25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Wauaji wa Ubungo wahukumiwa kunyongwa • Ni wale waliohusishwa na uporaji wa fedha za NMB

Jaji Mkuu Othman Chande
Jaji Mkuu Othman Chande

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam,
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa hukumu ya kunyongwa hadi kufa kwa washtakiwa sita katika kesi ya mauaji ya askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wa mkoani Morogoro na mfanyakazi wa Benki ya NMB, maarufu kama mauaji ya Ubungo Mataa.
Washtakiwa hao waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa jana na Jaji Projest Rugazia ni Haji Kiweru, Mashaka Pastory, Wycliff Imbora, John Mndasha, Martine Mndasha na Rashidi Abdikadir.
Jaji Rugazia alidai kwamba aliwatia hatiani washtakiwa hao na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa kutokana na ushahidi ulitolewa na mashahidi 29 upande wa mashtaka pamoja na vielelezo 78 vilivyowasilishwa mahakamani hapo na ushahidi wa utetezi.
“Maungamo ya washtakiwa, ushahidi wa kitaalam na utambuzi wa washtakiwa kutambiliwa eneo la tukio inaonesha wazi kwamba walikuwa na nia ya kujaribu kupora takribani Sh milioni 150 ambazo ni mali ya benki ya NMB zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro tawi la Wami,” Alidai Jaji Rugazia.
Alidai siku hiyo ya huzuni ya Aprili 20 mwaka 2006, majambazi hao walilivamia gari hilo kwa lengo la kupora lakini bila ya huruma yoyote walilimiminia risasi na kumwua askari huyo mwenye namba D 6866, Konstebo Abdallah Marwa na mfanyakazi wa NMB tawi la Wami Morogoro, Ernest Manyonyi.
Alidai washtakiwa walifanya tukio hilo katika eneo la Ubungo mataa jijini Dar es Salaam saa 6:30 mchana katika makutano ya barabara ya Morogoro na Sam Nujoma.
Hata hivyo Jaji Rugazia aliwaachia huru washtakiwa Rashid Lemblisi, Philipo Mushi, Yassin Juma,Hamisi Daud, MT 77754 Nazareth Amurike, MT 76162 Emmanuel Lameck, James Chamangwana na Hussein Idd baada ya kukutwa hawana hatia katika kesi hiyo.
Kwa upande wa washtakiwa, Jackson Issawangu aliyekuwa mshtakiwa wa sita katika kesi hiyo na Mussa Mustafa aliyekuwa mshtakiwa wa 10 waliachiwa huru awali baada ya mahakama hiyo kuwaona kuwa hawana kesi ya kujibu.
Hadi wanaachiwa huru hapo jana washtakiwa hao walikuwa wamekaa rumande kwa muda wa zaidi ya miaka 8.
Awali wakati kesi hiyo ilipokuwa ikisikilizwa, mahakama hiyo ilitupilia mbali vielelezo muhimu vya ushahidi katika kesi hiyo ya mauaji ikiwemo ripoti saba, kati ya nane za uchunguzi wa silaha zilizotumika katika mauaji hayo.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Godfrey Luhamba, Mtaalam wa milipuko kuiomba mahakama hiyo ipokee ripoti hizo kama vielelezo vya ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo.
Mawakili wa upande wa utetezi wakiongozwa na Richard Rweyongeza, walipinga ripoti hizo kupokewa, wakidai kuwa ziliwasilishwa kinyume cha sheria kwa kuwa hazikusomwa kwa washtakiwa wakati wa kuhamisha kesi hiyo kutoka Mahakama ya Kisutu kwenda Mahakama Kuu.
Katika uamuzi wake, Jaji Rugazia alikubaliana na utetezi kuwa kwa kuwa ripoti hizo hazikuwahi kusomwa kwa washtakiwa, basi mahakama hiyo haiwezi kuzipokea kwa sababu ziliwasilishwa kinyume cha sheria.
Pia alikataa hoja za upande wa mashtaka kutaka mahakama iamuru washtakiwa hao warudishwe tena mahakama ya chini (Kisutu), wakasomewe ripoti hizo, au iamuru upande wa mashtaka uwapatia upande wa utetezi wapate muda wa kuzipitia na kisha kuendelea.
Alidai mapendekezo hayo ya upande wa mashtaka hayaungwi mkono na kifungu chochote cha sheria.
Hata hivyo mahakama hiyo ilipokea ripoti moja tu ambayo ndio iliyosomwa kwa washtakiwa katika mahakama ya chini, ambayo inabainisha kuwa maganda mawili ya risasi, yaliyopatikana katika eneo ya tukio yalitoka kwenye bastola mojawapo zilizokamatwa kwa washtakiwa.
Ripoti nyingine zilizokataliwa ni zile zinazohusu bastola nane, SMG tano na Shortgun moja ambazo zote zilikamatwa kwa washtakiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles