawasiliano wa klabu hiyo, Haji Manara, alisema kikosi hicho kitaendelea na mazoezi leo, lakini kesho wataingia kambini rasmi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo dhidi ya JKT Ruvu.

“Wachezaji wote watafanya mazoezi pamoja na kocha atayafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo uliopita na Jumanne wataingia rasmi kambini,” alisema.

Wakati huohuo, kocha msaidizi wa timu ya Ndanda FC, Hamimu Mawazo, alisema ana kazi kubwa kuhakikisha anakinoa zaidi kikosi chake, ili kifanye vizuri kwenye michezo yake ya ligi inayofuata.

Mawazo alisema ameanza kuinoa timu hiyo huku usajili ukiwa umeshafanyika, hivyo atalazimika kuwaongezea makali ili kupata matokeo mazuri.

“Tunawapongeza Simba kwa kupata ushindi lakini kufungwa katika mchezo ni kitu cha kawaida, isipokuwa tutayafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo huo, ili yasijitokeze kwa mara nyingine,” alisema.

Alisema atawaongezea nguvu zaidi viungo wake ambao walionekana kupwaya kwenye mchezo huo ili waimarike zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles