Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), imeanza uchunguzi dhidi ya Kampuni ya Simon Group.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Rais Dk. John Magufuli, kuviagiza vyombo vya dola kuzirejesha mali za Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU LTD) kikiwemo Kiwanda cha New Era kilichouzwa kwa Kampuni ya Simon Group na kurejeshwa NCU.
Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Takukuru, Mussa Misalaba, alisema tayari taasisi hiyo imeanza uchunguzi dhidi ya Kampuni ya Simon Group ambayo inamilikiwa na mfanyabishara, Robert Kisena.
Pamoja na hali hiyo Misalaba alisema, kinachofanyika sasa ni kuainisha mambo muhimu ikiwemo kuongeza maeneo ya uchunguzi dhidi ya mfanyabishara huyo ambaye pia anaendesha Shirika la Usafiri jijini Dar es Salaam (UDA).
“Kuna mambo muhimu ambayo yameainishwa katika uchunguzi wetu yanamhusu Robert Kisena ambayo yanahitaji muda zaidi ya kuyafanyia kazi ili tuweze kujiridhisha kabla ya kumfikisha kwenye mikono mingine ya sheria,”alisema Misalaba.
Msemaji huyo wa Takukuru, alisema suala la uchunguzi ni hatua ndefu, hivyo basi lazima wahakikishe kuwa mambo yaliyokusudiwa yanakamilika kabla ya kulifikisha katika vyombo vingine ikiwemo mahakamani.
Kampuni ya Simon Group chini ya Mwenyekiti wake Mtendaji, Robert Kisena ndiyo walipewa tenda ya kuendesha Shirika la Usafiri katika Jiji la Dar es Salaam (UDA), ambapo suala hilo hadi sasa bado giza nene limetanda.
Mazonge kwa Simon Group
Pamoja na Rais Magufuli, kutoa agizo la kuhakikisha watu waliopora mali za Chama cha Ushirika cha Nyanza (NCU), wanapatikana na kuzirudisha mali hizo mara moja, huku akiitaja Kampuni ya Simon Group yenye umiliki katika kampuni za UDA na Mabasi ya Haraka Dar es Salaam (UDA-RT), bado kampuni hiyo imekuwa ikiandamwa na matukio mbalimbali yenye utata.
Akiwa jijini Mwanza Rais Magufuli alisema mfanyabiashara Robert Kisena, ambaye ndiye mmiliki wa Kampuni ya Simon Group, alipewa Kiwanda cha New Era kwa Sh bilioni moja lakini fedha aliyolipa ni Sh milioni 32 tu.
Simon Group ni kampuni iliyozaliwa na kampuni ya Simon Agency iliyoanzishwa mkoani Shinyanga na Robert Kisena, kushughulika na ununuzi na uchambuaji wa pamba karibu miaka minane iliyopita.
Hata hivyo kampuni hiyo imekuwa na historia ya kuingia kwenye migogoro mikubwa ya kibiashara na vyama vikuu vya ushirika katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Vyama ilivyoingia navyo kwenye migogoro ni pamoja na Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Mwanza (NCU) na Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU), ambavyo vinaidai mamilioni ya fedha dhidi ya Kisena kwa madai ya kukiuka mikataba mbalimbali, ikiwamo ya kukodi vinu vya kuchambulia pamba na ununuzi wa rasilimali.
Mkataba wa DART
Licha ya mfanyabishara huyo kuendelea kuaminiwa na hata kudaiwa kukingiwa kifua na baadhi ya vigogo, Serikali bado ilimfuatilia na kunusa harufu ya ufisadi katika mkataba unaoihusisha Kampuni ya Simon Group na Mradi wa Mabasi ya Mwendo wa Haraka (DART).
Aprili 19, mwaka huu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene, ameeleza namna mchezo mchafu ulivyotawala katika zabuni ya mradi huo.
Kwa mujibu wa Simbachawene, zabuni iliyotangazwa ilipaswa iwe katika mfumo wa kimataifa, lakini katika hali ya kushangaza Kampuni ya Simon Group ilianza maandalizi ya kuendesha mradi huo kinyume cha utaratibu.
Simbachawene, alisema Serikali ililazimika kuingilia kati suala hilo kwa lengo la kujiridhisha kuhusu zabuni hiyo.
Alisema katika hatua hiyo, Serikali ilibaini utata katika mkataba wa kampuni hiyo, kwani kila kitu kilikuwa chini ya Simon Group ambao ni wamiliki wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).
“DART katika kumpata mwekezaji ilitangaza tenda kutokana na maoni mbalimbali ambapo ilitakiwa kutangaza kimataifa (International tender), lakini ikafanya tofauti na maoni ya watu na kuipa Kampuni ya Simon Group kuendesha mradi huo.
“Kampuni ya Simon Group iliendelea kufanya maandalizi kwa ajili ya mradi na sisi tukaendelea kufuatalia uhalali wa mikataba waliongia na DART ili kuona ni jinsi gani huu mradi uanze lakini tulichokikuta pale kila kitu kipo chini ya Kampuni ya Simon Group kwa kuwa wao ndiyo wamiliki wa Shirika la UDA na wamenunua hisa zote za shirika hilo.
“…ndipo tulipo ulizia zile hisa ambazo haziuzwi bila wana hisa sambamba na kutaka kujua kama fedha zimeshalipwa ndipo napo tukagundua hakujalipwa hata senti tano na haijulikani ni nani kapokea zile hela,” alisema Simbachawene.
Sakata la umiliki wa Shirika la Usafirishaji jijini Dar es Salaam (UDA) ambalo limekuwa likitoa huduma za usafiri katika maeneo tofauti ya Jiji la Dar es Salaam limechukua sura mpya baada ya kuzungumziwa ndani ya Bunge huku Serikali ikishindwa kueleza sababu za shirika hilo kuendeshwa na mtu binafsi.
Hata hivyo wingu dhidi ya Kampuni ya Simon Group, lilikuwa likichukua sura mpya kila kukicha na kuibukia katika Bunge la 10 ambapo wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam walihoji uhalali wa uuzwaji wake.