24.6 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

Kauli ya JPM yaibua mazito

Mtzd Design Friday templateSiah.indd

Patricia Kimelemeta na Ramadhan Hassan, Dodoma

SIKU moja baada ya Rais Dk. John Magufuli  kutoa hotuba yake ya kwanza ya kukabidhiwa uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) mjini Dodoma juzi, kauli yake imewachanganya wasomi wa kada mbalimbali.

Pamoja na hayo,  Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) kimedai CCM bado inamuogopa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ndiyo maana makada na viongozi wakuu wa chama hicho walitumia muda mwingi kumshambulia na wengine wakimpiga vijembe.

Akizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti  Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari alisema ndani ya CCM hakuna ajenda nyingine inayojadiliwa zaidi ya kumtaja Lowassa, jambo linaloonyesha bado wanamuogopa kiongozi huyo.

Alisema ajenda ya vikao vyote tangu kuanza kwa mkutano mkuu wa CCM ni kumjadili Lowassa kwenye vikao vyake na kushindwa kujadili kwa kina mambo yanayohusu chama chao.

Mbali na hayo, Profesa Safari alisema kwa sababu hiyo chama hicho hakina muda wa  kujadili masuala yaliyotamkwa  na Rais Dk. Magufuli na chama chake kwa sababu hakuna jipya.

“Jambo hilo linaonyesha wazi joto la uchaguzi mkuu wa mwaka jana bado linaendelea kuwatoa jasho ndiyo maana wanaendelee kumtaja kila kukicha, alisema Profesa Safari huku akisisitiza kuwa Chadema kinafarijika kusikia CCM bado inamuogopa Lowassa na kiongozi huyo  bado ni tishio ndani ya CCM ndiyo maana tunaamini kiongozi tuliyempokea ni mtu makini.

“Tangu tumalize uchaguzi wa mwaka jana, ndani ya CCM hakuna ajenda nyingine zaidi ya kumjadili Lowassa, jambo linaloonyesha wazi Lowassa ni tishio kwao.

“Chadema tunafarijika kusikia  upepo wa Lowassa unaendelea kukitesa chama hicho “Bado anaendelea kuogopwa kutwa nzima juzi kila kiongozi akisimama ajenda kuu kumtaja kiongozi huyu,” alisema Profesa Safari.

Alisema katika hotuba yake, Rais Dk. Magufuli alidai kuwashughulikia makada wasaliti wa chama hicho ambao bado wapo jambo ambalo Profesa Safari anasema halitawezekana kwa sababu Chadema ina marafiki wengi ndani ya CCM kuliko anavyodhani.

Alisema katika chama hicho, kuna makada wengi ambao wana uswahiba na Lowassa na wengine wana uswahiba na viongozi wengine wa chama hicho ambao Rais Dk. Magufuli hawezi kuwajua wala kuwashughulikia.

Jina la Lowassa lilionekana kutawala ndani ya mkutano Mkuu wa CCM juzi ambapo kila aliyekuwa akitoa hotuba yake ajenda kuu ilikuwa lazima amtaje Lowassa, Sumaye, Chadema na Ukawa kwa ujumla.

Makada hao ni pamoja na Mwenyekiti mstaafu, Jakaya Kikwete, Katibu Mkuu mstaafu, Yusuph Makamba, Rais Magufuli, Fred Mpendazoe, Mgana Msindai ambao wamerudi CCM wakitokea upinzani. Wengine ni wenyeviti wa UDP, John Cheyo na wa TLP, Augustine Mrema.

LWAITAMA

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Josia Kibira University College cha Mjini Bukoba, Dk. Ezavel Lwaitama aaliponda kauli ya mwenyekiti mpya wa CCM, Rais Magufuli aliyedai kuwa siku ambayo wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM waliingia ukumbini wakiimba nyimbo ya ‘tuna imani na fulani’, kama angekuwa yeye angewapoteza, si kauli ya ustaarabu ikizingatiwa nafasi aliyonayo.

Kikwete aliimbiwa wimbo huo na wajumbe wa Halmashauri Kuu baada ya kuwapo taarifa za kukatwa jina la Lowassa katika kinyang’anyiro cha kugombea urais mwaka jana.

Dk. Lwaitama alisema Rais Magufuli hakupaswa kutoa kauli kama hiyo kwa sababu kumwamini mtu au chama ni jambo la hiari na  siyo lazima.

“Nimeshangaa kumsikia Rais Magufuli aliposema ‘siku ile Rais mstaafu Kikwete alipoingia ukumbini, kuna kundi la watu waliimba ‘wimbo wa tuna imani na fulani’ si ya kutolewa na kiongozi mkuu kama  yeye kwani ni kauli  inayoweza kuleta mfarakano, ,”alisema Dk. Lwaitama.

Aidha msomi huyo alisema Rais Magufuli anapaswa kuwa na uvumilivu kwa sababu siyo wote anaowaongoza wanamkubali, watakuwapo wa kumpinga, hivyo  hapaswi kutumia nguvu  kupambana nao.

Katika maoni yake, Dk Lwaitama alionyesha kumshangaza Rais  Magufuli kwa kauli yake kuwa watendaji wa Serikali wote ni waajiriwa wa CCM.

Alisema  mtendaji mkuu wa Serikali hawezi kuwa na mipaka ya kuabudu chama anachokitaka, bali ni uamuzi wake wa kuamini chama kipi kinachofaa aweze kukiunga mkono ilimradi asivunje sheria.

“Rais ameshindwa kutenganisha madaraka ya Serikali na chama, kwa sababu ukiwa mtendaji haufungwi kuabudu chama unachokitaka, bali ni uamuzi  binafsi,” alisema.

Alisema  kama ndiyo hivyo, hakuna haja ya kuwapo uchaguzi huru na wa haki kwa sababu CCM ikishinda watendaji wote ni waajiriwa wao.

“Tunapaswa kujifunza demokrasia kwa undani wake ili kila mmoja aweze kuchagua kitu anachokitaka na siyo kulazimishwa, hii ni hatari inaweza kusababisha nchi kwenda kubaya, tunapaswa kukemea ili tutoke kwenye giza,”alisema Dk. Lwaitama.

BANA

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk.Benson Bana amesema uamuzi wa Rais Magufuli kufikiri kuondoa makamanda na chipukizi ndani ya chama hicho  ni mzuri kwa sababu hawana tija katika  kipindi hiki.

Alisema kipindi kilichopita ambacho wananchi walikuwa wameshikamana kwa ajili ya kupigania uhuru, nafasi hizo zilikuwa za lazima kwa ajili ya kuhamamisha vijana kuwa wazalendo na nchi kuondoka mikononi mwa wakoloni, lakini hivi sasa mambo hayo yamepita.

“Katika kipindi hiki nafasi ya makamanda na chipukizi hazina nafasi kwa sababu tupo kwenye mfumo wa vyama vingi ambavyo kila mmoja ana haki ya kuingia kwenye chama anachokitaka.

“Hatuwezi kuruhusu kila chama kianzishe chipukizi au makamanda wake, itakua hatari,”alisema Dk. Bana.

Alisema mkakati uliopo ni kuangalia namna ya kukisafisha chama kiondoke kwenye mtazamo wa uchaguzi wa rushwa na kuingia kwenye uchaguzi huru na haki, jambo ambalo linaweza kusaidia kupata viongozi bora.

SEMBOJA

Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Dk.Hajji Semboja amesema siasa ya Tanzania ni ngumu hauwezi kuitafsiri kwa maneno kwa sababu mfumo mzima wa  utendaji ndani ya chama na serikali kwa ujumla una matatizo mbalimbali yakiwamo rushwa, ufisadi na uvivu.

Alisema kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli anapaswa kuangalia Katiba ya CCM kabla ya kuanza kukisafisha na kashfa ya rushwa kama anavyoendelea kufanya serikalini.

“Hivi sasa Rais Magufuli anasafisha Serikali, tunaamini safisha safisha hii itakwenda hadi ndani ya chama ili kuondoa uchafu ambao ulichangia kukidhohofisha,” alisema.

DODOMA

hABARI kutoka mkoani Dodoma, zinasema baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCCM uliomalizika juzi, waliduwazwa na Rais Dk. John Magufuli baada ya Rais Dk. Magufuli kuamua kuibakisha sekretarieti nzima ya Mwenyekiti mstaafu, Jakaya Kikwete.

Ratiba ya CCM ilikuwa inaonyesha kuwa jana ndiyo ilikuwa siku ambayo Dk.Magufuli angekutana na wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC ) kutangaza majina ya wana CCM watakaounda sekretarieti mpya, baada ya ile ya mwanzo inayoongozwa na Katibu Mkuu wao, Abdulrahman Kinana, kuomba kujiuzulu.

Kitendo cha Dk. Magufuli kutangaza kwamba ataendelea na Kinana na sekretarieti yake hakikutarajiwa na wajumbe wengi wa mkutano mkuu.

Baadhi ya wajumbe hao waliiambia MTANZANIA kuwa Rais Dk.Magufuli ameonyesha ni kwa jinsi gani anataka kuona mambo yake yanakwenda kama anavyopanga.

“Ratiba tuliyogawiwa ilionyesha kesho (jana) ndiyo ingekuwa siku ambayo Dk.Magufuli angetangaza Katibu Mkuu   na wajumbe wote wa sekretarieti.

“Lakini cha kushangaza hakutaka suala hilo lisubiri na badala yake aliamua kuendelea na Kinana na walio chini yake wote.

“Tumekuwa tukishuhudia mwenyekiti mpya wa chama anapoingia baada ya kupitishwa na wajumbe wa mkutano mkuu, siku inayofuata ndiyo tunasikia anatangaza jina la Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Bara, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar  na wakuu wa idara nyingine wa sekretarieti mpya ikiwamo Katibu wa Itikadi na Uenezi na Katibu wa Uchumi na Fedha.

Mmoja wa wajumbe wa sekretarieti hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliiambia MTANZANIA kwamba alitamani awe kando lakini anaona alichokuwa akifikiria ni tofauti na Dk.Magufuli alivyofikiria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,745FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles