23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 27, 2023

Contact us: [email protected]

Yanga pwaaa

IMG_2768

WINFRIDA NGONYANI NA ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

YANGA pwaaa, ndiyo kauli rahisi unayoweza kuitumia kuelezea anguko ambalo miamba hiyo ya Jangwani inaweza kukutana nalo baada ya jana kiongozi na bilionea wa klabu hiyo kutangaza kujiuzulu.

Uamuzi wa bilionea huyo kujiuzulu wadhifa wake umekuja siku moja baada ya Yanga kutolewa rasmi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kufuatia klabu ya Medeama SC kuifunga TP Mazembe kwa mabao 3-2.

Bilionea huyo amejiuzulu katika kipindi ambacho Yanga ilikuwa kwenye mchakato wa kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa klabu kutoka ule wa wanachama hadi mfumo wa kukodisha nembo ya klabu kwa miaka 10.

Kwa mujibu wa habari za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo zilizolifikia MTANZANIA jana, uamuzi wa kiongozi huyo kujiondoa Yanga unatajwa kuchangiwa na shutuma zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa Serikali waliokuwa wanapinga uamuzi wa kukodisha timu.

Inadaiwa kuwa kiongozi huyo amechoshwa na matusi na kebehi ambazo zimekuwa zikitolewa dhidi yake tangu mchakato wa kuikodisha nembo ya timu kwa miaka 10 ulipopitishwa wiki chache zilizopita.

Inasemekana kitendo cha bilionea huyo kujiuzulu wadhifa wake kilizua taharuki ndani ya klabu hiyo ya Jangwani na viongozi kadhaa wa juu wa Yanga walionekana kupigana vikumbo kwenye ofisi ya tajiri huyo.

Kujiuzulu kwa bilionea huyo kunadaiwa kuichanganya miamba hiyo ya Jangwani hasa katika kipindi hiki ambacho watani wao wa jadi, Simba wamepitisha maazimio ya kumpa timu bilionea, Mohamed Dewji ‘Mo’.

Inadaiwa kuwa kiongozi huyo ameonekana kuchoshwa na tabia za baadhi ya watu ambao wamekuwa wakimkebehi kwa hatua yake ya kuichukua timu ya Yanga na sasa ameamua kukaa pembeni kulinda heshima yake.

Awali, kumekuwa na taarifa kuwa kiongozi huyo ameamua kujitoa kwa kuwa kuna juhudi za chini pia zinazohusisha hadi watu wengine wenye mamlaka katika soka ambao wana hofu na uwekezaji wake.

Uamuzi wa kiongozi huyo ambaye pia ni mfadhili wa Yanga, unakuja siku chache baada ya Katibu wa Baraza la Wazee wa klabu hiyo, Ibrahim Akilimali, kudaiwa kupinga uamuzi wa kukodisha timu kwa kudai kuwa ulikuwa wa kukurupuka kwa kuwa haukufuata utaratibu.

“Uamuzi huu wa kukodisha timu ni wa kukurupuka kwa sababu kuna mambo mengi ya kujadili ya kisheria ambayo yana masilahi na klabu.

“Mwaka 2006 klabu hii iliingia mikataba ya kisheria juu ya uamuzi wake wa kuwa kampuni na jambo halo halijawahi kuzungumzwa tangu wakati huo, sasa inakuwaje kuja na uamuzi mwingine wakati huu bado haujamalizika.

“Hili si jambo la mchezo mchezo kwa mtu kuja na hoja zake na kuamua kama anavyopenda na ikizingatiwa anayependekeza mabadiliko haya ni kiongozi hivyo ni muhimu kufanya mjadala wakina na mkubwa juu ya jambo hili,” alisema Akilimali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,729FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles