22.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi watumie muda wa ziada kujifunza ujasiriamali – Sia

Sia MinjaNa Veronica Romwald, Dar es Salaam

DUNIA inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ajira, tunaona katika mataifa mengi Tanzania ikiwamo ambapo idadi kubwa ya vijana imekuwa ikizalishwa vyuoni lakini wanamaliza huku kukiwa hakuna fursa za ajira.

Viongozi mbalimbali wa dini na kisiasa wamekuwa wakitoa ushauri kwa vijana kuwa wasisubiri kuajiriwa bali wajiajiri wenyewe, hata hivyo wengi wao wanakuwa hawajui wajiajiri kufanya nini.

Hii ni kwa sababu mfumo wetu wa elimu umekuwa hauzalishi vijana wenye ujuzi wa kuwawezesha kwenda kujiajiri pindi wanapomaliza masomo yao ili waweze kuzalisha fedha zitakazowasaidia kuyaendesha maisha yao na wale wanaowategemea kwenye familia zao.

Hali hii imesababisha vijana wengi kukata tamaa ya maisha na kujikuta wakishawishiwa kujiingiza kwenye vitendo hatarishi.

Tumeona wengi wao wakijiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya, ukahaba na hata ujambazi.

Hata hivyo si wote, wapo ambao hujitambua, kujikubali na kuamua kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa kufanya biashara ndogondogo.

Sia Minja mwanafunzi wa kidato cha tano katika shule ya Sekondari Jangwani, anasema ni vyema wanafunzi wakajengewa utamaduni wa kuanza kujifunza shughuli mbalimbali za kiuchumi tangu wakiwa shuleni.

“Kweli ni changamoto kubwa kuona watu wanamaliza lakini hakuna ajira, mwisho wanaingia kwenye vitendo viovu. Wakati umefika wa kubadilika kuanzia kwa mwanafunzi mwenyewe, lazima atenge muda kujifunza vitu vya ziada hasa ujasiriamali.

“Binafsi tangu nikiwa mtoto nimekuwa na ndoto ya kuwa mhasibu siku moja katika maisha yangu Mungu atakaponijalia.

“Lakini pamoja na ndoto hiyo ya kuwa mhasibu natarajia kuwa mjasiriamali mkubwa katika siku za usoni hapa nchini,” anasema.

Sia anasema ili kufanikisha jambo hilo tayari ameanza kujifunza namna ya kutengeneza bidhaa mbalimbali ili kujijengea uwezo.

“Mama yangu ni mjasiriamali ndio maana imekuwa rahisi kwangu kujifunza ninapokuwa nipo nyumbani, kama unavyojua shule nyingi hazifundishi mambo haya,” anasema.

Anasema hivi sasa anajua kutengeneza sabuni, batiki pamoja na dawa ya kuoshea nywele (shampoo).

“Unaweza kuona ni vitu vidogo lakini vina umuhimu mkubwa katika maisha ya kila siku ya binadamu na vina uhakika wa soko.

“Ni vyema jamii ikasaidia vijana, yule aliye na ujuzi ampe na mwingine ili tuweze kusaidia kukuza uchumi wa Taifa letu,” anasema.

Anaiomba serikali kuhakikisha kuhakikisha kuwa somo la ujasiriamali linaingizwa kwenye mtalaa wa elimu nchini ili iwe lazima mwanafunzi kupata ujuzi tangu wakiwa shuleni.

Anaiomba pia kuwatambua na kuwawezesha wajasirimali kupata fursa ya mikopo na kuwatengea maeneo ya kufanyia biashara zao pamoja na kuwatafutia masoko ya ndani na nje ya nchi.

“Lakini pamoja na hayo yote nawashauri wanafunzi wenzangu kuwa makini na kuwekeza nguvu zao katika kusikiliza na kujifunza yale wanayofundishwa darasani,” anasema.

Anasema watumie vizuri fursa iliyopo sasa ya mitandao mbalimbali ya kijamii kwa kujifunza mambo yenye tija na kuachana na yale yasiyofaa.

“Mambo yamekuwa rahisi siku hizi hata kama huna kitabu unaweza kufungua mada tofauti tofauti kupitia mitandao na ukasoma kama kawaida, siku hizi kuna magroup ya Whatsapp wayatumie kujifunza na si kuishia kuchati peke yake.

“Elimu ni ufunguo wa maisha yao, wawekeze muda wao katika kutafuta maarifa yatakayowasaidia baadae, wasikate tamaa na kuishia kujiunga na makundi yasiyofaa,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles