29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Agizo la RC Makonda lagonga mwamba

Paul Makonda
Paul Makonda

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

AGIZO la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda la kuipiga marufuku Kampuni za Ujenzi za Belmonte na Scol kupewa zabuni za kujenga barabara katika Mkoa wa Dar es Salaam limegonga mwamba.

MTANZANIA limebaini kuwa kampuni hizo hasa ile ya Belmonte, imeendelea kufanya kazi ya ujenzi wa barabara katika Manispaa ya Kinondoni.

Wakandarasi wa kampuni hiyo hivi sasa wanaendelea  kuweka viraka katika Barabara ya Morogoro,   Dar es Salaam, ambayo iliharibika kutokana na mvua kubwa mwanzoni mwa mwaka huu.

Pia kampuni hiyo inaendelea na ujenzi wa barabara ya Polisi Mabatini ambayo ilijengwa awali na baadaye kuharibika na hivi sasa imebomolewa ili kujengwa upya kwa gharama za kampuni hiyo.

MTANZANIA lilimtafuta Meya wa Manispaa hiyo, Boniface Jacob (Chadema) kutaka kujua sababu za kuendelea kuitumia kampuni hiyo licha ya Mkuu huyo wa Mkoa kuipiga marufuku.

“Kutoa tamko si utaratibu wa kazi bali barua na kwa kunukuu sheria na vifungu. Serikali haifanyii kazi taarifa za mitandaoni bali waraka, barua na miongozo rasmi,” alisema Jacob.

Mmoja wa wahandisi wa manispaa hiyo, akizungumza na MTANZANIA kwa sharti la jina lake lisiandikwe gazetini, alikiri kuwa awali barabara nyingi hazikufanyiwa utafiti wa kina kabla ya kupewa wakandarasi jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kuharibika siku chache baada ya kujengwa.

“Unajua maeneo mengi ya   Dar es Salaam hasa Manispaa ya Kinondoni kuna majimaji. Jambo hili awali halikubainika, kwa mfano, ile Barabara ya Polisi Mabatini ambayo ilijengwa kwa kiwango cha lami na ikakamilika,   baadaye maji yalianza kupanda juu na kuiharibu.

“Kuna wenzetu ambao wamechukuliwa hatua kutokana na hali hiyo kwa sababu hawakufanya utafiti.  Kulihitajika yawekwe mabomba maalumu kitaalamu tunaita ‘sub surface drainage’  kuvuna maji ya bahari yanayotoka chini yasifike juu ya barabara,” alisema.

Alisema manispaa hivi sasa ipo makini   kuhakikisha  hakuna barabara itakayojengwa bila kufanyiwa utafiti wa kina.

“Tutafanya utafiti kwa kushirikiana na mhandisi mshauri aliyeajiriwa na manispaa. Baada ya utafiti tutajua iwapo barabara hiyo inafaa kujengwa kwa kiwango cha lami au zege kama zile za mabasi ya mwendokasi.

“Ile ya mabatini itajengwa kwa kiwango cha lami kwa sababu tayari mabomba yamewekwa ingawa ni gharama kubwa,” alisema.

Meya Jacob alikiri kusimamishwa kazi kwa wahandisi wa manispaa hiyo na kwamba hivi sasa wanasubiri uamuzi wa kikao cha Kamati ya Fedha ambayo itapendekeza adhabu wanayopaswa kupewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles