23.7 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

Lema, Gambo wasutana mbele ya naibu waziri

Mrisho GamboNa JANETH MUSHI, ARUSHA

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mrisho Gambo, wamechongeana kwa Naibu Waziri wa TAMISEMI, Seleman Jafo.

Lema na Gambo walichongeana jana mjini hapa wakiwa kwenye kikao cha watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kilichojumuisha wakuu wa idara, maofisa tarafa na waratibu wa elimu kata.

Aliyekuwa wa kwanza kuwasilisha malalamiko yake kwa Jafo ni Lema kwa kusema Gambo amekuwa akiingilia uamuzi unaopitishwa na baraza la madiwani la halmashauri hiyo lenye diwani mmoja wa CCM.

Lema alisema kwamba, tangu kiongozi huyo awasili ofisini kwake, amekuwa akiingilia zaidi majukumu yao ya kiutendaji na kusababisha kuwapo kwa mwingiliano wa majukumu ya kazi kati ya baraza la madiwani na mkuu huyo wa wilaya.

Akitoa mfano, Lema alisema Kamati ya Mipango Miji ilikuwa imeandaa ziara ya kikazi, lakini katika hali ya kushangaza, Gambo alimwagiza Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athuman Kihamia, aisitishe.

“Hivi sasa Gambo amekuwa akiagiza kubatilishwa kwa baadhi ya mambo yanayoamriwa na baraza la madiwani. Hivi karibuni ameagiza eti Takukuru wafanye uchunguzi wa baadhi ya mambo ikiwamo posho za madiwani,”alisema Lema.

Akijibu tuhuma hizo, Gambo alisema yeye ndiye rais wa wilaya hiyo kwa sababu anafanya kazi kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli.

“Kwenye suala la maendeleo hakuna siasa, mbunge atambue huduma za wananchi hazisubiri maamuzi ya baraza la madiwani kwani haiwezekani kila kamati kutembelea mradi mmoja wa elimu, afya au miradi mingine.

“Mimi ndio rais wa wilaya, ninafanya kazi bila kukurupuka wanaposema nawaingilia kwenye kazi unataka nifanyaje. Wananchi wana kero za barabara. Kuwaambia wananchi nitawapatia mafuta ya greda ili barabara itengenezwe hilo ni tatizo kwako? alihoji Gambo

Baada ya mvutano huo, Jafo alimwagiza Katibu Tawala, Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega, kuchukua malalamiko yanayohusiana na mwingiliano huo na kuyafanyia kazi kwa kuwa kila kiongozi anatakiwa kufanya kazi kwa niaba ya wananchi.

Katika mkutano huo, Jafo aliwataka wakuu wa idara na wafanyakazi wote, wafanye kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,745FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles