24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Olimpiki ilivyopunguza msisimko wa Tour de France

Tour de France

NA BADI MCHOMOLO,

MATAIFA mbalimbali yanajiandaa na michuano ya Olimpiki ambayo inatarajia kuanza kutimua vumbi Agosti 5 mwaka huu na kumalizika Agosti 21.

Michuano hiyo inatarajia kufanyika mjini Rio de Janeiro, nchini Brazil, ambako tayari kuna baadhi ya mataifa yamewasili nchini humo kwa ajili ya kuanza kuzoea mazingira.

Katika Olimpiki, kuna michezo mbalimbali ambayo itaendelea kama vile soka, kikapu, ngumi, riadha, baiskeli, tenisi na mingine mingi.

Kwa sasa kuna michuano mikubwa ambayo inaendelea nchini Ufaransa, inajulikana kwa Tour de France, kwa ajili ya mashindano ya baiskeli.

Hii ni michuano ambayo imekuwa ikifuatiliwa tangu kumalizika kwa michuano ya Euro 2016 nchini Ufaransa na kuwafanya watu wa michezo wageukie kwenye baiskeli.

Wengi walianza kuitupia macho michuano hiyo kutokana na ushindani uliopo pamoja na vituko mbalimbali kama vile washindani kuanguka, kukimbia bila baiskeli na mambo mengine mengi.

Lakini hali ya msisimko ilianza kupotea mara baada ya nyota wa mchezo huo kutangaza kujitoa kwa madai kwamba wanakwenda kujiandaa na michuano ya Olimpiki.

Mark Cavendish

Zikiwa zimebaki siku tano kumalizika kwa michuano ya Tour de France, nyota wa mchezo huo, Mark Cavendish, raia wa Isle of Man, alitangaza kujitoa katika michuano hiyo na kudai kwamba anakwenda kujiandaa na michuano ya Olimpiki.

Mashabiki wengi wa nyota huyo na timu ya Dimension Data, walishangaa kuona anajitoa katika hatua za mwisho.

Mashabiki wa timu hiyo wakadai kuwa timu itashindwa kufanya vizuri kwa kuwa wachezaji wengine watakuwa wamevunjika moyo.

Hii ina maana kwamba Olimpiki aliipa nafasi kubwa kuliko Tour de France, lakini kwa kuwa ratiba ilikuwepo tangu mapema na alikuwa anajua kwamba itamalizika siku chache kabla ya kuanza kwa Olimpiki alitakiwa kutoshiriki.

Hata hivyo, nyota huyo mwenye umri wa miaka 31, aliwaomba radhi mashabiki kwa maamuzi magumu ambayo ameyachukua kuachana na timu yake zikiwa zimebaki siku tano michuano kumalizika.

Kutokana na hali hiyo, mashabiki kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii walianza kuishambulia michuano hiyo na kudai kuwa kuna baadhi ya wachezaji wamepoteza msisimko.

Fabian Cancellara

Tofauti ya Cancellara na Cavendish, ilikuwa ni siku moja, ambapo na yeye alitangaza kuachana na michuano hiyo zikiwa zimebaki siku nne kumalizika.

Naye alidai kwamba lengo la kujitoa kwenye Tour de France ni kwenda kujiandaa na michuano ya Olimpiki nchini Brazil.

Cancellara mwenye umri wa miaka 35, raia wa nchini Uswisi, aliwahi kushinda tuzo ya dhahabu mwaka 2008 katika michuano hii, lakini aliwaweka mashabiki wake njiapanda ambao waliamini kuwa ana uwezo wa kushinda msimu huu.

Hali hiyo pia iliwafanya mashabiki hao kuanza kuiponda michuano hiyo huku wengine wakidai ni bora wachukuliwe hatua kwa wale ambao wanafanya maamuzi ya kujitoa kabla ya mashindano kumalizika.

Kuna mshabiki wengine ambao walidai kuwa ni bora nyota hao wangeendelea na Tour de France na wangeshinda kuliko kukimbilia kwenye Olimpiki na wasifanikiwe kushinda.

Hivyo heshima ya nyota hao imeanza kushuka labda waje kufanya vizuri katika michuano hiyo ambayo wanaikimbilia nchini Brazili.

Hata hivyo, kwa upande wa Cancellara naye aliwaomba radhi mashabiki wake baada ya kutangaza kujitoa na akawaomba waendelee kumuunga mkono kwenye michuano hiyo mikubwa ya Olimpiki.

Nyota huyo anaamini kuwa atafanya vizuri katika Olimpiki kutokana na mazoezi ambayo anaendelea kuyapata pamoja na kile ambacho amekifanya katika Tour de France.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles