MWILI wa aliyekuwa Mpigapicha Mkuu wa Gazeti la Tanzania Daima, Joseph Senga, jana ulipumzishwa katika makazi yake ya milele wilayani Kwimba mkoani Mwanza.
Senga (58) aliyefariki dunia Julai 27 mwaka huu nchini India, alizikwa nyumbani kwao katika Kijiji cha Shushi wilayani Kwimba.
Maziko hayo yaliongozwa na Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye pia mwenyekiti wa Chadema. Pia alikuwapo Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji na mamia ya waombolezaji.
Akizungumza katika maziko hayo, Mbowe alimuelezea Senga kuwa ni shujaa wa mapambano ya kupigania haki na demokrasia ya kweli nchini.
Alisema kazi za Senga aliyoiacha hapa duniani ni kielelezo thabiti cha uwajibikaji usioogopa vitisho.
“Senga alikuwa mfanyakazi na mtumishi mwenzetu. Senga hakuwa baraka kwa wana Kwimba pekee, bali alikuwa mtu wa wote. Nimefanya kazi naye kwa zaidi ya miaka 16. Tumezunguka naye kila eneo ndani ya nchi hii. Hakuna operesheni ya Chadema tuliyomuacha Senga,” alisema Mbowe.
Vilevile, alisimulia mazingira tatanishi yaliyosababisha kifo cha aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Channel Ten mkoani Iringa, Daud Mwangosi.
Mbowe aliyetumia dakika 20 kumzungumzia marehemu Senga, alisema usingekuwa ujasiri wake kupiga picha za tukio la kifo cha Mwangosi, dunia isingefahamu polisi ndiyo waliohusika na mauaji hayo.
Senga ameacha mke mmoja na watoto saba, kati yao wanne wa kike na watatu wa kiume.
Mungu ailaze mahala pema peponi, roho ya marehemu, Joseph Senga.