27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Kilichobaki kwa Yanga ni kudra za Mungu

YANGA 234

NA ZAINAB IDDY,

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, Yanga, kesho watakuwa Tokoradi nchini Ghana kucheza dhidi ya Medeama.

Mchezo huo wa hatua ya makundi wa Kombe la Shirikisho Afrika ni  wamarudiano baina ya timu hizo, ambapo awali zilitoka sare ya bao 1-1 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.

Timu hizo za Kundi A, kila mmoja inahitaji matokeo ili aweze kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutinga hatua inayofuata, licha ya kupitwa na zaidi ya pointi tatu na wapinzani wao waliopo juu yao.

Yanga wao katika michezo mitatu waliocheza wamejinyakulia pointi moja huku wakishika mkia kwenye msimamo wa kundi lao wakati Medeama wakiwa na pointi mbili mbele ya Wanajangwani.

Kundi hilo linaongozwa na TP Mazembe ya Congo wenye pointi saba wakifuatiwa na Mo Bejaia ya Algeria wenye pointi tano kibindoni.

Wanajangwani walianza kutupa karata yao katika hatua ya makundi kwa mechi dhidi ya Mo Bejaia ugenini na kufungwa 1-0, kisha wakapokea kipigo hicho tena kutoka kwa Mazembe wakiwa nyumbani kabla ya kupata sare mbele ya wageni wao Medeama.

Kwa hesabu za haraka haraka unaweza kujifariji kuwa  Yanga itatinga  hatua ya nusu fainali, kwani mpira unadunda ndani ya uwanja dakika 90 na soka lina maajabu yake.

Kulingana na nafasi waliyopo Yanga katika hatua hiyo ya makundi, zinahitajika rehema za Mungu ili waweze kusonga mbele, kwani ili watinge hatua ya nusu fainali wanahitaji kushinda michezo yake yote iliyobaki.

Kama uliuangalia mchezo wao dhidi ya Mazembe na ule wa Medeama, ni wazi utakubali kuwa Wanajangwani hao wana wakati mgumu katika michezo yao ya marudiano hususani mbele ya timu hizo wakiwa ugenini.

Katika mchezo wa Medeama, iwapo kama Waghana hao wangetulia ni wazi wangeondoka katika uwanja wa taifa si chini ya mabao matatu, kwani kipindi cha pili walikosa mabao mengi ya wazi lakini papara za wachezaji wake walipokuwa eneo la hatari ndio ilikuwa tatizo kwa Wanajangwani.

Hali kama hiyo ilijitokeza pia kwa Mazembe, Yanga waliolala mbele kwa bao 1-0, hivyo ugumu unaonekana kwa Wanajangwani kutinga hatua ya nusu fainali.

Inakumbukwa kuwa kila timu imebakiwa na mechi tatu mkononi kama Yanga watafanikiwa kushinda yote watakuwa wameweza kutinga nusu fainali.

Yanga wanahitajika kuanza kuzisaka pointi 9 kwa Medeama kisha TP Mazembe na kumaliza nyumbani mbele ya Mo Bejaia  ili kutimiza jumla ya pointi 10.

Iwapo ikishinda michezo hiyo itakuwa nyuma ya Mazembe watakaokuwa na pointi 13 kama watashinda mechi mbili, huku Bejaia ikiwa na pointi sita na Medeama tatu.

Matokeo ambayo yatawawezesha kutinga hatua ya nusu fainali na hatimaye kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza na kuwashangaza wengi kama ilivyokuwa kwa Ureno ilivyofanya Euro.

Licha ya hesabu Yanga inajifariji lakini benchi la ufundi linakazi kubwa kuhakikisha wanarekebisha makosa yaliyojitokeza kwenye michezo iliyopita.

Yanga inahitajika kufanya marekebisho katika safu ya ushambuliaji iliyoonekana kupoteza nafasi ya kupata mabao ya wazi, mabeki  na safu ya ulinzi ambayo mechi ya Medeama Wanajangwani watamkosa Vicent Bossou anayetumikia adhabu ya kadi mbili za njano lakini kukiwa na nafasi kubwa nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akaingia kuziba nafasi hiyo baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kutokana na kukosa namba katika kikosi cha kocha Hans van de Pliujm.

Mbali na hao, Bossou, Wanajangwani pia itawakosa Godfrey Mwashiuya na Deusi Kaseke ambao ni majeruhi na wanahitajika kuwa nje kwa kipindi kirefu.

Ili kufikia malengo, wachezaji wanahitajika kujua na umuhimu wa kushinda mchezo huo na kutoruhusu wachezaji kutawaliwa na presha katika mioyo yao.

Inawapasa kufahamu kuwa Medeama si timu ya kubeza ikiwa nyumbani, ukizingatia tayari wanawafahamu wachezaji gani hatari kwa Yanga  jambo ambalo wasipokuwa makini wanaweza kujikuta wakitawaliwa katika dakika zote za mchezo.

Yote kwa yote dua na kumwachia Mungu ndiko kunahitajika kulingana na timu anazokwenda kucheza nazo ambazo mechi za kwanza zimewanyima pointi, lakini pia kazi inahitajika ili kufika mahali pazuri timu ya Yanga.

Endapo Yanga itashindwa kupenya katika mashindano hayo ya pili kwa ukubwa Barani Afrika, itakuwa ni mara ya pili kwani mwaka 1998 iliishia hatua hiyo katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles