33.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Michezo inapaswa kuanzia shuleni

picNa Dk. Fredirick Mashili, MD, PhD

ILI kudumisha afya bora na kujikinga na magonjwa sugu, inashauriwa watoto na vijana wenye umri kati ya mika mitano  hadi 17, kufanya mazoezi yanayotumia nguvu ya wastani mpaka nguvu kubwa kwa muda usiopungua saa moja au zaidi kila siku. Mazoezi haya ni pamoja na shughuli za kila siku kama vile kufanya usafi, kusafiri kwa kutumia baiskeli au kutembea, mazoezi maalumu na michezo ya aina mbalimbali kama vile mpira wa miguu.

Mazoezi mazuri kwa kundi la watoto na vijana hawa, ni yale yanayojumuisha mazoezi ya aerobics kama vile kukimbia na ya nguvu ‘resistance exercise,’ kama vile kunyanyua au kusukuma vitu vizito. Mazoezi kama kucheza mpira, kuruka kamba, kuendesha baiskeli na mbio za kasi (sprinting) ni mazoezi mazuri kwa sababu hujumuisha mazoezi ya kasi na mazoezi ya nguvu, hivyo kuufanya moyo kufanya kazi vizuri wakati huo huo yakisaidia kukakamaza misuli na kuipa mifupa nguvu.

Asilimia kubwa ya muda wa mchana kwa watoto walio katika kundi hili, humalizikia shuleni. Kwa sababu za kimazingira ni asilimia ndogo sana ya wanafunzi waishio katika jiji kama la Dar es Salaam, hutumia usafiri wa baiskeli au hutembea kwa miguu kwenda shuleni. Suala hili la kimazingira huondoa fursa ya kufanya mazoezi wakati wa kusafiri kwenda na kutoka shuleni. Kwa maana hiyo basi, sehemu pekee ambayo mwanafunzi huyu anaweza kupata fursa ya kufanya mazoezi ni pale anapokuwa shuleni.

Tafiti zinaonyesha kwamba, mazoezi husaidia kudumisha afya bora kwa kuifanya mifupa na misuli kuwa yenye nguvu, kuzuia unene uliokithiri na magonjwa sugu kama vile kisukari, matatizo ya moyo na baadhi ya saratani. Tafiti zinaonyesha pia kwamba, suala la kupunja muda wa mazoezi na michezo na kuuongezea katika masomo limeshamiri katika shule nyingi duniani.

Wakati wanaopunja muda wa mazoezi wakifanya hivyo kwa kudhani kwamba wanampa mwanafunzi muda mwingi zaidi kusoma, tafiti nyingi nchini Marekani zinaonyesha kwamba sambamba na tabia hii ya kupunguza muda wa mazoezi na michezo shuleni kuongezeka, kumekuwa na ongezeko kubwa la matatizo ya unene uliokithiri kwa watoto na vijana, hivyo kuchangia kuongezeka kwa ugonjwa wa kisukari aina ya pili katika kundi hili.

Ujumbe huu unatukumbusha kwamba, mazoezi na michezo ni muhimu shuleni. Ni vema kwa shule zote za msingi na sekondari kuzingatia vipindi vya mazoezi na michezo. Ni muhimu pia kwa wizara husika kuhakikisha shule zinakuwa na mitaala na mazingira rafiki yanayosaidia kuhamasisha kufanya mazoezi na kushiriki katika  michezo. Wakati huohuo, tufikirie kutengeneza na kudumisha mazingira ambayo siku moja yatawawezesha watoto  kuendesha baiskeli na kutembea, kwenda na kurudi kutoka shuleni.

Kama mzazi, mwalimu, mtunga sera au mwanaharakati, unasema nini kuhusu suala la mazoezi shuleni? Je, unadhani watoto wetu wanatimiza kiwango cha mazoezi yanayotakiwa kiafya? Unadhani mazingira na mitaala vina mchango wowote katika hili? Nini mawazo yako kuhusu kinachotakiwa kufanyika ili kuhakikisha watoto wanafanya mazoezi na kushiriki michezo ipasavyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles