ISTANBUL, UTURUKI
SERIKALI ya Uturuki imetishia kuwafungulia milango wahamiaji haramu kumiminika katika Umoja wa Ulaya (EU), iwapo haitapatiwa kibali cha hati huru za kusafiria kwa ajili ya raia wake.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu, wakati wa mahojiano na Gazeti la Bild la Ujerumani jana.
Alipoulizwa iwapo mamia ya wakimbizi nchini Uturuki wataruhusiwa kuingia Ulaya endapo Umoja huo utashindwa kuipatia nchi hiyo pasi huru za kusafiria kuanzia Oktoba mwaka huu, Cavusoglu alisema, “ndiyo, tutajiweka kando katika mpango huu wa ukimbizi,” alisema.
Hata hivyo, alisema asingependa kuzungumzia mazingira hayo mabaya, akiongeza kuwa mazungumzo na EU bado yanaendelea, lakini ni wazi mikataba yote itumike au iwekwe kando.
Ruhusa ya kuingia EU bila ya viza ni moja ya makubaliano katika ushirikiano na Uturuki wa kupunguza wahamiaji barani Ulaya.
Lakini imekuwa ni ajenda inayocheleweshwa kufuatia kile kinachosemekana sheria ya Uturuki ya kupambana na ugaidi pamoja na kamata kamata ya baada ya kushindwa kwa mapinduzi.