Jafo atoa onyo kwa watumishi wa afya

Suleiman Jafo
Suleiman Jafo
Suleiman Jafo

NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Suleiman Jafo, ametoa onyo kwa watumishi wa afya kuacha tabia ya kuihujumu sekta hiyo.

Aliahidi kuwachukulia hatua kali watakaobainika kwenda kinyume cha maadili ya utumishi wa umma.

Waziri Jafo alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki wilayani Kisarawe, mkoani Pwani, wakati akipokea msaada wa mashuka yaliyotolewa na Mfuko wa Pensheni wa LAPF kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe.

Alisema anazo taarifa baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo wanatumia taaluma zao kuhujumu huduma za afya kwa wananchi, hivyo hatakuwa na msamaha kwa yeyote atakayebainika.

Waziri huyo alisema baadhi ya watumishi kwa dhamira yao mbaya wameamua kuomba uhamisho wa vituo ili kukomoa wananchi kwa lengo la kudidimiza huduma za afya.

Katika hotuba yake hiyo, Jafo alisema anashangaa hospitali hiyo imekuwa na rufaa nyingi, jambo ambalo anaona ni hujuma kwa baadhi ya wataalamu wa afya hivyo malalamiko ya wananchi ndani ya hospitali hiyo yanatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa kina.

“Wapo hapa baadhi ya wataalamu wa afya kwa makusudi wanakwamisha huduma za afya…haiwezekani kila kukicha rufaa zipo nyingi ndani ya hospitali hii wakati kuna wataalamu wa kutosha,” alisema Jafo.

Alisema kitendo cha kutoa rufaa nyingi kwa makusudi ni kuibebesha mzigo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Jafo alisema uzembe na hujuma hakubaliani navyo hivyo kama kuna kundi la watumishi wanapanga njama hizo wakae chonjo siku zao zinahesabiwa.

Alisema hospitali hiyo imekuwa ikisifiwa kwa kuwa na  wataalamu wa tezi dume na ung’oaji meno, jambo ambalo wanatakiwa kulizingatia ni utendaji kazi uliotukuka.

“Haiwezekani tukakaa kimya eti mtu kaja kung’oa jino mnamwambia ganzi hamna, wengine mnawang’oa, hujuma hii haikubaliki,” alisema.

Aidha, Waziri huyo aliwataka watumishi wa hospitali hiyo kudhibiti vifo vya watoto na wanawake.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa LAPF, James Mlowe, alisema eneo la afya lina umuhimu wa mkubwa, hivyo jamii inapaswa kulipa kipaumbele cha kutosha.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Dk. Elizabeth Oming’o, alisema wanakabiliwa na changamoto ya vifaa tiba, dawa na uhaba wa maji katika vituo na zahanati mbalimbali wilayani humo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here