Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
KABLA hujafa hujaumbika ni msemo madhubuti ambao katika makala haya ya Mwanafunzi Shupavu sina budi kuanza nao.
Katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) nimekutana na Johari Salehe (10) mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Sai iliyoko Chanika jijini hapa.
Mama wa binti huyo anasema Johari alizaliwa bila tatizo lolote lakini wakati wa ukuaji wake alipatwa na tatizo la kuwa na kichwa kikubwa.
Anasema iligundulika hivyo baada ya madaktari kumfanyia uchunguzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Johari anasema kuwa na ulemavu huo kamwe hakuwezi kumkatisha tamaa ya kufikia ndoto zake katika maisha yake atakayojaliwa kuishi hapa duniani.
“Kwanza namshukuru Mungu kwa kuniumba hivi nilivyo, hata siku moja sitajidharau na najiona kuwa sawa na watoto wengine ambao hawana ulemavu wowote.
“Lakini pia namshukuru mama yangu kwa sababu hakunitupa na alijitahidi kwa hali na mali kunihudumia na kunifikisha hapa hospitalini ili nipatiwe huduma, sijui leo ningekuwa wapi,” anasema.
Johari anawashukuru madaktari wote waliomuhudumia na kufikia hatua ambayo anayo sasa ambapo anaweza kusimama na kufanya kila jambo linaloweza kufanywa na mwanadamu mwingine asiyekuwa na ulemavu,
“Huwa kila ninapozungumza juu ya hali yangu lazima nimshukuru Mungu, mama yangu na madaktari wangu kwa sababu walikuwa msaada mkubwa kwangu katika kipindi chote.
“Huwa namsikia mama akisema kama si madaktari kunisaidia basi leo nisingeweza hata kusimama na kutembea au kufanya shughuli yoyote ile, kwa sababu katika hatua za awali za ugonjwa nilikuwa siwezi kufanya mambo hayo.
“Na kwa sababu hiyo huwa najisikia kuwa nina deni kubwa ndani ya moyo wangu, kwamba siku moja nije nisaidie watu wengi zaidi kama nilivyosaidiwa mimi,” anasema.
Mtoto huyo anasema anatamani aje kuwa daktari bingwa wa magonjwa mbalimbali hasa yale ambayo yamekuwa yakiwasumbua watoto.
“Watoto wengi wanateseka kwa kuumwa maradhi mbalimbali, natamani niwe daktari wa magonjwa ya watoto ili nisaidie kuokoa maisha yao na naomba Mungu anisaidie nitimize ndoto yangu hiyo,” anasema.
Anasema alimjulisha mama yake juu ya ndoto yake hiyo pamoja na daktari wake ambao wamemtia moyo kuwa hilo linawezekana na kwamba anapaswa kuongeza juhudi katika kujifunza kwa bidii.
“Nimeambiwa nijifunze kwa bidii masomo ya sayansi ili niweze kufikia malengo yangu, nitajifunza bila kuchoka masomo hayo pamoja na lile la hisabati,” anasema.
Johari anasema pia Mungu amemjalia kipaji cha uimbaji na kwamba atahakikisha anatunga mashahiri mbalimbali ya kuelimisha jamii.
“Kuna baadhi ya jamii ambazo bado zinaendeleza mila potofu za kukataa watoto wenye ulemavu na hata kuwatekeleza, nimetunga nyimbo za kuelimisha juu ya jambo hilo,” anasema.
Johari anasema pia atahakikisha anakuwa mfano bora kwa jamii inayomzunguka kwa kutenda matendo mema na kufanya vizuri zaidi darasani.
“Mwalimu wangu ameniambia kuwa yote yanawezekana hapa duniani kikubwa na cha muhimu ni kutia bidii katika kila jambo ili kuweza kufikia malengo, na ameahidi kunisaidia katika hilo na kaka zangu nyumbani ni msaada mkubwa kwangu,” anasema Johari.