Yaliojiri ufunguzi Ligi Kuu Tanzania Bara 2016/17

 2

ZAINAB IDDY NA BADI MCHOMOLO

BAADA ya miezi mitatu ya mapumziko, usajili na maandalizi ya jumla, pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2016/17, limefunguliwa rasmi Jumamosi iliyopita kwa kucheza michezo sita kwenye viwanja tofauti kabla ya kumalizia mmoja uliochezwa jana.

Timu zilizoshuka dimbani Jumamosi ni pamoja na Simba waliowaalika Ndanda kwenye uwanja wa Taifa, Majimaji waliwakaribisha Tanzania Prisons, Ruvu Shooting iliyopanda daraja ikiwa ugenini Maungu Comlex dhidi ya Mtibwa Sugar, Azam wakiwa nyumbani kuwaalika Africans Lyon iliyopanda daraja huku ndugu zao Mbao FC wakiwa ugenini kukipiga na Stand United.

Mchezo mwingine wa mzunguko wa kwanza ulichezwa Jumapili kati ya Mbeya City waliokuwa ugenini mbele ya Kagera Sugar, huku mechi ya kukamilisha mzunguko huo kati ya Yanga na JKT Ruvu ikisogezwa mbele hadi Agosti 31, ili kutoa nafasi kwa Wanajangwani kukamilisha ratiba yao ya michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho wakiwa ugenini dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.

Katika michezo sita iliyoshiriki pazia la Ligi Kuu, yapo mengi yaliyojiri kwenye mechi hizo za ufunguzi na SPOTI KIKI inakuletea baadhi ya mambo hayo ambayo huenda yakawa ni tofauti au sawa na misimu iliyopita kwenye mechi za kwanza.

Simba kiboko

Simba ambayo imefungua dimba na Ndanda FC kwenye uwanja wa taifa Dar es Salaam, imeendelea kuwa tishio katika mchezo wake wa ufunguzi wa ligi, baada ya kuendeleza rekodi ya kutoruhusu pointi kuondoka mikononi mwao kwa misimu tisa sasa.

Tangu ilipofungwa msimu wa 2007/8 bao 1-0 dhidi ya Coastal Union, Simba haijapoteza mechi yoyote ya ufunguzi kwani hadi sasa imeshinda mara saba na kutoka sare mbili.

Imeshinda mabao 4-1 msimu wa 2008/09 dhidi ya Villa Squad, 2-0 dhidi ya Majimaji 2009/10, 2-0 mbele ya, Africans Lyon 2010/11, 2-0 kwa JKT Oljoro 2011/12, 3-0 dhidi ya African Lyon 2012/13, sare ya 2-2 mbele ya Coastal Union 2014/15,  ushindi wa 1-0 dhidi ya Africans Sports  2015/16 na msimu huu ulioanza Jumamosi wameweza kupata ushindi wa 3-1 kutoka kwa Ndanda FC.

Azam FC haipotezi mchezo Chamanzi

Azam imefungua dimba kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Azam Complex uliopo chamanzi dhidi ya African Lyon.

Wanalambalamba hao hawajawahi kupoteza mechi yoyote ya ufunguzi kwenye uwanja wake huo tangu mara ya mwisho msimu wa 2008/09 ilipokubali kipigo cha mabao 3-2 dhidi ya Moro United, Tangu ilipoingia katika kipusa cha Ligi Kuu Tanzania Bara, imecheza mechi sita sasa za ufunguzi kwenye uwanja huo, ikishinda michezo minne na kutoka sare moja.

Msimu wa 2010/11, ilifungua dimba na African Lyon na kuichapa 2-0, 2011/12 ikashinda 1-0 dhidi ya Moro United na kupata sare ya 1-1 mbele ya Mtibwa Sugar, 2013/14 ikaifunga 3-1 Polisi Morogoro, 2014/15, ukaitandika 2-1 Tanzania Prisons msimu uliopita na msimu huu imetoka sare ya 1-1 dhidi ya Africans Lyon.

Ndanda FC bado ‘vilaza’ Taifa

Wakali wa Mtwara ‘Ndanda Kuchele’, wameendelea kuonekana si lolote si chochote, hawapo kwenye dimba la taifa, Dar es Salaam.

Tangu ipande daraja misimu miwili iliyopita, Ndanda imeshindwa kuondoka na pointi tatu katika uwanja wa taifa, kwani imecheza mechi tano hadi sasa ambapo imepata sare mbili huku ikifungwa mara nne.

Waliopanda wang’ara

Timu zilizopanda daraja msimu uliopita na kushiriki Ligi Kuu msimu huu Ruvu Shooting, Mabo FC na Africans Lyon, zimeanza ligi vizuri baada ya kila mmoja kuondoka na pointi kibindoni huku zikiwa ugenini.

Ruvu ambayo ilikuwa ugenini mkoani Morogoro, waliondoka na pointi tatu baada ya kuwafunga wenyeji wao Mtibwa Sugar, bao 1-0 katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Mnaungu Complex Turiani.

Kwa upande wa Mbao FC ambao wamepanda daraja kwa zali, wakiwa ungenini kwenye uwanja wa Kambarage Shinyanga wakicheza za Stand United, waliweza kutoka sare na hivyo kuondoka wakiwa na pointi moja kibindoni.

Africans Lyon jana ilionyesha kuwa haikuja kutembea baada ya kuiburuza Azam katika dakika 90 za mchezo wakiwa mbele kwa bao 1, kabla ya Wanalambalamba kuchomoa dakika ya 93 kupitia kwa Bocco na hivyo matokeo kuwa ya sare ya 1-1 na kujikuta wakiondoka na pointi moja mfukoni.

Mechi tano, mabao nane

Katika michezo sita iliyochezwa kwenye mechi za ufunguzi, ni mabao sita pekee ndiyo yaliyowekwa kimiyani.

Katika michezo hiyo, Simba wameonekana kung’ara kutokana na kufunga idadi kubwa ya mabao 3 kuliko timu nyingine.

Mabao ya Simba yalifungwa na Ludit Mavugu (dk 19), Frederick Blagnon (dk 73) na Shiza Kichuya(dk 79), wakati bao pekee la Ndanda likitupiwa na Omary Mponda (36).

Kwa upande wa Africans Lyon waliocheza na Azam FC, bao lao lilifungwa na Mayanja Abdul (46), huku lile la kusawazisha la Wanalambalamba likitiwa kimiyani na Bocco ( dk 93).

Nao Tanzania Prisons waliokuwa wakicheza na Majimaji, waliweza kutoka kifua mbele kwa ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Sabiyanka (dk 8) na kuwa bao la kwanza kabisa katika michuano hiyo ya ligi kuu.

Huku Ruvu Shooting wakiwatungua Mtibwa Sugar 1-0 lililoingizwa nyavuni na Shabani Kisiga (dk 18), wakati Stand United na Mbao FC wakitoka suluhu.

Rekodi ya Atupele yashindwa kuvunjwa

Rekodi aliyoiweka mshambuliji wa zamani wa Ndanda FC, Atupele Green ya kufunga bao la mapema katika mechi ya ufunguzi wa ligi, imeshindwa kuvunjwa kwenye mechi sita zilizochezwa Jumamosi.

Msimu uliopita, Atulepe aliweza kufunga bao la mapema kwenye dakika ya 2 ya mchezo, wakati msimu huu mchezaji wa Prisons, Lambarti Sabiyanka, ambaye ndiye aliyefunga bao la mapema kwenye dakika ya nane, huku wafungaji wengine wakianza kuziona nyavu kuanzia dakika ya 10 na kuendelea.

Bocco ni  mchezaji wa pekee kufunga bao katika dakika za mwisho kwenye michuano hiyo ya ufunguzi ambapo alifunga katika dakika ya 93.

Timu ambazo zilipewa nafasi

Katika michezo hiyo ya awali, kuna timu ambazo mashabiki walizipa nafasi kubwa ya kufanya vizuri, zipo ambazo zilifanya hivyo, lakini zingine zilifanya tofauti na vile ambavyo wengi walidhani.

Simba SC, hii ni klabu ambayo imeonekana kufanya usajili wa nguvu kwa ajili ya kupambana na wapinzani wao na ikiwezekana kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu, hivyo katika mchezo wao dhidi ya Ndanda FC (Kuchele), wengi waliipa nafasi Simba ya kuweza kuibuka na ushindi na ndivyo ilivyotokea katika mchezo huo.

Stand United, hii nayo ilipewa nafasi ya kufanya vizuri katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Mbao FC ambayo imeanza ligi kuu msimu huu kwa mara ya kwanza baada ya kupanda daraja, lakini hali ilikuwa tofauti kwa Stand United ambao walikuwa nyumbani na kujikuta wakitoka suluhu.

Mtibwa Suger, japokuwa walikuwa kwenye uwanja wa nyumbani Manungu, lakini walichezea kichapo cha bao 1-0 dhidi ya wapinzani wao Ruvu Shooting, Mtibwa walipewa nafasi kubwa ya kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani, lakini hali ilikuwa kinyume na matarajio ya wengi.

Azam FC, walikuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani ambao wanautumia kwa mazoezi ya kila siku, lakini walishindwa kuonesha ubora wao pamoja na nyota wao wapya waliosajiliwa msimu huu, walijikuta wakilazimshwa sare ya 1-1 dhidi ya African Lyon, tena Azam wakipata bao la kusawazisha katika dakika ya lala salama.

Majimaji, mara nyingi timu ambayo inakuwa kwenye uwanja wa nyumbani, inapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri, hivyo Maji Maji walipewa nafasi ya kufanya vizuri kwa kuwa walikuwa nyumbani, lakini walishindwa na kujikuta wakipokea kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons.

Mwitikio wa mashabiki

Viwanja karibu vyote vilionekana kuwa na idadi kubwa ya mashabiki kwa lengo ya kuja kuziona timu zao kwa mara ya kwanza, hali hiyo inaweza kuendelea kama timu hizo zitakuwa zinafanya vizuri katika michezo mingine, lakini kinyume na hapo idadi inaweza kupungua taratibu.

Matukio

Timu ya Majimaji ilikuwa katika wakati mgumu kwa siku hiyo ya mchezo wao wa kwanza, kwa kuwa ilikuwa katika mazishi ya mchezaji wao wa zamani wa timu hiyo, Kelvin Haule, ambaye alifariki siku ya Ijumaa ya wiki iliyopita, hivyo walishuka dimbani huku wakiwa na huzuni wa kumpoteza mchezaji huyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here