25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Boris Johnson anayefananishwa na Donald Trump

Boris Johanson (kulia) na Donald Trump (kushoto)

SIASA zinastaajabisha kwa yasiyotarajiwa kama ilivyotokea nchini Uingereza, badala ya wanasiasa kutafuta uongozi, madaraka yaliwatafuta yakasababisha kuundwa serikali mpya ya Waziri Mkuu Theresa May.

Haikutarajiwa Boris Johson kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje licha ya kujiondoa kwake kwenye kinyang’anyiro kumwezesha Theresa May apite bila kupingwa katika mchakato wa chama cha Conservative.

Boris anayefahamika zaidi kama ‘Bojo’ katika kampeni za kubaki au kujiondoa EU alishabikia kujiondoa sasa amepewa rungu kushughulikia mataifa mengine, yaliyoshikwa kihoro kwa uteuzi wake kutokana na tabia yake ya utata akifananishwa na Donald Trump ingawaje mwenyewe anapinga dhana hiyo.

Duniani wawili wawili, kwani Boris na Trump hawafanani kwa hulka tu bali pia wajihi na kauli tata zisizojali diplomasia.

Wengi hawampendi Bojo kisiasa wakidai ni mzushi aliyeshawishi Uingereza ijitoe EU wakitamani kuteuliwa kwake kuwe jinamizi la usingizini lakini ni jambo halisi.

Boris alitumia nafasi yake akiwa mwandishi wa safu magazetini kabla hajawa Meya wa London kuwaponda wanasiasa asiowapenda, aliwahi kumtungia shairi Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan kwamba alikuwa na siasa za kujamiana na mbuzi, akamsifia Bashar Assad wa Syria kwa kuwapa kisago IS licha ya kukandamiza raia wake.

Mwaka 2008 Boris aliukwaa Umeya wa London kupitia Conservative baada ya Nick Boles kujiondoa akiungwa mkono na David Cameron alishinda kwa asilimia 53.2, alijiuzulu Ubunge wa Jimbo la Henley na kuwakera wapiga kura wa jimbo hilo waliomwita msaliti aliyewatosa.

Aliwahi kuwakera Wachina alipoenda kupokea mwenge wa Olimpiki mwaka 2008 kwa mavazi yasiyozingatia diplomasia, kwa kuwa baada ya China nchi yake ndiyo iliyofuatia katika zamu ya michezo hiyo katika jiji la London.

Bojo alidai kuwa mshahara wa Umeya wa pauni 140,000 kwa mwaka haumtoshi hivyo hakuacha kuandika safu katika gazeti la Telegraph, akijipatia pauni 250,000 zaidi alizotakiwa kuchangia jamii asilimia 5.

Lakini aligoma kufanya hivyo, akidai kuwa ni sawa na punje kwa kuku akiwakera wengi kwani kipato hicho ni mara kumi kuzidi anachopata mfanyakazi wa kawaida wa Uingereza.

Akajiteua kuwa msimamizi mkuu wa mamlaka ya polisi akimlazimisha Kamishna wa polisi kujiuzulu.

Alishutumiwa kwa kuwa na nyumba ndogo mbili na kumchagua swahiba wake Veronica Wadley, Mhariri wa jarida alilowahi kufanyia kazi kuwa Mkuu wa Baraza la Usimamizi wa Maendeleo ya Sanaa licha ya kutokuwa na uwezo wa kazi hiyo, akafuja kasma kwa matumizi ya usafiri wa kazi wa matanuzi na kumsukumia zigo hilo Naibu Meya aliyelazimika kujiuzulu.

Kama alivyo pacha wake Trump kwa hulka za matamshi ya kukera Bojo aliwahi kuhudhuria kongamano la Kiislamu la dunia lililohusu uchumi, akiwa na Waziri Mkuu wa Malaysia Najib Razak, akasema wanawake wa Malaysia huhudhuria elimu ya juu ili kujitafutia wanaume wa kuwaoa akiwakasirisha na kuwaghadhabisha.

Baada ya kumaliza kutumikia Umeya alirudi Bungeni akichaguliwa kuwakilisha Jimbo la Uxbridge na South Ruislip akitarajia kumrithi Cameron kuongoza chama na kuwa Waziri Mkuu lakini hakufanikiwa. Wakati wa kuelekea kura ya maoni ya UK kujiondoa EU alimwambia Obama aache kiherehere cha kuingilia yasiyomhusu kwanza yeye ni Mkenya si Mmarekani!

Usidhani kuwa anachukiwa na wote kwa hulka yake, hapana kuna wanaovutiwa naye kama wanavyovutiwa na Donald Trump kwa makeke ya kutamka ukweli mchungu bila kuupamba kidiplomasia, ingawaje kihoro mithili sinema ya kutisha kilichokuwa kikiogopewa endapo angemrithi Cameron na Trump kushinda Marekani kwa sasa hakipo.

Lakini cheo alichokabidhiwa Boris kinachokanganya msimamo wake uliotofautiana na Bosi wake Theresa kuhusu EU, ni kama mtego utakaommaliza mwanasiasa huyu mwenye uraia wa Uingereza na Marekani kwani alizaliwa New York na wazazi wake Waingereza.

Muundo mpya wa Serikali ya Uingereza una wasimamizi mahususi wa mchakato wa kujitoa EU na mahusiano ya kiuchumi kimataifa. Hiyo inampunguzia madaraka Boris atakayeshughulika zaidi nje ya nchi akiwajibika kwa lolote litakalotatanisha mchakato wa Uingereza kujitoa kutoka EU. Tusubiri tuone pacha wa Donald Trump atakavyojibainisha kisiasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles