Na Hamisa Maganga, Morogoro
TAKWIMU zinaonyesha wanawake waliopo nje ya ndoa wanaongoza kwa matumizi ya dawa za uzazi wa mpango kuliko wale walio kwenye ndoa.
Takwimu hizo zilitolewa juzi mkoani Morogoro katika semina ya waandishi wa habari kuhusu masuala ya idadi ya watu, afya na uzazi wa mpango, iliyodhaminiwa na Asasi isiyo ya kiserikali ya Pathfinder.
Mshauri wa masuala ya uzazi kutoka Hospitali ya Marie Stopes, Dk. Dismas Damian, alisema matumizi ya dawa za uzazi wa mpango kwa wanawake waliopo ndani ya ndoa ni asilimia 32 wakati wale wasioolewa ni asilimia 54.
Dk. Damian alitaja sababu za wanawake wengi walioolewa kutotumia dawa hizo kuwa ni vikwazo kutoka kwa waume zao.
“Wanaume wengi huwa hawapendi wake zao watumie njia za uzazi wa mpango hivyo hawawapi ushirikiano katika suala hilo.
“Wale waliopo nje ya ndoa huwa wanajiamulia wenyewe ni lini wapate watoto au wasizae kabisa, tofauti na ndani ya ndoa ambako mwanamume ndiye anaamua, hivyo wanawake hujikuta wakizaa bila mpangilio,” alisema Dk. Damian.
Akizungumzia suala la dawa inayopendwa na kinamama katika kupanga uzazi, alisema sindano inaoongoza ikilinganishwa na dawa nyingine.
Wanawake wengi huona rahisi kuchoma sindano kuliko kutumia dawa ya vidonge, kijiti au kitanzi, alisema.
Alisema sindano ina uwezo wa kuzuia mimba kwa asilimia 99 na kati ya wanawake 100 wanaotumia njia hiyo, mmoja tu ndiye anayeweza kubeba mimba wakati akiwa amechoma.
“Dawa hii haina madhara bali inaweza kugandisha damu kama ilivyo kwa dawa nyingine za kuzuia mimba au kwa wajawazito,” alisema.
Hata hivyo, Dk. Damian aliwashauri wanaume kutoa ushirikiano kwa wake zao katika kupanga uzazi kwa vile licha ya kuzaa bila mpangilio kudhoofisha afya ya mzazi, pia huchangia kuyumba kwa uchumi wa familia.