25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Watoto wazaliwa wameungana

Pg 1 watoto

 

Na Shomari Binda, Musoma
MKAZI wa Kata ya Buhare Manispaa ya Musoma, Helena Paulo (21), amejifungua watoto pacha walioungana sehemu za kifuani na tumboni katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara.
Kutokana na taarifa za kuzaliwa kwa watoto hao kusambaa mitaani, wananchi wengi walimiminika hospitalini hapo kushuhudia.
Watoto hao, walizaliwa Januari 4, mwaka huu saa moja asubuhi.
Hili ni tukio la pili, baada ya lile lililotokea Agosti 6, mwaka jana.
Katika tukio hilo, mkazi wa Katoro wilayani Geita, Neema Luswetura (24), alijifungua watoto pacha wakiwa wameungana sehemu ya kifua na tumbo wakiwa na uzito wa kilo 5.1, lakini walifariki dunia muda mfupi baadaye.
Akielezea hali ya pacha hao, mkunga wa zamu aliyemzalisha mwanamke huyo, Elisifa Makala, alisema walimpokea mjamzito Helena Januari 3, mwaka huu saa 6 mchana akiwa mwenye uchungu wa kawaida.
Alisema walimpumzisha ili kusubiria kujifungua kutokana na kutokuwa na shida yoyote.
Makala alisema ilipofika saa 8 usiku, mwanamke huyo alianza kupata dalili za uchungu ambapo alipewa msaada wa kujifungua na wauguzi, lakini alishindwa kujifungua kwa njia ya kawaida kutokana na mtoto kutanguliza miguu.
Alisema kutokana na hali hiyo, waliamua kumfanyia upasuaji ambapo waliwakuta watoto hao wakiwa wameshikana.
“Kwa vile tuliona ni uzazi wake wa pili, tulimpa uangalizi maalumu mzazi huyo, baada ya kufika hospitalini na kumpima tulibaini atajifungua pacha. Hatukuwa tukijua kama ni pacha wa aina hii,” alisema.
Akizungumzia pacha hao, mtaalamu wa Idara ya Magonjwa ya Kinamama, Dk. Simon Kamuli, alisema watoto hao watahamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza kwa uchunguzi zaidi.
“Hapa kwetu Mara hatuna uwezo wa kufanya chochote kwa watoto hawa, tunaona njia pekee ni kuwapeleka kwa wenzetu pale Bugando ambako kuna madaktari bingwa,” alisema.
Alisema watoto hao wenye jinsi ya kike, kwa pamoja wamezaliwa wakiwa na uzito wa kilo 4.8 na wanapumua vizuri.
Kwa upande wake, mzazi wa watoto hao Helena, licha ya kumshukuru Mungu, alisema hakuwa na tatizo lolote wakati wa ujauzito wake na kwamba alikuwa hatarajii kujifungua pacha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles